Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaodaiwa kuvamia Hifadhi ya Iluma matatani

Wananchi walioondolewa kwenye eneo la hifadhi ya jamii ya Iluma iliyopo Kijiji cha Mbuyuni Kata ya Minepa, Wilaya ya Ulanga. Picha Hamida Shariff, Mwananchi

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Ulanga ameagiza wananchi wote waliovamia maeneo ya hifadhi kuondoka haraka na kueleza kwamba Serikali itaendelea kutunza na kuyalinda maeneo yote ya hifadhi.

Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Julius Ningu amewapa wananchi waliovamia hifadhi ya jamii ya Iluma, iliyopo Kijiji cha Mbuyuni, Kata ya Minepa wilayani Ulanga, siku tatu kuhama kwa hiari.

Pia, Ningu amewataka askari wanaolinda hifadhi hiyo kutotumia nguvu wanapowaondoa wananchi hao.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatano Januari 15, Ningu amesema wananchi hao walianza kuvamia hifadhi hiyo Agosti mwaka jana na kuhamia kwenye hifadhi ambayo inapakana na Hifadhi ya Mwalimu Nyerere.

“Wengi wao ni wale waliondolewa kutoka Hifadhi ya Misitu ya Tawa iliyopo vijiji vya Namhanga, Ilaguha na Peramenja,” amesema Ningu.

Amesema kabla ya kutoa agizo hilo, alitembelea eneo hilo na kukuta wananchi wakiwa wamejenga vibanda vya miti na nyasi, akawaeleza hilo ni eneo la hifadhi wanapaswa kuondoka kwa kuwa hakuna anayeweza kubadili matumizi yake bila idhini ya Rais.

Hata hivyo anasema wananchi hao wanaweza kuhamia katika maeneo mengine wilayani humo lakini kwa kufuata sheria na kuepuka kuingia kwenye hifadhi na wahame kwa hiari ili kuepuka usumbufu.

Aidha, Ningu amesema uvamizi huo umeleta uharibifu mkubwa kwenye hifadhi ya Mwalimu Nyerere, mbao zaidi ya 80 zimekamatwa. “Wenye mbao wamekimbia. Pia baadhi ya watu wanatapeli wananchi kwa kujifanya madalali wa kuuza ardhi ya hifadhi, hili haliwezi kukubalika,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Awali, Mwenyekiti wa kijiji cha Mbuyuni, Raphael Makindamba, alikiri kuwepo kwa uvamizi na kusema baadhi ya wananchi wameshaanza kuondoka kwenye hifadhi hiyo, huku wengine wakiwa wakirejea kijijini kutafuta maeneo ya wazi kwa ajili ya makazi.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa baadhi ya wananchi walioamriwa kuondoka wameomba kupewa muda zaidi ili kutafuta makazi mengine ya kuishi.