Mtaalamu ataja chanzo wananchi kuvamia hifadhini

Muktasari:
Wakati Taifa likiendelea kushuhudia migogoro ya mpaka kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, mtaalam wa upimaji ardhi ametaja kukosekana kwa alama za mpaka kati ya hifadhi na vijiji jirani kuwa chanzo cha migogoro hiyo.
Tarime. Wakati Taifa likiendelea kushuhudia migogoro ya mpaka kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, mtaalam wa upimaji ardhi ametaja kukosekana kwa alama za mpaka kati ya hifadhi na vijiji jirani kuwa chanzo cha migogoro hiyo.
Akizungunza na waandishi wa habari Aprili 10, 2023 akiwa eneo la kazi ya kuweka vigingi vya mpaka kati ya vijiji saba vya Wilaya ya Tarime vinavyopakana na Hifadhiya Taifa ya Serengeti, Ofisa Mpima Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Sorwa amesema kukosekana kwa alama ya mipaka kunasababisha wananchi kuingia na kufanya shughuli za kibinadamu ndani maeneo ya hifadhi bila kujua.
“Kukosekana kwa alama ya mipaka siyo tu inasababisha wananchi kushindwa kufahamu mipaka ya vijiji vyao, bali pia hata maofisa uhifadhi nao hujikuta wakipata shida kutambua mipaka ya hifadhi,” amesema Sorwa
Ametoa mfano wa mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji vya Kata ya Kwehancha wenye urefu wa karibia kilometa 9 ambao haukuwa na kigingi cha alama ya mpaka.
“Ilikuwa ni vigumu hata kwa maofisa wa hifadhi wenyewe kujua mipaka yao kutokana na kukosekana kwa vigingi vya alama ya mipaka,”amesema Sorwa
Kuhusu vigingi vya alama vinavyosimikwa katika mpaka wa hifadhi na vijiji jirani, mtaalam huyo amesema Serikali inazingatia GN namba 235 ya mwaka 1968 inayokubalika kwa pande zote, yaani Serikali, hifadhi na wananchi.
“Tayari tumesimika vigingi 86, sawa na asilimia 75 ya vigingi 162 vinavyosimikwa katika eneo la mpaka wa vijiji na hifadho lenye urefu wa kilometa 29. Kazi hii inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 10 hadi 12 zijazo,”amesema Sorwa
Kazi hiyo iliyoanza Machi 27, 2023 imekumbana na changamoto ya upinzani kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kegonga na kulazimika kusitishwa kwa muda wa wiki moja kabla ya kuanza tena.
Kwa mujibu wa Sorwa, kazi inayotekelezwa siyo kuweka vigingi vya alama ya mpaka pekee, bali pia ni kupima eneo la buffer zone, kulichora na kulikabidhi kwa mamlaka husika kwa ajili ya matumizi ya vijiji kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi.
“Nawasihi wananchi kuheshimu mipaka kwa sababu kazi hii itawanufaisha kupitia uwekezaji na shughuli zingine za kijamii zinazozingatia uhifadhi wa ardhi, mazingira na utalii," amesema mtaalam huyo wa ardhi
Diwani wa Kata ya Kwehancha inayoundwa na vijiji vya Karakatonga, Gibaso na Nyabirongo, Ragitha Mato amesisitiza umuhimu wa vigingi vya mpaka kusimikwa kwa kuzingatia GN ya mwaka 1968 huku akitaja baadhi ya alama muhimu kuwa ni Mto Mara, Kijito Swetu na tindiga la Gongora.
“Mimi ni diwani wa kata hii tangu mwaka 2,000; sihitaji kupingana na Serikali lakini naomba vitu vya asili vilivyoko kwenye GN ya mwaka 1968 ndivyo vitumike kuweka vigingi,” amesema Mato
Amesema viongozi wa vijiji vya kata hivyo kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali tayari waliweka utaratibu wa kutambua mipaka hiyo na kuweka sheria ndogondogo kuzuia watu kuingia ndani ya hifadhi kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo uwindaji.
“Tumekubaliana eneo la buffer zone linalorejeshwa kwa wananchi litumike kufuga nyuki, kulisha mifugo na uwekezaji kwenye miradi ya uhifadhi na utalii,” amesema Diwani Mato