Wanaodaiwa kutapeli wastaafu, waendelea kusota rumande

Muktasari:
- Rwechungura na wenzake watatu wanakabiliwa na mashitaka 49 yakiwemo ya kutapeli wastaafu na kujipatia Sh5 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Dar es Salaam. Serikali imedai upelelezi wa kesi ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na kutapeli wastaafu, inayowakabili wakazi wanne wa Kagera na Mwanza, bado haujakamilika.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Eradius Rwechungura (43) maarufu Rwamakala na mkazi wa Kiseke- Mwanza; Heri Kabaju (37), maarufu Babylon ambaye ni mchuuzi wa samaki na mkazi wa Rwamisheni mkoani Kagera, Abdurahim Karugila (42), maarufu Obra ambaye ni dereva na mkazi wa Kahororo- Kagera pamoja na Eradius Apornary (22) ambaye ni wakala na mkazi wa Kashai Rwamishenyi mkoani Kagera
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 49 yakiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh5 milioni.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Januari 31, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.
Hata hivyo, leo Jumatano, Aprili 9, 2025 kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na wakili wa Serikali, Aron Titus amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na hivyo, wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 22, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashitaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana.
Kati ya mashitaka 49 yanayowakabili washtakiwa hao, 23 ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, 13 kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, 11 kujiwasilisha kwa utambulisho wa mtu mwingine na shitaka moja ni kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha walizozipata kwa njia ya udanganyifu kwa kuwalaghai watu kuwa watawatafutia kazi.
Rwechungura na wenzake, pia wanadaiwa kuwapigia simu watu mbalimbali na kujitambulisha kuwa wao ni Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Tunduma, Bukoba, Momba na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa madai kuwa watawasaidia kupata kazi ya ualimu, jambo ambalo walijua kuwa ni uongo.
Vilevile , mshtakiwa Kabaju anadaiwa kujitambulisha kama Mkuu wa Mkoa kwa Christopher Msemwa, kuwa anahitaji kufanya uhakiki wa taarifa zake za utumishi, pamoja na kujitambulika kama ofisa utumishi kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa mstaafu Anuciata Mwageni, wakati akijua ni uongo.
Washtakiwa wengine wanadaiwa kujitambulisha kuwa wao ni ofisa kutoka Hazina kitengo cha wastaafu, maofisa rasilimali watu kutoka wilaya ya Njombe, Bukoba na Kahama, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Katika kesi hiyo ya msingi, washtakiwa wadaiwa kwa pamoja kati ya Oktoba Mosi na Desemba 31, 2024 katika eneo na mkoa usiojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliendesha genge la uhalifu lenye lengo la kutapeli watu tofauti na kujipatia Sh5 milioni.
Shitaka la pili, tatu ni kujiwasilisha kwa utambulisho wa mtu mwingine linalomkabili Rwechungura pekee yake ambapo anadaiwa kati ya Oktoba 4 na Desemba 12, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutumia simu iliyosajiliwa kwa jina la Benetson Rwenyagira na Rukia Kombo, alijitambulisha kuwa yeye ni ofisa kutoka wilaya ya Bukoba na Kahama kwa Eliberth Kaliman na Filberth Mashim, wakati akijua kuwa ni uongo.
Shitaka la nne hadi la tisa, lilifanywa na Kaguja kwa kujiwasilisha kuwa ni Ofisa kutoka PSSSF kwa Anunciata Mwageni.
Vilevile Kaguja anadaiwa kujiwasilisha kuwa ni Ofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata taarifa za mwajiriwa Christopher Msemwa, na pia alijitambulisha kuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa Jesca Kibena.
Pia, inadaiwa Kabuja alijiwasilisha kuwa ni Ofisa Rasilimali watu kutoka ofisi ya Halmashauri ya Njombe mjini kwa Rustica Kayombo na Upendo Nsellu pia alijiwasilisha kama Muweka Hazina wa Idara ya Pensheni kwa Lucas Nzota, huku akijua kuwa si kweli.
Katika shitaka la 10 hadi 12 linadaiwa kufanywa na Rwechungura kwa kujiwasilisha kuwa yeye ni Ofisa Takwimu kutoka Halmashauri ya Tunduma Mjini kwaTupilike Mbwile, pia alijitambulisha kuwa ni Ofisa mradi kutoka Halmashauri ya Momba mjini kwa Elistulida Mwakyusa na Ofisa rasilimali watu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe kwa Emmanuela Mwambichi.
Mashitaka 13 ni ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na inadaiwa walikuwa wakitumia laini zilizosajiliwa kwa majina ya Bazil Katono, Happyness Jems, Aziza Ramadhani, Royce Frenki, Sajda Abed, Valence Rwezaula, Ben Mhimbira, Benetson Rwenyagira na Sabitina Ally.
Katika mashitaka 23 ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu washtakiwa, wanadaiwa kujiwasilisha kwao kwa uongo na kujipatia fedha jumla ya kiasi cha Sh5 milioni kutoka kwa watu waliojitambulisha kwao, wakiwaahidi kuwa wangewasaidia kupata kazi ya ualimu, jambo ambalo ni uongo.
Vile vile wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha wakati wakijua fedha hizo ni za makosa tangulizi ambayo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.