14 wapandishwa kizimbani tuhuma za utapeli wa ajira

Baadhi ya watu wanaotuhumiwa kufanya utapeli wakielekea katika chumba Mahakama ya Mwanzo mjini Morogoro (Nunge) kusikiliza mashtaka yao mkoani hapa. Picha na Juma Mtanda
Muktasari:
- Watu 14 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Mjini Morogoro (Nunge) kwa tuhuma ya kujifanya maofisa wenye mamlaka ya kutoa ajira, na kuwakusanya vijana 48 kutoka sehemu mbalimbali nchini na kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Morogoro. Watu 14 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Mjini Morogoro (Nunge) kwa tuhuma ya kujifanya maofisa wenye mamlaka ya kutoa ajira na kuwakusanya vijana 48 kutoka sehemu mbalimbali nchini, na kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Aprili 4, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Beatha Richard ambapo walikanusha mashitaka hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Aprili 10 wakati kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa.
Washtakiwa hao ni Kenedy Mwanza, Maghembe Nyorobi, Mashaka Jajiro, Lasoy Lazier, Sahenga Sokala, Hajard Habibu, Zaina Habibu, Elenuru Moleli, Ericky Francis, Baraka Ally, Daud Joshua, Anitha Elirehema, Donard Edward na Dickson Akyoo,
Mkuu wa Operesheni wa Wilaya ya Morogoro, Geoffrey Kalugendo ameieleza mahakama kuwa Aprili 1,2025, alipokea simu kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama kumjulisha uwepo wa malalamiko ya kutapeliwa.

Malalamiko hayo yalikuwa ni kutoka maeneo na mikoa mbalimbali ambapo wananchi walidai kutapeliwa kwa njia ya mtandao, ambapo wananchi wawili walitafutwa kwa simu na upelelezi wa madai yao ulianza mara moja.
Uchunguzi huo ulifanikisha kukamatwa kwa vijana 48 wakiwemo watuhumiwa 14 waliofikishwa mahakamani leo Aprili 4.
“Mmoja wa wananchi waliopigiwa simu na Kamanda Mukama ni mwananchi kutoka mkoa wa Simiyu aliyeeleza kuwa kijana wake amemjulisha kuwa amepata ajira Morogoro na mzazi huyo anatakiwa atume Sh5 milioni,”amesema.
Fedha hizo zilikuwa zimwezeshe kijana ahudhurie mafunzo kwa vitendo, lakini hakuweza kutuma fedha hizo kwa sababu mzazi alitaka kwanza kuwasiliana na kijana wake moja kwa moja na sio mmoja wa kiongozi ilhali kijana wake ana simu.
Akitoa ushahidi wake, Karugendo aliieleza mahakama kuwa malalamiko mengine ni kutoka kwa mwananchi wa Mkoa wa Arusha ambaye kijana wake, Erick Onesmo (19) alielezwa kuwa amepata ajira ya kufanya kazi hotelini nchini Dubai.
Kulingana na shahidi huyo, kijana huyo alielezwa kuwa angelipwa mshahara wa Sh2 milioni kwa mwezi baada ya kufuzu mafunzo kwa vitendo ambapo anapaswa kulipia Sh5.8 milioni.
Katika uchunguzi wa Jeshi la Polisi baada ya kuwakamata vijana 64 waliokuwa katika mchakato huo wa kutapeliwa na wote katika eneo la Azimio Kihonda ambapo hakuna hata mmoja anayetokea mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Karugendo, vijana hao hulipa Sh150,000 kwa uongozi na kupatiwa jarida la “Milionea Papo Hapo” na baada ya muda vijana hao huwalazimisha wazazi wao kutuma fedha kwa viwango tofauti kwa uongozi kwa mategemeo kupata ajira hoteli za Zanzibar, Dubai, Malaysia, Kenya na nchi nyingine.
Mbali na ushahidi wake, lakini Karugendo amewasilisha vitabu viwili (note book) mbili, jarida la “milionea papo hapo” na kueleza kiongozi namba moja wa viongozi hao bado anaendelea kuhojiwa kutokana na uzito wa mashitaka yanayowakabili na uchunguzi utakapokamilika ataunganishwa na wenzake.
Shahidi mwingine ambaye ni Diwani wa viti maalumu Kata Malula wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Rosemary Joseph, alieleza kuwa mtoto wao, Erick Onesmo (19) alikutana na mmoja wa viongozi hao akiwa katika mafunzo kwa vitendo ya usimamizi wa hoteli huko Kibaha mkoani Pwani.
Rosemary ameeleza kuwa akiwa Kibaha alikutana na mwanamke ambaye alimuomba amuandalie chakula aina ya Pizza na baada ya kukiandaa aliomba namba ya simu ya Erick Onesmo na kumpatia Sh7,000 na kumuahidi kumtafutia kazi, na siku tatu baadaye Erick alipigiwa ili kwenda Morogoro ambako kuna kazi na kutakiwa kuwa na Sh150,000 kwa ajili ya usaili.
“Baada ya Erick kutupa taarifa za kutakiwa Morogoro tulimpatia Sh150,000 na siku chache akiwa Morogoro tuliongea naye kwa njia ya simu kupitia simu ya viongozi wake na kutuambia kuwa yeye ni mmoja wa vijana sita wamepita kwenye usaili”.
Shahidi huyo aliongeza kusema kuwa waliambiwa ameshika nafasi ya kwanza hivyo anatakiwa alipe Sh5.8 milioni kwenda Dubai kufanya kazi ambayo kwa mwezi atalipwa Sh2 milioni, lakini walishtuka na kushindwa kuamini jambo hilo.
Rosemary ameeleza kuwa baada ya kushtuka na kuona kuna dalili za utapeli aliomba namba ya simu ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro na kuwasilisha malalamiko na Jeshi la Polisi na kufanikisha kumuokoa mtoto wake pamoja na vijana wengine.