Wananchi waiangukia Serikali ubovu wa barabara

Barabara ya katanini ambayo wananchi wameomba serikali kuijenga ili kurahisisha shughuli za usafirishaji na usafiri.
Muktasari:
- Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara ya Katanini ili kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Moshi. Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara ya Katanini ili kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ombi hilo wamelitoa leo, Alhamisi Januari 18, wakati wakizungumza na Mwananchi Digital, ambapo wamesema wameahidiwa kujengewa barabara hiyo tangu mwaka 2019, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika, hali inayowatesa hasa kipindi cha mvua.
"Barabara yetu shida kubwa haipitiki wakati wa mvua, tumekuwa tukipewa ahadi za ujenzi wa barabara hii kwa zaidi ya miaka mitano sasa lakini hakuna kilichofanyika, tunaomba Serikali itusaidie ili kuwezesha barabara hii kupitika na kuchochea ukuaji wa uchumi," amesema Charles Noah.
Ortensia Lucas amesema ubovu wa barabara hiyo umewafanya wenye magari kuyalaza mjini wakati wa mvua kutokana na makorongo yaliyosababishwa na mvua hivyo barabara kutopitika.
"Kupita kwenye hii barabara wakati wa mvua ni shida, hadi tumefikia kuiita ya ng'ombe, tunashindwa kwenda Kanisani na hata watoto wanachelewa shule kutokana na utelezi na ubovu wa barabara hii," amesema.
Naye Cyril Mwacha amesema: “Changamoto hii ya barabara ni kubwa, kama mnavyoiona ni mbovu, mbaya na shughuli za usafiri na usafirishaji ni ngumu, tunaiomba Serikali iangalie barabara hii, kwani miundombinu ni mibovu hakuna hata mitaro na mvua zinaponyesha maji yanaenda hadi nyumbani kwa watu"
Akizungumza Meneja Wakala wa Barabara za vijijini na Mjini (Tarura) Wilaya ya Moshi, Orota Africano amesema barabara hiyo imetengewa zaidi ya Sh200 milioni ambapo itajengwa kwa kiwango cha changarawe.
"Barabara ambayo wananchi wanaizungumzia, ina urefu wa kilometa 1.37 na mwaka huu wa fedha 2023/2024 tunayo kwenye mpango wetu, tayari mkandarasi amepatikana na ameshasaini mkataba na kazi itaanza muda wowote ndani ya wiki mbili," amesema Africano.
"Tutajenga barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe na mitaro ya maji, kimsingi barabara zote za pembezoni hapa manispaa tunao mpango wa kuzitengeneza," amesema.