Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri Trump, Zelensky kukaa viti vya mbele Vatican

Sababu halisi iliyomfanya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kupata nafasi ya kukaa mstari wa mbele katika mazishi ya Papa Francis imefichuliwa, ikikanushwa uvumi kuwa waandaaji walitaka kumchokoza Donald Trump.

Taratibu za kidiplomasia zilivunjwa ili kumhamisha Rais huyo wa Ukraine kutoka sehemu yake ya awali, ambayo ilipaswa kuwa nyuma zaidi, hadi kwenye kiti maarufu nafasi 11 kutoka alipokuwa amekaa Trump.

Vatican haikukanusha kuwa taratibu zilivunjwa, ambapo msemaji Matteo Bruni aliambia gazeti ‘The Telegraph’ la Uingereza: "Naamini walijaza nafasi iliyokuwa wazi."

Haijulikani ni nani aliyekosa nafasi dakika za mwisho katika siku hiyo ya huzuni, hali iliyompa Zelensky nafasi ya mbele, lakini kulikuwapo na tetesi kwamba huenda ilikuwa familia ya kifalme ya Uholanzi.

Uvumi huo ulijitokeza baada ya Mfalme Willem-Alexander na Malkia Máxima wa Uholanzi kuonekana leo mapema, si Vatican, bali katika mji wa Doetinchem, Uholanzi, wakisherehekea sikukuu ya kitaifa iitwayo ‘Siku ya Mfalme’.

Mamia ya watu waliokusanyika, wakiwa wamevaa nguo za rangi ya machungwa, walipokea familia hiyo ya kifalme katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Mfalme, ambaye leo atatimiza miaka 58.

Waliandamana na binti zao, Malkia wa baadaye, Princess Catharina-Amalia mwenye miaka 21, na Princess Alexia mwenye miaka 19.

Wakati huohuo, katika Jiji la Vatican, viongozi wa dunia akiwamo Sir Keir Starmer na Emmanuel Macron walitawanywa katika mpangilio wa viti ulioelezwa kuwa mpango kabambe wa kudhibiti viongozi wenye jeuri kubwa.

Na ingawa kulikuwapo na tetesi kuwa Trump angekuwa mstari wa tatu jambo ambalo angeliangalia kama dharau, alijikuta katikati kabisa mbele kwa ajili ya ibada hiyo.

Mbali na Trump na mkewe Melania, watu wengine mashuhuri mstari wa mbele walikuwa Rais wa Ireland, Michael Higgins, Volodymyr Zelensky wa Ukraine  aliyefanya safari ya ghafla kuhudhuria na Javier Milei wa Argentina, aliyeketi nafasi ya juu zaidi.

Milei alipata kuwa karibu zaidi na jeneza la Papa, kwa kuwa Francis alikuwa mzaliwa wa Argentina, ambako alizaliwa kama Jorge Mario Bergoglio Desemba 1936.

Nafasi iliyofuata ilichukuliwa na Italia, kwa kuwa Papa pia ni Askofu wa Roma. Rais wa Italia Sergio Mattarella na binti yake Laura walikalia viti karibu na kiongozi wa Argentina. Moja kwa moja nyuma yao aliketi Waziri Mkuu wa Italia, Georgia Meloni.

Bega kwa bega na Rais Mattarella walikuwa viongozi wa mataifa kama Albania na Angola.

Kwa upande mwingine, Prince William alikaa bega kwa bega na Olaf Scholz, Kansela wa Ujerumani, mistari miwili nyuma ya Javier Milei na dada yake Karina Milei, Katibu Mkuu wa Urais wa Argentina.

William alihudhuria kwa niaba ya baba yake, Mfalme Charles III, mkuu wa nchi wa Uingereza.

Kwa upande wa Sir Keir, ilimbidi akubali kukaa mistari kadhaa nyuma pamoja na mkewe Victoria, kama kiongozi wa serikali badala ya mkuu wa nchi, hali iliyomkumba pia Ursula von der Leyen, Rais wa Tume ya Ulaya.

Wazo kwamba Uingereza na mataifa mengine yalipuuzwa au kuwekwa nyuma zaidi katika mpangilio huo halina uzito mkubwa kwa kuwa waandaaji wa Vatican walijitahidi kutumia diplomasia katika kupanga vipaumbele.

Mpangilio wa viti wa Vatican kwa wageni mashuhuri waliokaa moja kwa moja mbele ya makasisi waandamizi, ulizingatia wafalme walioko madarakani na marais kabla ya mawaziri wakuu.

Hata hivyo, kulikuwapo na utaratibu zaidi wa kipaumbele. Licha ya kutangaza Kilatini na Kiitaliano kuwa lugha rasmi, Vatican ilipanga viti kwa kufuata mpangilio wa alfabeti ya Kifaransa.

Uamuzi huu ulitokana na historia ya nguvu za Ufaransa barani Ulaya, ambako Kifaransa bado kinachukuliwa kama lugha rasmi ya diplomasia ya Ulaya.

Hivyo, Marekani inakuwa ‘les États-Unis’; Ujerumani inakuwa ‘Allemagne’, na Uingereza inashushwa nyuma kama ‘Royaume-Uni’.

Hii inaeleza ni kwa nini Trump alijikuta mbele kabisa miongoni mwa marais takribani 50, huku wakuu wa serikali kama Sir Keir wakijikuta nyuma kwenye viti vya ‘bei chee’.

Pembeni mwa Milei, alikuwapo Joan-Enric Vives i Sicilia, kasisi wa Kikatoliki na Co-Prince wa taifa dogo lisilo na bandari la Andorra, akiwa bega kwa bega na Bajram Begaj, Rais wa Albania, na Joao Lourenço, Rais wa Angola.

Hata hivyo, haielezei kwa nini Rais Zelensky alipata nafasi ya mstari wa mbele licha ya kuwa jina la Ukraine halibadiliki kwa Kifaransa.

Yeye na mkewe waliketi kati ya Ufaransa na Ireland, katika kile kilichoonekana kama uvunjaji wa sheria za mpangilio wa viti.

Alipoulizwa na gazeti ‘The Telegraph’, msemaji wa Vatican Matteo Bruni hakukanusha hali hiyo. Alisema: "Ninaamini walijaza nafasi iliyokuwa wazi."

Msimamo wa marehemu Papa kuhusu Ukraine ulikosolewa kabla ya kifo chake, kwani alipendekeza Ukraine ‘iwe na ujasiri wa bendera nyeupe’ na kutafuta amani na Russia, jambo lililokataliwa na Ukraine. Papa Francis pia hakuwahi kumlaumu moja kwa moja Vladimir Putin kama mchochezi wa vita hivyo.

Hakukuwa na upendeleo maalumu kwa Uingereza. Sir Keir, Lady Victoria na Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy walijikuta wamekaa katikati ya wageni wa Qatar na Serbia.

Kardinali Vincent Nichols, kiongozi wa Wakatoliki England na Wales, alisema waandaaji wa mazishi hayo wana uzoefu mkubwa wa kushughulikia matukio ya ukubwa huo.

Katika mahojiano na shirika la habari la PA jijini Roma kabla ya mazishi, alisema: "Bila shaka mazishi haya yatakuwa kazi nyingine bora ya usimamizi wa jukwaa, hasa ukiangalia viongozi wa mataifa wenye hisia za kujiona muhimu."

Aliongeza: "Nimeona mara nyingi hapa Roma na Vatican, kwamba wana kipaji cha kushughulikia matukio makubwa tangu enzi za Kaizari."

"Amini usiamini, kila kiongozi atarudi nyumbani akiwa ameridhika kwa namna fulani."

Kardinali Nichols anatarajiwa kushiriki katika mchakato wa kumchagua Papa mpya katika wiki zijazo. Leo ni siku ya kwanza miongoni mwa siku tisa za maombolezo kabla ya kuanza kwa majadiliano yoyote kuhusu Papa mpya.

Viongozi wengine mashuhuri waliotamani kuhudhuria walipata nafasi, akiwamo Rais wa zamani wa Marekani na Mkatoliki wa maisha yote, Joe Biden, aliyefika na mkewe Jill. Wao waliketi mistari mitano nyuma ya Trump na Melania.

Juzi Ijumaa, Msemaji wa Vatican Matteo Bruni alisema kuwa hakukuwa na ubaguzi kati ya familia za kifalme Wakatoliki na zisizo za Kikatoliki katika mpangilio wa viti.

Mkutano huo wa viongozi wa dunia tayari umechochea minong'ono ya mazungumzo zaidi ya kidiplomasia, mbali na yale yaliyopangwa kupitia viti.

Trump na Zelensky walikutana na kuzungumza kabla ya ibada, picha zikiwaonyesha wakizama katika mazungumzo ya ana kwa ana.

Mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufuatia ugomvi wao wa Februari Ikulu ya Marekani, katika juhudi za kufikia makubaliano ya kumaliza uvamizi wa Russia wa miaka mitatu dhidi ya Ukraine.


Pia walionekana wakizungumza na Emmanuel Macron na Keir Starmer. Downing Street ilisema Starmer alikubaliana kuendeleza juhudi za haraka katika kuhakikisha amani Ukraine.

Maelfu walijaa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na mitaa ya Roma kwa ajili ya misa ya wazi ya Papa Francis, kisha jeneza lake likapelekwa kwenye makazi yake ya Jiji la Roma.

Francis, aliyejulikana kama Papa wa watu kwa kujitolea kwa wanyonge, alifariki akiwa na miaka 88 Jumatatu iliyopita, saa chache baada ya kuwasalimia waumini katika maadhimisho ya Pasaka.

Alilazwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwa siku tatu, ambapo waumini wapatao 250,000 walimtembelea usiku na mchana kabla ya jeneza lake kufungwa rasmi Ijumaa.

Francis alikuwa Papa wa watu, mwenye moyo wa wazi, aliyelenga Kanisa la Kikatoliki lenye huruma na uwazi zaidi, alisema Kardinali Giovanni Battista Re katika mahubiri ya mazishi