Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Silaa asema mapambano ya VVU na Ukimwi yanapaswa kuendelezwa


Dar es Salaam. Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema jitihada za wadau mbalimbali zinapaswa kuendelezwa ili kupambana na kupunguza unyanyapaa unaohusiana na VVU, kuboresha upatikanaji wa matibabu na kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu.

Mbali na Waziri Silaa, Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imeeleza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia ni muhimu ili kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95 ambayo ni asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU kujua hali zao, 95 ya wanaojua hali zao kuwa kwenye matibabu, na asilimia 95 ya walioko kwenye matibabu kufanikisha kudhibiti kiwango cha virusi mwilini.

Silaa amebainisha hayo mwisho mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizindua  mbio za Kilimanjaro, maarufu Kili Marathon kwa mwaka 2025 zinazofanyika mara ya 22 zikiwa na lengo la kukusanya zaidi ya Sh2.2 bilioni kusaidia mapambano ya Ukimwi nchini.

Silaa amesema hatua hiyo haiishii kuchangisha fedha, bali kuunganisha nguvu kupunguza unyanyapaa unaohusiana na VVU, kuboresha upatikanaji wa matibabu na kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu.

 Amesema takwimu zinaonesha matumaini ya kupungua kwa maambukizi mapya kutoka watu 72,000 kwa mwaka 2016–2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022–2023.

"Huu ni ushahidi kwamba jitihada zetu zina matokeo, lakini safari bado ni ndefu maana hadi kufikia Desemba 2024, Tanzania inakadiriwa kuwa na takriban watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, ambapo zaidi ya milioni 1.5 tayari wanapata dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo," amesema Silaa.

Amefafanua wadau wote wanakaribishwa kushiriki katika tukio la kuchangisha fedha kwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kufanya matembezi ya baiskeli kuuzunguka mlima huo.

Hafla ya kuwaaga washiriki amesema itafanyika Julai 18, 2025, ikifuatiwa na hafla ya kuwakaribisha wakati wakishuka mlima Julai 24, mkoani Kilimanjaro.

Awali, Meneja Mwandamizi wa Masuala ya Uendelevu wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Gilbert Mworia amesema mwaka 2024 jumla ya wapandaji mlima 42 na waendesha baiskeli 18 walishiriki katika safari hiyo ya kihistoria ya kupanda kilele cha Mlima Kilimanjaro na kuzunguka kingo zake.

Amefafanua kuwa juhudi hizo za kishujaa zilisaidia kupatikana kwa zaidi ya dola za Marekani 850,000 (sawa Sh2.2 bilioni) na kutoka kwa mashirika, taasisi na watu binafsi.

“Fedha hizi zimechangia sana katika kusaidia miradi ya jamii inayowawezesha watu wanaoishi na Ukimwi, kutoa elimu na chakula kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kutoa ruzuku kwa miradi mbalimbali ya kitaifa na kijamii inayotoa huduma muhimu kwa waathirika wa janga hili.

“Ni jukumu letu kuhakikisha michango yetu inaendelea kugusa maisha ya watu wengi, tupande pamoja, tuendeshe kwa ajili ya Taifa letu na kuleta mabadiliko," amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Catherine Joachim, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kati ya Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia ili kufikia malengo ya kimataifa ya  kukabiliana na ugonjwa huo.

“Serikali imeendelea kuhakikisha huduma za VVU na Ukimwi zinapatikana nchini kwa makundi yote. Sambamba na mafanikio mengi yaliyopatikana, bado kuna baadhi ya makundi katika jamii yetu yapo kwenye  hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU na pia kuna upatikanaji hafifu wa huduma," amesema.

Ameyataja makundi hayo ni jamii ya wachimbaji wadogo, wavuvi, wanaoishi pembezoni mwa njia kuu za usafirishaji, vijana hasa wasichana na wanawake wanaofanya biashara ya ngono akiongeza kuwa uhitaji wa huduma za VVU na Ukimwi katika makundi hayo ni wa kipekee.