Wanafunzi wa kike kupewa kipaumbele masomo ya urubani

Muktasari:
- Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kutumia Sh50 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na ndege za mafunzo kwenye mradi wa ujenzi wa chuo cha wataalamu wa anga kitakachojengwa Juni mwaka huu mkoani Kilimanjaro
Hai. Wanafunzi wa kike wanaomaliza kidato cha sita kupewa kipaumbele kujiunga na elimu ya juu katika mafunzo ya usafiri wa anga katika fani ya urubani.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kutolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),kupitia chuo cha wataalamu wa anga kitakachojengwa Juni mwaka huu kwenye eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Hayo yamesemwa jana na mkuu wa NIT, Zacharia Mganilwa wakati wa makabidhiano ya eneo lenye ukubwa wa hekta 60 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho.
“Wanawake wajitokeze kwa wingi, mwanafunzi wa kike mwenye sifa atakayejitokeza hatutamuacha kwa sababu wanawake wamekuwa wakiamini kazi ya urubani haiwafai, ”amesema Mganilwa.
Mganilwa amesema chuo hicho kitakua chuo bora Afrika na kitatoa wataalamu bora na wabobezi katika fani hizo ambao wataweza kufanya kazi ndani na nje ya nchi.
Amesema mradi wa ujenzi huo unatarajiwa kuanza mapema Juni mwaka huu ambapo gharama za miundombinu pamoja na ndege ni zaidi ya Sh50 bilioni ikiwamo ununuzi wa ndege tano za mafunzo, ambapo Serikali imeahidi kununua mbili kati ya hizo.
Naye Mwenyekiti wa uongozi wa baraza la chuo hicho Bavo Nyichomba amesema wataanza kupokea wanafunzi 10 katika kipindi cha awali ili waweze kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa.
Amefafanua kuwa gharama za kupata mafunzo hayo zitaanzia Sh72 milioni hadi mwanafunzi anahitimu, ikiwa ni gharama nafuu ukilinganisha na zinazolipwa kwenye vyuo vya nje.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa kampuni ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (Kadco), Christopher Mkoma, amesema ujio wa ujenzi wa chuo hicho ni neema kwa Watanzania ambao wana kiu ya kuwa wataalamu wa ndege na urubani.
Mkoma amesema ukubwa wa uwanja cha Kia, utasaidia katika mafunzo hayo sambamba na uwanja huo kuwa jirani na viwanja vya Moshi , Arusha na Tanga.