Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waonywa kula vyakula vya mafuta kuepuka maradhi

Meneja wa Maradhi yasioambukiza Zanzibar (ZANCDA), Dk Omar Mohammed Suleiman akizungumza wakati wa mafunzo ya maradhi hayo kwa waandishi. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya Zanzibar mwaka 2001, shinikizo la damu liliongoza kwa vifo.

Unguja. Ili kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza kisiwani Zanzibar, wananchi wamehimizwa kupunguza matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi, sukari na chumvi kupita kiasi.

Badala yake, wametakiwa kuzingatia ulaji unaofaa kwa kula vyakula vya wanga, matunda, mboga mboga ili kupunguza hatari ya maradhi hayo.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Aprili 27, 2025, na Meneja wa Magonjwa yasiyoambukiza Zanzibar (Zancda), Dk Omar Mohammed Suleiman wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu maradhi hayo.

Dk Omar amesema magonjwa hayo yamekuwa tatizo kubwa duniani, mwaka 2016 yalisababisha vifo vya watu milioni 42, sawa na asilimia 71 ya vifo duniani kote.

Amesema kati ya kila vifo 10, vifo vinane husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza, hivyo kuwa chanzo kikuu cha vifo na ulemavu.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya Zanzibar mwaka 2001, shinikizo la damu liliongoza kwa vifo, asilimia 31 ya watu walibainika kuwa na tatizo hilo.

Utafiti wa mwaka 2023 umeonesha kiwango hicho kimeongezeka hadi kufikia kati ya asilimia 33 na 43.

Akizungumzia ugonjwa wa kisukari, Dk Omar amesema, “mwaka 2001 ulikuwa ukikumba asilimia 3.8 ya watu, lakini mwaka 2023 umeongezeka hadi asilimia 7.5."

Aidha, Dk Omar amesema sehemu kubwa ya bajeti ya Wizara ya Afya Zanzibar hutumika kununua dawa za kutibu maradhi yasiyoambukiza, matibabu ya mgonjwa mmoja yanaweza kugharimu zaidi ya Sh500,000.

Amesema pia, matumizi ya shisha yamekuwa tatizo miongoni mwa vijana wengi visiwani hapa.

Dk Omar amesema mtu akivuta pafu moja la shisha ni sawa na kuvuta sigara 100, hivyo kuongeza hatari ya maradhi kama vile figo kushindwa kufanya kazi.

Hivyo, amewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi hali kuwa mbaya ndipo waende hospitalini.

Daktari huyo amesema magonjwa hayo yanatibika kwa ufanisi zaidi yanapogunduliwa mapema.

Mtaalamu wa Afya na Mazoezi kutoka Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (Tancda), Waziri Ndondi amesema magonjwa hayo husababishwa na mtindo mbaya wa maisha, ikiwamo kutofanya mazoezi ya mwili na kuendekeza tabia zisizofaa.

Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linahimiza watu kuzingatia ulaji wa chakula bora na kufanya mazoezi ili kulinda afya dhidi ya maradhi yasiyoambukiza.

Hivyo, jamii imetakiwa kufanya mabadiliko ya tabia na kuzingatia mtindo wa maisha unaoimarisha afya.

Mtaalamu wa lishe, Adelina Munuo amesema watu wanapaswa kula vyakula vinavyokidhi mahitaji ya mwili kwa ajili ya makuzi na maendeleo bora ya mwili.

Amesisitiza umuhimu wa kula mlo kamili wenye virutubisho sahihi na kuepuka vyakula vya kukaanga kwa mafuta pamoja na matumizi ya pombe kupita kiasi.