Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yazindua kanuni ya uongezaji virutubishi kwenye chakula: Kila mzalishaji anatakiwa kuongeza virutubishi

Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dk Ashura Katunzi (kushoto) na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania Bi. Elke Wisch (kulia) pamoja na wawakilishi wengine wa Serikali kutoka Wizara ya Afya, Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) na Katibu Tawala wa Mkoa wakati wa uzinduzi wa kanuni za urutubishaji chakula mkoani Ruvuma.

Katika mkakati wa kihistoria ulioanzishwa ili kuharakisha mapambano dhidi ya utapiamlo na kufanya marekebisho ya viwango vya usalama wa chakula nchini, Machi 2025 Serikali ilizindua rasmi Kanuni ya uongezaji virutubishi kwenye chakula ya mwaka 2024.

Hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika mkoani Ruvuma, iliongozwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, pamoja na viongozi wakuu wa kitaifa na kikanda, wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa, wadau wa afya na lishe, wasindikaji wa chakula, wadau kutoka sekta mbali mbali na wawakilishi wa kijamii.

Sheria hii mpya inagusa wasindikaji wote wakubwa na wadogo wa bidhaa za unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kula na chumvi, wote wanatakiwa kuongeza virutubishi (vitamin na madini) kwenye bidhaa hizo.


Urutubishaji wa lazima kwa wasindikaji wote

Kanuni hii mpya inawalazimu wasindikaji wote wa unga wa mahindi, unga wa ngano na mafuta ya kula kuongeza virutubishi (mchanganyiko wa vitamini na madini) kwenye chakula wanachozalisha.

Wasindikaji wa chakula wamepewa miezi saba tu, ya kuhakikisha wanafunga mashine za kuongeza virutubishi kwenye chakula (vinyunyizi), kununua virutubishi na kuanza kufanya urutubishaji wa chakula ili kuhakikisha wanaendana na viwango vipya vya usalama wa chakula vilivyowekwa.

Ujumbe kutoka kwa viongozi wa Serikali unasema: ‘Wakati umekwisha. Msindikaji Rutubisha au ukumbane na mkono wa sheria kuanzia Desemba 2025, au kuiweka biashara yako katika hatari ya kufungwa!’


Maelekezo muhimu

Ulazima wa kufuata kanuni: Bidhaa zote za unga na mafuta ya kula ni lazima sasa ziongezwe virutubishi wakati wa usindikaji kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni.

Muda uliosalia ni miezi saba: Hatua za kisheria za kanuni hii zitaanza kutekelezwa kikamilifu kuanzia Disemba 2025.


Walengwa

Kanuni hii inawagusa wasindikaji wote, wadogo kabisa, wa kati na wakubwa. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeagizwa kutekeleza kikamilifu kanuni hizo kuanzia Disemba 2025.

Naibu Waziri Mhe. Kigahe alisema kuwa, kipindi hiki cha miezi saba ni nafasi ya mwisho ya maandalizi. Hakutakuwa na visingizio.

Wasindikaji watakaopuuza utekelezaji wa kanuni watakabiliwa na adhabu ikiwemo kufungiwa biashara zao. Hii ni pamoja na wasindikaji kutorutubisha bidhaa zao, urutubishaji wa kiwango cha chini au kurutubisha kwa kutumia virutubishi ambavyo havijakidhi viwango vya ubora.


Ubunifu wa kiteknolojia na kuwainua wazalishaji wa ndani

Ili kuhakikisha kanuni hizo zinafuatwa bila vikwazo, Serikali imewezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za urutubishaji unga. Mashine zenye ubora uliothibitishwa kwa ajili ya urutubishaji zenye uwezo mkubwa, zinawezesha uchanganyaji sahihi wa virutubishi ambao hupunguza makosa ya kibinadamu yanayoweza kutokea wakati wa uchanganyaji na upotevu wa virutubishi hivyo.

Mashine hizo (vinyunyizi) zinatolewa bila gharama yoyote na kampuni kama Sanku, kampuni ambayo inawawezesha wasindikaji, wadogo, wa kati na wakubwa kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi na ngano kulingana na matakwa ya sheria.

Aidha, ili kukabiliana na virutubishi visivyo na ubora sokoni, kiwanda cha kisasa cha kuchanganya virutubishi (Nutrient Blending Factory) kilichozinduliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam kimewezesha wasindikaji wa ndani kupata virutubishi bora kwa gharama nafuu. Uzalishaji wa kiwanda hicho sio kwa mahitaji ya ndani tu, bali pia nchi za jirani kama Kenya, Rwanda na Ethiopia.


Kitu gani ambacho Sanku wanacho?

Mashine ya kisasa ya Dosifier: Teknolojia ya kisasa ambayo inapunguza makosa ya kibinadamu wakati wa uchanganyaji virutubishi na kuhakikisha urutubishaji unafanyika kwa usahihi.

Meneja wa Sanku Dosifier, Mhandisi Joseph Mtwangwe akitoa maelezo kwa Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe ya jinsi teknolojia hiyo inavyohakikisha urutubishaji sahihi wa unga.


Miundombinu ya kuwasaidia wasindikaji wa ndani: Kiwanda cha kuchanganya virutubishi kiko tayari kuzalisha na kusambaza virutubishi vyeye ubora na vya bei nafuu.


Uelewa na utekelezaji wa kanuni

TBS kuanza utekelezaji wa kanuni Desemba 2025

Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji, TBS imeagizwa kuanza utekelezaji kamili wa kanuni mpya kuanzia Desemba 2025. Mhe. Kigahe alisisitiza kuwa muda huu unatoa fursa ya kutosha kwa wasindikaji wa chakula kufuata mahitaji ya kanuni hizo huku akiwataka kuutumia muda huu vizuri kujiandaa.

Utekelezaji wa programu za uhamasishaji na mafunzo Sambamba na utekelezaji, Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuzindua programu za uhamasishaji na mafunzo zinazolenga wadau wote, wakiwemo wasindikaji wa chakula, mamlaka za Serikali za mitaa na watumiaji.


Kuunga mkono kampeni za uhamasishaji

Kutambua kwamba mahitaji ya walaji ni kichocheo kikubwa katika kukabiliana na janga la njaa, washirika wa kimaendeleo na mashirika ya kiraia kwa muda mrefu wamesisitiza hitaji la elimu thabiti kwa umma kuhusu urutubishaji wa chakula. Hii inathibitishwa na;

• Utafiti uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na GAIN mwaka 2015 ulionyesha kuwa ni asilimia 2.5 pekee ya kaya zinatumia unga uliorutubishwa.

• Baada ya Sanku kufunga mashine 70 za Dosifiers katika viwanda vidogo vya kuzalisha unga mkoani Morogoro, utafiti uliofanywa na taasisi ya Helen Keller International ulionyesha kuwa kaya zinazotumia unga uliorutubishwa zimeongezeka kufikia asilimia 72.

• Utafiti uliofanywa na DCD mkoani Morogoro mwaka 2018 ulionyesha kuwa, asilimia 66 ya kaya zilikuwa tayari zinatumia unga uliorutubishwa. Hii inaongeza matumizi ya folic acid kwa wakina mama ambayo inasaidia kupunguza changamoto wakati wa kujifungua.

• Hadi kufikia mwaka 2025, zaidi ya viwanda vidogo 1,200 vya kuzalisha unga nchini vilikuwa vimewezeshwa kufanya urutubishaji na Sanku. Mbali na idadi hiyo lakini bado kuna pengo kubwa ambapo inakadiriwa kuwa viwanda vidogo 3,000 bado vinahitajika kufanya urutubishaji.

Takwimu hizi zinasisitiza kwamba inapojumuishwa na machaguo sahihi ya watumiaji, mipango ya urutubishaji sio tu inaboresha matokeo ya afya kwa kupunguza hatari za kudumaa, upungufu wa damu, na kasoro za kuzaliwa (kama vile kichwa kujaa maji na mgongo wazi) lakini pia huongeza mahitaji ya vyakula vilivyorutubishwa.


Faida katika elimu na afya ya umma

Kanuni hizi mpya pia zinajumuisha maelekezo kwamba shule zote zinapaswa kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubishi katika programu zake za chakula mashuleni.

Mwongozo huu unatekelezwa ili kupambana na utapiamlo miongoni mwa watoto walio katika umri wa kwenda shule, ili kuhakikisha kwamba lishe bora inachangia mahudhurio na matokeo mazuri ya watoto shuleni.

Takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 33 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, na asilimia 37 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wanakabiliwa na upungufu wa damu, hali inayohusishwa kwa kiasi kikubwa na ulaji duni unaopelekea upungufu wa madini na vitamini muhimu mwilini.


Faida za kiafya na elimu

• Milo iliyorutubishwa ni lazima mashuleni: Hii inalenga moja kwa moja utapiamlo wa utotoni na kuimarisha ukuaji.

• Kupunguza hatari za kiafya: Urutubishaji unatarajiwa kupunguza udumavu, upungufu wa damu na ulemavu wa kuzaliwa ikiwa ni pamoja na tatizo la kichwa kujaa maji na mgongo wazi.

Urutubishaji wa chakula nchini ulianza miaka ya 1990 kwa kuongeza madini joto kwenye chumvi ili kukabiliana na tatizo la uvimbe wa tezi ya shingo (goiter).

Mwaka 2011 ilitoka kanuni ya uongezaji virutubishi kwenye chakula iliyojumuisha bidhaa za unga wa mahindi, wa ngano na mafuta ya kula ikiwalazimu wasindikaji wakubwa na wakati, huku ikiwaacha wasindikaji wadogo ambao wanalisha sehemu kubwa ya jamii ya Tanzania.

Kanuni mpya ya mwaka 2024 inalenga kuziba pengo hilo kwa kujumuisha wasindikaji wote wa chakula, hata wale wadogo kabisa, ili kuhakikisha kwamba vyakula vilivyoongezwa virutubishi vinawafikiwa watu wate nchini.

Ulimwenguni kote, urutubishaji wa chakula unatambuliwa kama mojawapo ya mbinu bora zaidi za kuimarisha afya ya jamii. Zaidi ya nchi 125 zimepitisha sera za lazima za urutubishaji chakula, huku 93 kati ya hizo zikihitaji zaidi urutubishaji wa unga.

Mwaka 2004, jopo la wataalamu wa Copenhagen Consensus lilibainisha afua ya urutubishaji kama mojawapo ya mikakati madhubuti ya maendeleo, matokeo ambayo yalithibitishwa tena mwaka 2008 na 2012. Tafiti zinaonyesha kuwa, uwekezaji wa kimkakati katika urutubishaji wa chakula umeleta matokeo chanya nchini.

Kulingana na tafiti uliofanywa na Gates Foundation, kila dola moja inayowekezwa kwenye urutubishaji wa chakula huzalisha wastani wa dola 27 kama faida ya kiuchumi kupitia kupunguza mzigo wa magonjwa, kuongeza uwezo wa kuzalisha kipato na kuboresha uzalishaji.


Wito wa kuchukua hatua za pamoja kama Taifa

Katika hotuba yake ya kufunga uzinduzi huo Mhe. Kigahe alieleza lengo la mkakati wa Serikali, akisema kuwa “Chakula ni lishe, chakula ni afya, chakula ni uchumi.” Alitoa wito kwa wasindikaji wote wa chakula kuzingatia kanuni mpya na kuzitaka taasisi za Serikali na viongozi kutumia kila jukwaa kueneza taarifa sahihi kuhusu faida za kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubishi.