Wanafunzi 59 wadakwa na simu kwenye chumba cha mtihani

Muktasari:
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kagera inawashikilia wanafunzi 59 wa vyuo viwili vya ufundi Veta kwa madai ya kukutwa na simu za mkononi katika chumba cha mtihani.
Kagera. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kagera inawashikilia wanafunzi 59 wa vyuo viwili vya ufundi Veta kwa madai ya kukutwa na simu za mkononi katika chumba cha mtihani.
Mbali na kuwashikilia wanafunzi hao wa chuo cha Veta Kagera na kile cha Veta Tuinuane kilichopo Bukoba vijijini, taasisi hiyo pia inawashikilia walimu watatu na kukamata Sh151,000 zinazodaiwa kuchangwa na wanafunzi kwa ajili ya kuwapatia wasimamizi wa mtihani.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Desemba 15, 2020 na mkuu wa Takukuru mkoani Kagera, John Joseph katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Ametumia mkutano huo kuonyesha simu hizo na kubainisha kuwa wanafunzi wa chuo cha Tuinuane ni 21 na Veta Kagera wapo 38.