KONA YA MZAZI: Tusiwaharibu watoto kwa hoja ya kulinda haki za binadamu

Katika hali kama hii, wazazi wameachwa na jukumu kubwa na gumu zaidi la kulea watoto katika njia ya haki na kuwaepusha na maangamizi ya kimaadili, kijamii na kisaikolojia.
Hali halisi inayotokea kwenye jamii zetu kama mzazi kumpiga mtoto kwa nia ya kumrekebisha, jirani kuingilia na kuleta tafrani, inaonesha jinsi malezi yalivyopoteza dira na mshikamano wake wa awali.
Haki za binadamu ingawa zina umuhimu mkubwa, wakati mwingine zinapotafsiriwa vibaya, zimewapa watoto nafasi ya kukosa nidhamu bila kuelewa mipaka ya uhuru wao. Sasa ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa wazazi kushirikiana na kuchukua hatua madhubuti ili kuwalinda watoto kwa kuongeza umakini katika malezi.
Natamani kuona kila mzazi anamlea mwanawe kwa nidhamu ya hali ya juu na kwa kufuata tabia njema ya wazazi wake.
Tabia ya mzazi ina uzito mkubwa katika kujenga tabia ya mtoto. Wazazi wanapaswa kuonesha maadili wanayotamani kuona kwa watoto wao.
Nao wawe watu wa kuheshimu wengine, kuzungumza kwa staha, kujizuia hasira na kuishi kwa uadilifu.
Mtoto anayekua akiona wazazi wake wanaishi maisha ya kistaarabu, wenye maadili na wavumilivu, naye atajifunza kuishi kwa mfano huo.
Katika wakati huu ambao taarifa za mtandaoni ni nyingi, watoto hupata maarifa mengi kutoka vyanzo mbalimbali.
Wazazi watambue si vyanzo vyote vinafaa kutazamwa na watoto. Hivyo wazazi wanapaswa kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na watoto wao, wakifafanua tofauti kati ya mema na mabaya.
Wasiwe waoga kuzungumzia mambo magumu kama vile ngono, matumizi ya dawa za kulevya, au tabia hatarishi.
Watoto wanapopata fursa ya kuzungumza wazi, hujihisi salama na hujifunza kuwaamini wazazi wao.
Malezi si kazi ya mtu mmoja; ni jukumu la jamii nzima. Zamani, mtoto alikuwa wa jamii yote. Ipo haja ya kurudisha moyo huo utamaduni wa usaidizi wa pamoja.
Wazazi washirikiane pia na walimu, viongozi wa dini na majirani ili kuhakikisha watoto wanapata maadili bora kutoka pande zote. Badala ya kupigana au kuhukumiana haraka, wazazi wanapaswa kushirikiana na kusikilizana kwa hekima.
Uhuru bila mipaka huzaa uharibifu. Watoto wanahitaji kujua ni nini wanachoruhusiwa kufanya na nini hawaruhusiwi.
Lazima kuwepo na sheria ndogo za nyumbani kuhusu matumizi ya muda, simu, michezo na marafiki. Nidhamu isipowekwa, watoto hukosa mwongozo wa ndani wa kufanya uamuzi sahihi.
Lakini pia ni muhimu nidhamu hiyo itolewe kwa upendo na kueleweka vizuri na si kwa hasira wala kwa unyanyasaji. Kuwachapa watoto kupita kiasi au kwa hasira, hakujengi, bali kunavunja moyo. Kila adhabu iwe na mafunzo ndani yake, siyo kulipiza kisasi cha hisia za mzazi.
Nasema hivyo kwa sababu wazazi wengi wanajitenga na maisha ya watoto wao kwa kisingizio cha shughuli nyingi.
Hili ni kosa kubwa. Wazazi wanapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watoto wao ili kuwasaidia kazi za shule, kujua marafiki zao na kushiriki katika matukio yao muhimu.
Mtoto anayemwona mzazi kama rafiki, hushiriki matatizo yake kirahisi, hivyo mzazi hupata nafasi ya kusaidia kabla mambo hayajaharibika.
Imani ya kidini imekuwa mwongozo muhimu kwa vizazi vingi. Mafundisho ya dini yanawasaidia watoto kuelewa thamani ya maadili kama uaminifu, heshima na upendo. Hivyo, ni vema wazazi wajenge utamaduni wa kuwahimiza watoto kushiriki katika shughuli za kiimani na kutumia maandiko matakatifu kama rejea katika maisha ya kila siku.
Katika ulimwengu wa leo unaoteteresha misingi ya maadili, wazazi hawawezi kulea kwa mazoea ya jana. Wanahitaji kuamka, kushirikiana, kuelimika na kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watoto wao kuishi kwa maadili mema na mafanikio.
Kila mmoja anapaswa kutambua kuwa katika nyakati hizi, kulea ni kazi ngumu, dunia inawahitaji wazazi wenye maono, upendo na uthabiti wa kweli.