Waliofariki kongamano la Mtume Mwamposa kuagwa leo

Ndugu jamaa na marafiki wakiwa katika hospitali ya mawenzi kwa ajili ya kuwachukua ndugu zao.Miili ya watu 20 itaagwa katiks viwanja vya mashujaa moshi.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Watu 20 walifariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa Jumamosi Februari Mosi, 2020 mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro waliposhiriki ibada ya Kongozi wa kanisa la Inuka Uangaze, Nabii na mtume Boniface Mwamposa katika uwanja wa Majengo, wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyomwagwa milango ya kutokea uwanjani.
Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania, Anna Mghwira amesema ibada ya pamoja ya kuwaaga watu 20 waliofariki dunia Jumamosi Februari Mosi, 2020 mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro itafanyika leo saa tano asubuhi.
Akizungumzia taratibu za mazishi leo Jumatatu Februari 3, 2020, Mghwira amesema ibada ya kuaga miili hiyo itafanyika saa tano asubuhi mjini humo.
Watu hao walifariki Jumamosi Februari Mosi, 2020 usiku wakati waliposhiriki kongamano la kidini la kiongozi wa kanisa la Inuka Uangaze, Nabii na mtume Boniface Mwamposa katika uwanja wa Majengo, wakigombea kukanyaga mafuta ya upako yaliyomwagwa milango ya kutokea uwanjani.
“Tutaanza saa tano, tutaleta miili na tutafanya misa ya pamoja tutawaaga” amesema Mghwira
Mghwira amesema walikuwa wanafanya utaratibu wa kuwasiliana na kiongozi mkuu wa hilo kanisa ambaye anatoka Nairobi nchini Kenya ili kumpa jukumu la kugharamia mazishi.
“Hapa tulikuwa tunaangalia kuna huyo kiongozi mkuu wa hilo kanisa (kanisa la Inuka Uangaze) anaitwa Maboya sijui, anatoka Nairobi toka jana jioni nilikuwa bado sijampata lakini leo asubuhi nimepata namba yake nimemtumia ujumbe kwamba tuonane asubuhi” amesema RC Mghwira
“Kimsingi kwa kweli wao ndio wanaotakiwa kugharamia hii kitu, majeneza, usafiri wa kuwapeleka marehemu kwao na ndugu zao waliokuja kuwachukua, sisi (Serikali) tumechukua jukumu kwa sehemu ya kuanzia lakini hizi gharama ndio wanatakiwa wazilipe” amesema
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi