Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliodai kubadilishiwa mtoto, waendelea kususia mwili

Muktasari:

  • Familia ya Neema Kilugala ilianza kususia mwili wa mtoto huyo tangu Aprili 3, 2025, siku ambayo majibu ya DNA yalitoka

Arusha. Zikiwa zimepita siku 26 tangu matokeo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) yatolewe, yakionesha Neema Kilugala (26), mkazi wa Mtaa wa Ndarvoi, hakubadilishiwa mtoto kama alivyodai, familia yake imeendelea kususia mwili ikisema wameamua kumwachia Mungu suala hilo.

Familia hiyo ilianza kususia mwili wa mtoto huyo tangu Aprili 3, 2025, siku ambayo majibu ya DNA yalitoka.

Ilitaka uchunguzi wa ziada na waliomba msaada wa wananchi wenye mapenzi mema ili vipimo hivyo vipelekwe nje ya nchi kwa majibu ya uhakika zaidi.

Uchunguzi huo ulijumuisha wazazi watatu waliokuwa wamejifungua kwa kipindi kimoja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, kwa lengo la kuthibitisha iwapo kulikuwa na kubadilishwa mtoto.

Majibu yaliyotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali yalionesha kuwa, mtoto aliyekabidhiwa kwa Neema alikuwa wake kwa asilimia 99.99, ingawa alifariki dunia kabla ya majibu hayo kutolewa.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 28, 2025, na Mwananchi, mama mzazi wa Neema, Sabrina Andrew, amesema familia haiwezi kuuchukua mwili wa mtoto huyo kwa kuwa wanaamini si wa kwao.

Sabrina amesema familia ilijaribu kutafuta huduma ya vipimo vya DNA Nairobi, Kenya, lakini gharama zilikuwa kubwa, hivyo wakaamua kumwachia Mungu.

"Tulitaka vipimo virejeshwe, lakini gharama ni kubwa. Hatuna uwezo, tumeamua kunyamaza na kumlilia Mungu. Tunaamini haki yetu iko kwa Mwenyezi Mungu," amesema Neema.

Amesema kama wangekuwa na uwezo wa kifedha, wangechukua hatua zaidi, hata kuhama mkoa huo.

Amesisitiza msimamo wao kuwa mtoto wao alibadilishwa na yupo hai.

Tangu kutolewa kwa majibu ya DNA, Neema na familia yake wamekataa kuyakubali huku akidai kuwa mtoto aliyefariki dunia si wake na anaamini mtoto wake halisi bado yupo hai.

"Siwezi kumzika mtoto ambaye si wangu. Hakuna msiba kwetu kwa sababu tunaamini mtoto wetu hajafa," amedai Neema kwa msisitizo.

Neema alijifungua mtoto wa kike Machi 24, 2025.

 Kufuatia malalamiko yake ya kubadilishiwa mtoto, Wizara ya Afya ilimwamuru muuguzi aliyemhudumia kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi.

Muuguzi huyo alikiri kuchanganya vitenge vya watoto, hatua iliyozua mkanganyiko.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha baada ya kutolewa kwa matokeo ya DNA, Makamu wa Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Jane Bararukuliliza alisema chama hicho kilifuatilia suala hilo kwa karibu. Alieleza kuwa, Serikali ilitoa nafasi kwa wazazi ambao hawakuridhika kuchukua hatua zaidi na kuwataka wauguzi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.