Wanaodai kubadilishiwa mtoto wasusia mwili, wataka DNA irudiwe nje ya nchi

Neema Luligala aliyedai kubadilishiwa mtoto wake wa kike aliyejifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru,akizungumza na waandishi wa habari Arusha leo baada ya majibu ya DNA kutoka
Muktasari:
- Neema Lilugala, mkazi wa Mtaa wa Ndarvoi, Kata ya Daraja Mbili, alidai kujifungua mtoto wa kike Machi 24, 2025, akiwa na uzito wa kilo 3.1 hata hivyo, alidai baadaye alibadilishiwa mtoto na kupewa mtoto mwingine ambaye siyo wake.
Arusha. Ikiwa zimepita siku sita tangu majibu ya vinasaba (DNA) kutolewa na kuonyesha kuwa mkazi wa Mtaa wa Ndarvoi, Neema Kilugala (26), aliyedai kubadilishiwa mtoto siyo kweli na kuwa mtoto aliyepewa (ambaye kwa sasa ni marehemu) ndiye wa kwake, familia hiyo imesusia mwili wa mtoto huyo ikitaka uchunguzi zaidi.
Pamoja na kususia familia hiyo inaomba msaada wa wananchi wenye mapenzi mema wawasaidie vipimo hivyo vikarudiwe nje ya nchi, ili wajiridhishe.
Wakizungumza leo Jumatano Aprili 9,2025 nyumbani kwao katika Kata ya Daraja Mbili, Neema na mama yake (Sabrina Andrew), wamedai kuwa mtoto aliyefariki siyo wa kwao, hivyo hawawezi kuweka msiba nyumbani kwao.
Aprili 3, 2025 majibu ya DNA yalitolewa na kuonyesha kuwa wazazi watatu waliojifungua katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru muda mmoja walipopimwa ili kubaini ukweli kuhusu madai ya kubadilishwa mtoto, majibu ya vinasaba kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali yalionyesha mtoto aliyepewa na Neema anafanana naye kwa asilimia 99.99.
Hata hivyo, tangu siku hiyo Neema aliendelea kuyakataa matokeo hayo na hadi sasa msimamo wa familia hiyo ni kuwa mtoto huyo siyo wa kwao na hawakubaliani na majibu hayo.
“Yule mtoto aliyefariki siyo wa kwangu, mtoto wangu bado yuko hai na nina imani kuna mtu anaye, sina imani na majibu ya DNA kwani nilivyojifungua sikuambiwa mtoto wangu ana shida yoyote, angekuwa na shida wangeniambia kuanzia kwenye chumba cha upasuaji.”
“Siwezi kumzika mtoto ambaye siyo wa kwangu, ndiyo maana hapa kwetu hakuna msiba kwa sababu mtoto wetu hajafa, ninamtambua mtoto wangu nilionyeshwa baada ya kujifungua ila huyu wanasema ni wangu siyo wa kwangu.”amesisitiza Neema.
Kwa upande wake Sabrina (mama wa Neema), amedai baada ya familia kukaa na kujadiliana kuhusu suala hilo, hawakubaliani na majibu hayo na kuwa mtoto aliyefariki siyo wa kwao na kuomba Watanzania wawasaidie kuwachangia ili waweze kurudia vipimo vya DNA.
“Bado ninakataa yule mtoto siyo wa kwetu, hatutazika maana sina mjukuu aliyefariki, ninawaomba Watanzania wenye mapenzi mema watusaidie tuweze kurudia DNA nje ya nchi, ili tujiridhishe kwa kile kilichofanyika, kwani hatuna imani kuwa huyu mtoto aliyefariki ni wetu,” ameomba.
Neema amedai kubadilishiwa mtoto wake wa kike aliyejifungua Machi 24,2025 ambapo kufuatia malalamiko hayo Wizara ya Afya ilichukua hatua ya kumsimamisha kazi muuguzi aliyemhudumia mzazi huyo ili kupisha uchunguzi.
Muuguzi huyo alidai kuchanganya vitenge na vya mtoto mwingine hivyo alikwenda kubadilisha ambapo licha ya kufanya hivyo hali ya sintofahamu iliendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha baada ya majibu hayo kutolewa, Makamu wa Raisi wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Jane Bararukuliliza, alisema baada ya kuona taarifa kuhusu changamoto hiyo iliyojitokeza walichukua hatua kama chama kufuatilia suala hilo.
Makamu huyo bila kuwataja majina wazazi hao wengine (wawili) alisema Serikali ilishauri kama mtu hajaridhika anaweza kuendelea kuchukua hatua na kuwataka wauguzi kuendelea kutoa huduma vizuri kwa wananchi.
Awali Neema alidai baada ya kufanyiwa upasuaji alifanikiwa kumuona mtoto wake na muuguzi alimjulisha kuwa mtoto ni mzima na yuko mwenye afya akiwa na uzito wa kilo 3.1.
“Mtoto wangu wamemchukua na kwa vile tu nilifanyiwa operesheni wasingemchukua, mimi ninamtaka mtoto wangu mwenye kilo 3.1, mweupe tena ana alama mikononi kama yangu, si huyu mweusi mwenye kilo 2.285 tena ana matatizo ya moyo kuwa mkubwa,” alilalama Neema.