Walimu wa Tanzania sasa kupimwa kama mawakili

Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda akikabidhi mfano wa hundi ya Sh3 milioni kwa mshindi wa shindano ya stadi za ufundishaji wa somo la Kiingereza, Mwalimu Jenipha Chuwa wa Shule ya Msingi Enaboishu Academy.

Muktasari:

  • Wahitimu wa ualimu sasa watapitia mtihani maalumu wa kitaaluma kama wahitimu wa sheria na uhasibu. Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, asema utaratibu huo utaanza baada ya kuajiri walimu 13,000 hivi karibuni.

Dar es Salaam. Ule mchakato wanaopitia wahitimu wa shahada za sheria, unaowataka kufanya mtihani maalumu, ili wafuzu kuwa mawakili, sasa umeangukia katika taaluma ya ualimu.

Kutokana na hilo, wahitimu wa ngazi mbalimbali za taaluma ya ualimu, baada ya kuanza kwa mchakato huo, ili wawe walimu watapaswa kufanya mtihani maalumu wa kupima uwezo wao.

Hiyo ni kama inavyofanywa katika taaluma ya uhasibu, kadhalika madaktari ambao pamoja na kuwa na shahada bado hawastahili kusajiliwa kutekeleza taaluma zao, hadi watakapofanya mtihani wa itihabi ya kitaaluma.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo Juni 26, 2024 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipohutubia katika hafla ya kutoa tuzo za Shindano la Stadi za Ufundishaji wa Somo la Kiingereza zilizoratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).


Sababu za mtihani huo, amesema ni kuhakikisha wanapatikana walimu wenye weledi na kukomesha upendeleo katika ajira bila kujali uwezo wa mwanataaluma husika.


Sababu nyingine kwa mujibu wa Profesa Mkenda, ni kuiongezea hadhi taaluma ya ualimu isitazamwe kuwa kila mwenye uwezo duni wa kitaaluma ndiye anayepaswa kuwa mwalimu.

“Kwa walimu wapya, mnapaswa kujua mnaingia kwenye kazi maalumu, ili kuhakikisha mnakuwa bora katika kufanikisha hilo, tutawapima kwa mtihani maalumu,” amesema.

Ameeleza utaratibu huo utaanza kwa walimu wapya watakaoajiriwa baada ya 13,000 wanaotarajiwa kuajiriwa hivi karibuni.

"Kwenye sera tumesema utasoma huko uliposoma taratibu tumeziweka, lakini tutakupitisha kwenye mtihani, kwa sasa tunatarajia kuajiri walimu 13,000 ambao hawatapitia mchakato huu, lakini baada ya hao wengine watalazimika kupitia,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, amesema utaratibu huo utaondoa dhana kuwa ualimu ni taaluma isiyo na hadhi.

Licha ya kuanza kwa utaratibu huo, Profesa Mkenda amesema waliopo kazini wataendelea kufanya kazi kama ilivyokuwa awali, lakini wapya wote watapitia mchakato huo.

“Hii pia itakomesha ajira za vimemo, bali juhudi na uwezo wa mtu ndiyo utakaompa nafasi,” amesema.


Kuhusu Kiswahili

Katika hotuba yake hiyo, Profesa Mkenda amesema shindano hilo limehusu ufundishaji wa somo la Kiingereza, akisisitiza ni muhimu kuwajengea Watanzania maarifa ya kuijua lugha hiyo.

Ameeleza itakuwa makosa kufikiria kukieneza na kukitangaza Kiswahili, bila kujifunza lugha nyingine zenye nguvu duniani, kikiwemo Kiingereza.

“Kiswahili kinabaki kuwa lugha kidedea nchini na kitaendelezwa na kukuzwa nchini na duniani, hata kama tunakipenda sana Kiswahili, hautaweza kukieneza kama hatutajifunza na lugha nyingine.

“Ili kukieneza Kiswahili inahitajika kujua Kiingereza pia, wanafunzi wasipofundishwa vya kutosha kutakosa wakalimani,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kuwaheshimu walimu, kuwapa motisha na ari ya kutekeleza majukumu yao, akieleza Serikali imejikita kufanikisha hayo.

Amewataka watumishi wa wizara yake kuhakikisha wanawahudumia walimu haraka watakapofika ofisini, ili warudi kuendelea na kazi ya ufundisaji.

Hata hivyo, ameeleza pamoja na uwepo wa changamoto ya miundombinu katika sekta ya elimu, walimu wanapaswa kuwa wabunifu kwa kuitumia iliyopo kufundisha kwa weledi.

Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Profesa Carolyne Nombo amesema shindano hilo ni la pili na kwamba linahamasisha matumizi ya Tehama katika ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, tayari mazingira wezeshi yameshawekwa kwa ajili ya kuendelea kutumia Tehama, ikiwemo kuwapa walimu vishikwambi.

“Haihitaji ununue data ili kutumia intaneti kwenye vishikwambi hivyo kwa sababu tumeingia mikataba na kampuni za mawasiliano ikiwemo Airtel, kwa hiyo mwalimu anaweza kutumia bila kununua data,” amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Husna Sekiboko amesema kuna umuhimu wa kuandaa utaratibu wa kuwapa motisha walimu.

Amesema jambo hilo limekuwa likifanywa zaidi katika shule binafsi, huku za umma likidorora.

Mkurugenzi wa TET, Dk Aneth Komba amesema katika shindano hilo video za walimu zilikuwa zaidi ya 3,000 baadaye walichujwa na kubaki 25 kisha wakapatikana 10.

Tofauti na mwaka jana, amesema katika shindano la mwaka huu, halmashauri zote nchini zimehusishwa.

“Mwitikio umekuwa mkubwa na Benki ya Dunia ndiyo mfadhili kupitia mradi wa Burst,” amesema.

Katika shindano hilo, Mwalimu Jenipha Chuwa wa Shule ya Msingi Enaboishu Academy kutoka mkoani Arusha ameshinda na kuzawadiwa cheti na Sh3 milioni.

Mshindi wa pili ni Sophia Kawegere kutoka shule hiyo aliyepata cheti na Sh2.5 milioni na wa tatu ni Mwalimu Jenister Mmasi aliyepata cheti na Sh2 milioni.