Wakurugenzi waonywa kudharau, kubagua watumishi waliowakuta ofisini
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza jana Julai 21, 2026 wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali.
Muktasari:
- Tangu programu ya mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali ilipoanzishwa mwaka 2024, zaidi ya watendaji wakuu 187 wamepatiwa mafunzo hayo, huku viongozi wapatao 57 wakishiriki mwaka huu.
Dar es Salaam. Serikali imewaonya viongozi wanaoteuliwa kwa mara ya kwanza kuacha tabia ya kuwaona watumishi waliowakuta ofisini hawana uwezo na kukimbilia kufanya mabadiliko badala ya kuwajengea uwezo.
Hilo linatajwa kuchangiwa na baadhi yao kuingia madarakani wakiwa na mtazamo kuwa taasisi imejaa watu wasioweza kufanya kazi, jambo linalowafanya kutegemea zaidi washauri binafsi na kupuuza wataalamu waliopo.
Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo jana Julai 21, 2026 wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali.
Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Profesa Mkumbo amewataka viongozi hao kutokuwa sehemu ya changamoto bali kuleta mageuzi na mabadiliko kwani mwisho wa utendaji wao watapimwa kwa kile walichokifanya.
“Kuna viongozi ambao kila siku wanaeleza watumishi waliowakuta hawana uwezo, wanaomba wahamishiwe watu au wanabadilisha karibu kila kitu. Huo si uongozi unaotatua matatizo bali unaongeza,” amesema.
Pia, amesema wapo baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakibadilisha karibu watumishi wote wa taasisi kwa madai hawana uwezo, ilhali waliajiriwa kwa kufuata taratibu zote za Serikali huku akisema badala ya kuwaondoa ni vyema kuhakikisha wanapewa nafasi, mafunzo na uongozi bora ili kuongeza tija.
“Hata ukienda kwenye taasisi ukakuta changamoto, jukumu lako ni kuzitatua si kuzitumia kama sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yako,” amesema.
Amesema mafanikio ya Serikali yatapimwa kupitia utendaji wa taasisi zake, uwepo wa huduma zote muhimu ikiwemo afya, reli, elimu na miundombinu.
Ili kufikia hilo amewataka wakuu wa taasisi kuacha kujikita katika kutimiza taratibu pekee kama kufuata bajeti, sheria na ulipaji wa gawio badala yake waongeze thamani kwa kuchangia ajira, uwekezaji, mauzo ya nje, mapato ya Serikali na maendeleo ya viwanda.
Profesa Mkumbo pia aliwataka viongozi kuwekeza zaidi katika kuwajengea uwezo watumishi badala ya kulaumu vyuo vikuu kwa kutowazalisha wafanyakazi wenye ujuzi wote unaohitajika.
“Vyuo vikuu vinaelimisha lakini waajiri ndio wanaotoa mafunzo ya kazi. Ujuzi hubadilika kila siku hivyo ni wajibu wa taasisi kuendelea kuwanoa watumishi wake,” amesema.
Akizungumzia Dira 2050, Profesa Mkumbo amesema lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 hayatategemea ubora wa sera na mipango iliyoandaliwa pekee, bali uwezo wa viongozi wa taasisi za umma kutafsiri maono hayo kuwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
“Jukumu mlilonalo ni kubwa, tunahitaji viongozi wenye maono, uwajibikaji, ubunifu na uadilifu watakaoweza kutafsiri Dira 2050 kuwa matokeo yanayopimika,” amesema.
Amesema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, ushindani wa kimataifa wa kuvutia uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya masoko ya dunia, hivyo Taasisi za Umma hazina budi kubadilika ili ziwe sehemu ya suluhisho la changamoto za maendeleo. Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amewataka wakuu wa taasisi kuwasilisha mapendekezo ya mahitaji halisi ya rasilimali watu kulingana na majukumu ya taasisi zao ili kurahisisha upangaji wa ajira.
Amesema baadhi ya taasisi zina vifaa vya kisasa lakini zinakabiliwa na upungufu wa watumishi wenye ujuzi wa kuviendesha, hali inayopunguza ufanisi wa utoaji huduma.
“Hatutaifikia Tanzania tunayoitamani kwa kutegemea sera pekee. Tunahitaji taasisi zenye viongozi wanaoweza kutafsiri maono ya Taifa kuwa matokeo yanayopimika katika kila sekta,” amesema.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema tangu programu hiyo ilipoanzishwa mwaka 2024, zaidi ya watendaji wakuu 187 wamepatiwa mafunzo hayo, huku viongozi wapatao 57 wakishiriki katika awamu ya mwaka huu.
“Mafunzo hayo yanawajengea viongozi uelewa wa matarajio ya Serikali, utawala bora, uwajibikaji, usimamizi wa uwekezaji wa umma, matumizi bora ya rasilimali na uongozi unaozingatia matokeo,” amesema.
Amesema uwekezaji huo katika maendeleo ya viongozi tayari umeanza kuleta matokeo chanya, ambapo makusanyo ya gawio na michango yameongezeka kutoka Sh637 bilioni mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 108.
“Matokeo haya yanaonesha kuwa uwekezaji katika uongozi ni uwekezaji katika uchumi wa Taifa. Kadiri tunavyojenga viongozi wenye uwezo, ndivyo tunavyojenga taasisi zenye tija na kuongeza mchango wake katika mapato ya Serikali,” amesema.