Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yapiga hatua SDGs, yaweka mkakati mpya kuelekea 2050

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mafanikio hayo yameelezwa kuwa ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutekeleza Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030.

Dar es Salaam. Safari ya Tanzania katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) imeanza kuonyesha matokeo katika maeneo muhimu ya maisha ya wananchi, huku upatikanaji wa maji safi vijijini ukipanda hadi asilimia 85.3 na wananchi wanaofikiwa na umeme kufikia asilimia 86.2.

Mafanikio hayo yameelezwa ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutekeleza Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030, huku Tanzania ikiwasilisha tathmini yake ya tatu ya utekelezaji wa malengo hayo katika Jukwaa la Ngazi ya Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa (HLPF), linaloendelea New York, Marekani.

Akiwasilisha taarifa hiyo leo Jumatano, Julai 15, 2026 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema tathmini hiyo imekuja katika kipindi ambacho Tanzania inabadilika kutoka hatua ya kuripoti mafanikio kwenda kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo hayo, kabla ya mwaka 2030.

Amesema hatua mbalimbali zilizochukuliwa zimechangia maboresho katika sekta zinazogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.

Profesa Mkumbo amesema katika sekta ya maji, upatikanaji wa huduma hiyo vijijini umeongezeka kutoka asilimia 72.3 mwaka 2020 hadi asilimia 85.3 mwaka 2025, hatua inayotajwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa jamii nyingi.

Katika sekta ya nishati, Profesa Mkumbo amesema idadi ya wananchi wanaopata huduma ya umeme imeongezeka hadi asilimia 86.2, sambamba na ongezeko la uwezo wa Taifa kuuzalisha zaidi ya mara mbili.

“Hatua hizi zinaonyesha maendeleo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu zinazochochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao,” amesema Profesa Kitila.

Katika eneo la viwanda na miundombinu, linaloendana na Lengo la Tisa la SDGs, ameeleza mafanikio katika sekta ya usafiri wa reli, ambapo idadi ya abiria wanaotumia treni imeongezeka kutoka milioni 1.2 hadi milioni 4.1.

Ongezeko hilo limehusishwa na uwekezaji katika miundombinu ya usafiri unaolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumzia utekelezaji wa lengo la 17 linalohusu ushirikiano kwa maendeleo, Profesa Mkumbo alisema mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo.

“Zaidi ya mashirika 824 ya kiraia na taasisi 1,000 za sekta binafsi zilishiriki katika maandalizi ya taarifa hii,” amesema.

Amesema ushirikiano huo unaonyesha umuhimu wa ushiriki wa jamii nzima katika kufikia malengo ya maendeleo.

Katika eneo la kujitegemea kifedha, amesema uwezo wa Serikali kugharamia bajeti kupitia vyanzo vya ndani umeongezeka kutoka asilimia 58.3 mwaka 2020/21 hadi asilimia 78 mwaka 2025/26.

Pamoja na mafanikio hayo, Tanzania imeeleza kuwa bado inakabiliwa na changamoto ikiwemo kupunguza umaskini kwa kasi zaidi, kuongeza thamani katika uzalishaji wa viwandani, ajira kwa vijana, athari za mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa duniani ni kati ya asilimia 15 hadi 18 pekee ya malengo ya SDGs ndiyo yanayoelekea kufikiwa ifikapo 2030, huku mengine yakisonga taratibu au kukwama.