Wakulima wa ulezi kicheko, Tari ikizalisha mbegu tisa za kisasa

Mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa kilimo kituo cha Uyole Dk Denis Tippe (wa kwanza kulia) akimuonesha aina mojawapo ya mbegu iliyozalishwa na kituo hicho, Katibu Tawala Msaidizi wa uchumi na uzalishaji Mkoa wa Mbeya Said Madito wakati wakati wa maadhimisho ya siku ya mkulima wa zao la ulezi yaliyofanyika katika kituo hicho jijini Mbeya.
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, ulezi una kiwango cha juu cha wanga, zaidi ya asilimia 57 ambacho ni mara kumi ya baadhi ya mazao mengine ya nafaka yanayolimwa nchini.
Mbeya. Ili kufufua na kurejesha zao la ulezi, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kupitia Kituo cha Uyole jijini Mbeya, imeanza kuzalisha aina tisa za mbegu za kisasa zenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na visumbufu vya mimea.
Aidha, taasisi hiyo imeanzisha mpango maalumu wa kushirikisha wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini ili wachague mbegu tatu bora zaidi.
Lengo ni kuziwasilisha kwa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) kwa ajili ya usajili rasmi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Ulezi leo Jumamosi Julai 5, 2025, Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk Denis Tippe amesema hatua hiyo inalenga kufufua zao hilo la asili ambalo limeanza kupotea.
Amewaomba wananchi, hususan wakulima kutoa ushirikiano mkubwa.
“Ulezi ni miongoni mwa mazao ya asili ambayo kwa miaka ya karibuni yameanza kupotea. Tunafanya kila jitihada kulifufua kwa sababu lina umuhimu mkubwa kiafya na kibiashara,” amesema Dk Tippe.
Amebainisha kwamba ulezi una kiwango cha juu cha wanga, zaidi ya asilimia 57 ambacho ni mara kumi ya baadhi ya mazao mengine ya nafaka yanayolimwa nchini.
“Vilevile, ulezi una kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi na protini, ambavyo ni muhimu kwa afya ya binadamu, hasa katika kupambana na udumavu na magonjwa mengine,” amesema.
Ameongeza kwamba zao hili linaweza kustawi kwenye maeneo yenye kiwango kidogo sana cha mvua na haliathiriwi sana na visumbufu vya mimea.
“Ni zao la nafaka linaloweza kuhifadhiwa hadi miaka mitano bila kuharibika kwa sababu lina ganda gumu,” amefafanua.
Dk Tippe amesema katika utekelezaji wa mpango huo, kila mwaka wakulima watashirikishwa kuchagua mbegu tatu bora ili kuondoa changamoto ya ugeni wakati wa usambazaji. Amesema tayari kuna mbegu kadhaa ambazo zimesajiliwa.
Mtafiti wa ulezi katika kituo hicho, Bobnoel Asenga amesema wanafanya utafiti kwa kutumia mbegu za asili zilizokusanywa kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kuzalisha mbegu za kisasa na chotara kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
“Asilimia ya mbegu tunazozalisha zinalenga maeneo yenye ukame na zitapelekwa zaidi mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora kwa sababu zinahimili ukame na hukomaa kwa muda mfupi,” amesema Asenga.
Ameongeza kuwa, pia wanazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kaskazini ambayo hupata mvua nyingi.
“Ili kusogeza zaidi teknolojia kwa wakulima, tumeanzisha mashamba darasa kwenye halmashauri mbalimbali nchini, kushiriki maonyesho ya wakulima (Nane Nane) na kuanzisha maadhimisho ya Siku ya Ulezi.
“Hapa mkulima anachagua aina ya mbegu anayotaka. Akihitaji mbegu za asili tunampa, akitaka chotara tunampa na akitaka za kisasa tunampa. Lakini tunashauri watumie zaidi mbegu za kisasa kwa sababu zina tija kubwa,” amesema Asenga.
Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mbeya, Said Mdito amesema zao hilo ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la udumavu.
Amewataka wazazi kuwapatia watoto wao uji wa ulezi ili kupambana na udumavu na pia akawahimiza wajawazito kutumia uji huo kipindi chote cha ujauzito.
Mkulima wa zao hilo, Beldina Mwasenga, amesema hatua hiyo itawarudishia ari ya kulima zao hilo.
“Hizi ni juhudi ambazo sisi wakulima tulizihitaji kwa muda mrefu. Tunashukuru na kupongeza Serikali kwa hatua hii, lakini tunaomba mkakati huu uwe endelevu na uangalie pia upande wa bei ili kutukomboa,” amesema Beldina.