Prime
Mbinu za ulezi wa watoto zama za dijitali

Muktasari:
- Ulezi wa kidijitali ni uwezo wa mzazi au mlezi kuelewa, kuelekeza, na kusimamia matumizi ya teknolojia kwa watoto wao kwa njia salama, yenye faida na yenye usawa.
Katika dunia ya leo, ambapo watoto wanaweza kutumia simu kabla ya kujua kusoma, huku wanafunzi wakichota maarifa kwa njia ya mtandao, ulezi umeingia kwenye enzi mpya ya kidijitali.
Wazazi wanajikuta wakikabiliana na changamoto na fursa mpya katika kulea watoto waliozaliwa kwenye zama za teknolojia.
Watoto wa kizazi hiki wanakua wakiwa wamezungukwa na vifaa vya kielektroniki kama simu, tabiti, kompyuta na televisheni za kisasa.
Hali hii imebadilisha si tu namna wanavyopata elimu, bali pia jinsi wanavyocheza, kujifunza, na hata kujenga uhusiano wa kijamii.
Katika familia nyingi, vioo vya simu, runinga na vifaa vingine vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Muda mwingi macho ya watoto hayabanduki kwenye vioo hivi.
Wapo wazazi wanaouliza, ni kiasi gani cha muda wa kutazama vioo hivi kwa maana ya kutumia vifaa hivi kinachofaa?
Je, ni programu gani salama na zenye mafundisho na je, tunawezaje kuhakikisha watoto wetu wanajifunza kwa usalama bila kuwa watumwa wa teknolojia?
Changamoto kwa wazazi
Moja ya changamoto kuu ni kuweka mipaka. Katika baadhi ya familia, watoto hata wale wa miaka mitatu au minne, tayari wanajua kutumia mitandao kama YouTube au michezo ya kidijitali.
Kadri wanavyokua, wanajiunga na mitandao ya kijamii, wanazungumza na watu wasiowajua, na mara nyingine wanakumbana na maudhui yasiyofaa.
Aidha, kuna hofu ya madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya muda mrefu wanapotazama vioo vya vifaa hivi kama vilw matatizo ya macho, uzito kupita kiasi, usingizi duni na hata msongo wa mawazo au unyong’onyevu.
Watoto wanaweza pia kuathirika kijamii, wakikosa ustadi wa mawasiliano ya uso kwa uso na kuwa waoga kuhusiana na mazingira halisi.
Ni fursa kwa wazazi
Hata hivyo, teknolojia imeleta mabadiliko chanya pia. Wazazi wanaweza kutumia vifaa vya kidijitali kama nyenzo za kujifunzia.
Kuna programu zinazowasaidia watoto kujifunza hesabu, kusoma, au hata kujifunza lugha za kigeni. Pia, wazazi wengi wanafanya kazi kutoka nyumbani na wanaweza kutumia teknolojia kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.
Katika baadhi ya shule, wanafunzi sasa wanapewa kompyuta au tabiti kama sehemu ya mtalaa. Walimu wanatumia mitandao ya elimu kufundisha na kutoa kazi za nyumbani. Hali hii imewaweka wazazi kwenye nafasi ya lazima ya kuelewa teknolojia, hata kama wao wenyewe hawakulelewa nayo.

Ulezi wa kidijitali ni nini?
Ulezi wa kidijitali ni uwezo wa mzazi au mlezi kuelewa, kuelekeza, na kusimamia matumizi ya teknolojia kwa watoto wao kwa njia salama, yenye faida na yenye usawa. Hii ni pamoja na mosi, kuweka mipaka ya muda wa kutumia vifaa. Mzazi anaamua ni saa ngapi kwa siku mtoto atumie kifaa cha kidijitali, na kuhakikisha muda huo unatumika kwa shughuli zenye tija.
Pili, kuchagua maudhui sahihi kwa kuhakikisha watoto wanatazama au kutumia programu ambazo ni salama, zinazoelimisha na zinazowafaa kwa umri wao.
Tatu, kujadili hatari za mtandaoni kwa kuwaelimisha watoto kuhusu usalama wa kidijitali, kama vile kutowasiliana na watu wasiojulikana, kuepuka maudhui ya matusi au ya watu wazima, na kutoweka taarifa binafsi mtandaoni.
Nne, kuwa mfano mzuri kwani watoto hujifunza kwa kuiga. Wazazi wanapaswa kuonyesha matumizi mazuri ya teknolojia, kama vile kuweka simu pembeni wakati wa chakula au mazungumzo ya kifamilia.
Tano, kujenga mawasiliano ya wazi. Badala ya kutumia vitisho au makatazo, wazazi wanapaswa kujenga mazingira ya kuaminiana ambapo watoto wanaweza kueleza wanachokiona au kukutana nacho mtandaoni bila hofu.
Taarifa njema kwa wazazi
Kwa sasa, kuna programu na zana nyingi zinazowasaidia wazazi kufuatilia matumizi ya vifaa hivii kwa watoto wao. Programu kama Google Family Link, Qustodio na Bark, hutoa ripoti kuhusu muda wa matumizi, aina ya maudhui yanayotazamwa na hata tahadhari za usalama.
Aidha, familia unaweza kuweka sheria ya matumizi ya teknolojia kati ya mzazi na mtoto, wakikubaliana kwa pamoja juu ya matumizi ya vifaa vya kidijitali kama vile kutotumia simu wakati wa chakula au muda wa kulala.
Kwa sasa na kwa miaka mingi ijayo, wazazi hawana budi kuwa na uelewa wa kina kuhusu teknolojia. Kusimamia matumizi ya vifaa si jambo la kupiga marufuku tu, bali ni safari ya pamoja kati ya mzazi na mtoto –safari ya kuelekeza, kujifunza na kulinda.
Ulezi wa kidijitali ni sehemu muhimu ya malezi ya kisasa. Ni nafasi ya kuwajenga watoto kuwa raia wa mtandaoni wenye uwajibikaji, wanaojitambua, na wenye maarifa ya kutumia teknolojia kwa njia chanya. Wazazi hawahitaji kuwa wataalamu wa Tehama bali wanahitaji kuwa karibu na watoto wao kidijitali na kihisia.