Wafanyabiashara Iringa wafunga maduka, wananchi wahaha

Muktasari:
- Hali hiyo imetokea baada ya wafanyabiashara kutangaza mgomo wa kutofungua maduka kuanzia leo Mei 12, 2025 kwa muda usiojulikana, kuishinikiza Serikali ya mkoa kuwaondoa wafanyabiashara holela katikati ya mji wa Iringa na kuwarudisha katika maeneo yao rasmi ya kufanyia biashara.
Iringa. Wananchi wa Mkoa wa Iringa wamejikuta katika hali ya taharuki na usumbufu, kufuatia kufungwa kwa biashara nyingi katikati ya mji kuanzia asubuhi ya leo, Mei 12, 2025.
Tukio hilo limeathiri upatikanaji wa huduma na bidhaa muhimu kwa wakazi wa Iringa, ambao kwa kawaida hutegemea sana biashara za mjini kwa mahitaji yao ya kila siku.
Katika mahojiano na Mwananchi Digital, leo Mei 12, 2025 baadhi ya wakazi wa Iringa wameeleza kuwa walikuwa na shughuli muhimu za kufanya, lakini wamekosa huduma nyingi ikiwemo chakula, mavazi na vifaa vya ujenzi.

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa. Picha na Christina Thobias
Aidha hali hiyo imesababisha watu wengi kurandaranda mitaani wakitafuta maduka yaliyofunguliwa, bila mafanikio kwani baadhi ya yaliyofunguliwa si yale ya mahitaji ya msingi.
Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Iringa, wapo katika kikao katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, lengo ni kujadili hali hiyo na kuitafutia ufumbuzi.
Janeth Aloud, mkazi wa Mkwawa amesema aliamka mapema kwenda kununua mahitaji ya familia, lakini ameshangazwa kukuta maduka yote makubwa na madogo yakiwa yamefungwa.

Baadhi ya maduka mtaa wa stendi ya zamani ya mabasi katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa yakiwa yamefungwa. Picha na Christina Thobias.
"Nilifika sokoni leo asubuhi kutafuta mahitaji ya nyumbani, lakini maduka yote yamefungwa. Sina uhakika nitapata wapi bidhaa hizi sasa," amesema Janeth.
Hata hivyo, Janeth amesema hali hiyo inawavunja moyo wananchi wanaotegemea kununua bidhaa kwenye maduka ya jumla mjini kwa ajili ya kwenda kuchuuza wanakoishi.
Nao walanguzi wa bidhaa mbalimbali kutoka maeneo ya vijijini wameeleza kusikitishwa na hali hiyo, wakisema walifunga safari mapema alfajiri ili kuja mjini kununua bidhaa za kuuza, lakini wamekuta mji umenyamazishwa ghafla.

Naye Lucy Nyato ameeleza jinsi alivyoshangazwa na hali ya kufungwa kwa maduka kwani huduma za msingi zimekuwa ni changamoto kupatikana.
"Nimetoka kijijini kuja mjini kununua bidhaa, lakini nimekuta maduka yamefungwa. Hii imeniletea hasara kubwa," amesema Lucy kutoka kijiji cha Uhambingeto mkoani Iringa na kuongeza;

"Tunaomba Serikali ichukue hatua za haraka kutatua mgogoro huu, ili maisha yaendelee kama kawaida na hatujui hali hii itaendelea hadi lini. Tunahitaji suluhisho la haraka."
Lakini pia wachuuzi hao wamesema kuwa wamepoteza muda na gharama za usafiri bila mafanikio yoyote.
“Mimi natoka Kilolo, nimetoka saa 10 alfajiri ili nifike mjini mapema, lakini nimekuta hali kama hii. Hata kupata mkate wa chai ni taabu,” amesema Mzee Rashid Othuman, muuza bidhaa za nyumbani.
Mzee Rashid ameongeza kuwa bado hajajua kama atasubiri hadi usiku au kugeuza na kurudi kijijini bila mzigo.

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa. Picha na Christina Thobias
Vilevile wengine wameeleza hofu kuwa hali hiyo inaweza kuchochea kuibuka kwa ulanguzi wa bidhaa mtaani, kutokana na uhaba wa huduma rasmi na kuiomba Serikali ya mkoa na mamlaka husika kuingilia kati, ili kudhibiti hali isije kuwa mbaya zaidi.
“Tumeamua kufunga maduka yetu kama njia ya kuishinikiza Serikali kutusikiliza. Wafanyabiashara holela wanatuharibia biashara zetu kwa kuuza bidhaa mbele ya maduka yetu,” amesema John Kingu mmoja wa wafanyabiashara kutoka mkoani Iringa.
“Hatuwezi kuendelea kufanya biashara katika mazingira haya ya ushindani usio wa haki. Tunahitaji Serikali ichukue hatua madhubuti,” amesema Grace Mlowe, mfanyabiashara wa vifaa vya nyumbani kutoka mkoani Iringa.
“Nimeamua kufungua duka langu kwa sababu sina njia nyingine ya kujipatia kipato. Ingawa ninaunga mkono madai ya wenzangu, maisha lazima yaendelee,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye hakutaka jina lake lifahamike.
“Kufunga duka ni hasara kubwa kwangu. Nategemea biashara hii kulipa ada za watoto na mahitaji mengine ya familia,” ameongeza.