Mgomo wa wafanyabiashara Tunduma wafunga maduka, Arusha nao ‘wabip’

Maduka ya soko kuu la Manzese katika Halmashauri ya mji wa Tunduma Mkoani Songwe yakiwa yamefungwa. Picha na Denis Sinkonde

Muktasari:

  • Unaweza kusema ni kama mgomo wa wafanyabiashara unazidi kutamaliki, wafanyabiashara wa mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Dodoma na Iringa wameingia kwenye mgomo na maduka yao yamefungwa wakisubiri tamko la Serikali kuhusiana na madai yao.

Songwe/ Arusha. Wakati wafanyabiashara wa maduka maeneo ya soko kuu katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba, mkoani Songwe wakifunga maduka yao leo, mkoani Arusha wao waliyafunga kwa saa mbili kuanzia saa moja asubuhi.

Ilipofika saa tatu asubuhi wakakubaliana kuyafungua kwa madai ya kuendelea kusubiri majibu kutoka kwa viongozi wao waliokwenda Dodoma kufanya mazungumzo na Serikali.

Matenga ya nyanya ya baadhi ya  wafanyabiashara yakiwa katika geti kuu ya kuingilia kwenye soko hilo la Manzese.

Wafanyabiashara hao wameungana na wenzao wa mikoa ya Dar es Salam, Mbeya, Mwanza na leo Iringa na Dodoma kuendeleza mgomo huo ulioanza juzi Jumatatu Juni 24, 2024 unaoshinikiza Serikali kuondoa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali ambazo wadai si rafiki kwao.

Leo Jumatano Juni 26, 2024, Mwananchi Digital imetembelea baadhi ya maeneo nchini, kushuhudia maduka makubwa yakiwa yamefungwa, hususan kwenye mikoa iliyotajwa.

Kutokana na mgomo huo, katika Mji wa Tunduma, baadhi ya wafanyabiashara kutoka nchi za Malawi, Zambia na Congo wanaotegemea kununua bidhaa kwa bei ya jumla kwenye maduka yaliyopo eneo la Soko kuu katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma wamesema hali hiyo inawaongezea gharama na kupoteza muda na kwmaba hawajui mgomo huo utakwisha lini.

Mfanyabiashara kutoka Zambia, Julita Nsamweya amesema atalazimika kutumia gharama kubwa kununua bidhaa kwa wafanyabiashara wadogo ambao bei zao si sawa na zile za maduka ya jumla.

"Tunategemea maduka ya Tunduma kunumua mizigo, lakini leo imekuwa kero kwetu, tunalazimika kununua mzigo kwa bei kubwa. Mfano mzigo wa Sh1.2 milioni leo tunaununua kwa Sh1.5 milioni, hii ni hasara, naiomba Serikali ya Tanzania ikae chini na hawa watu wamalize tofauti zao,” amesema Nsamweya.

Naye mbeba mizigo wa soko la Manzese, amesema kufungwa kwa maduka hayo kumeathiri uingizaji wa kipato chake.

Amesema kazi yake ya kubeba mizigo ndiyo inayompatia mahitaji yake muhimu ya kila siku na familia yake.

Baadhi ya wafanyabiashara ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wameitaka Serikali iondoe utitiri wa kodi.

“Tunaumia, tumevumilia kwa muda mrefu sasa tumefika kikomo, Serikali isiposikiliza kilio chetu, basi hatutafungua maduka,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Mwingine amehoji; “Iweje ukikutwa na kosa faini unatozwa Sh15 milioni wakati mtaji wako waSh10 milioni, hii haikubaliki, hatuwezi kufanya biashara ya kuitumikia Serikali.”

Viongozi wa Soko la Manzese hawajapatikana kuzungumzia sakata hilo na Mwananchi inaendelea kuwatafuta.

Hata hivyo, Mwananchi imewashuhudia baadhi ya wanyabiashara wa maduka madogo yaliyoko pembezoni wakiendelea na biashara na wanunuzi wengi wakielekea huko.


Hali ilivyokuwa Arusha

Katika Jiji la Arusha baadhi ya wafanyabiashara nao walifunga maduka kwa saa mbili kabla ya kufikia uamuzi wa kuyafungua kwa madai wanasubiri majibu ya viongozi wao waliokwenda Jijini Dodoma kufanya mazungumzo na Serikali.

Hata hivyo, wamesema wataungana na wafanyabiashara wa mikoa mingine kuendeleza mgomo, iwapo mkutano wa viongozi wao na Serikali hautajibu hoja walizoziwasilisha.

Hoja za wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha mbali na utitiri wa kodi na tozo, pia wanadai mazingira mazuri ya ufanyaji biashara pamoja na kuondolewa kwa machinga mbele ya barabara zinazopakana na maduka yao.

Akizungumza na Mwananchi digital, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Adolf Locken amesema wamefanikiwa kuuzima mgomo huo ulioanza alfajiri hadi saa mbili asubuhi.

"Wenzetu wametuelewa na wamefungua maduka kwa sharti la kupata majibu ya hoja zao kutoka kwa viongozi wa wafanyabiashara walioko Dodoma wanaoendelea na majadiliano na Serikali juu ya kutatua kero hizo" amesema Locken.

Mfanyabiashara, Amina Ally wa duka la nguo amedai faini wanazotozwa na TRA za Sh15 milioni kwa kosa la kutokutoa risiti za Kielektroniki (EFD) inawaumiza.

“Hatufanyi makusudi kutotoa hizo risiti, tuna sababu zinazotufanya tusitoe, kwa hiyo watusikilize wasitushinikize.

"Hivi umewahi kuona wapi mtu nauza nguo ya Sh7,000 au 12,000 na  mteja anaondoka kwa haraka zake au mashine inasumbua halafu unaletewa faini ya Sh15 milioni! Kama huu si uonevu ni nini sasa, hatutaelewa endapo viongozi wetu hawatakuja pia na majibu ya hili.”

Ezekiel Mbise, amesema tatizo lingine ni kuruhusiwa kwa machinga kupanga bidhaa zao mbele ya maduka yao, kuwa inawanyima wateja na kujikuta wakifunga hasara kila mwezi.

Mgomo wa wafanyabiahsara ulioanzia Kariakoo, jijini Dar es Salaam kabla ya kupokewa jana na mikoa ya Mwanza na Mbeya hoja kubwa ni unyanyasaji wanaodai kufanywa na  Mamlaka ya ukusanyaji Mapato nchini (TRA), ikiwemo utitiri wa Kodi na tozo.

Licha ya Waziri wa Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo kutangaza kusitishwa kwa ukaguzi wa risiti za Kielektroniki (EFD), bado wafabiashara hao wameendelea na mgomo kwa madai kuwa tamko hilo ni la kisiasa.