Wafanyabiashara Mbeya, Mwanza wakomaa na mgomo, Iringa nao walianzisha

Hali ilivyo katikati ya mji wa Iringa, maeneo ya Miyomboni

Muktasari:

  • Mgomo wa wafanyabiashara hao ulianza jana wakishinikiza Serikali ifanyie kazi malalamiko yao kuhusiana na kodi na tozo nyingine.

Mbeya/Iringa/Mwanza. Wakati wafanyabiashara katika mkoa ya Mbeya na Mwanza wakiendelea na mgomo waliouanza jana, mkoani Iringa nako wamegoma.

Mgomo wa wafanyabiashara hao wa maduka jijini Mbeya na Mwanza ulianza jana Juni 25, unalenga kuishinikiza Serikali kuondoa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali ambazo si rafiki kwa wafanyabiashara.

Leo Jumatano Juni 26, 2024, Mwananchi Digital ambayo ipo maeneo ya Soko la Sido, Mwanjelwa na Kabwe imeshuhudiwa maduka makubwa yakiwa yamefungwa, huku madogo ya pembeni yakiendelea kutoa huduma.

Hata hivyo,  wafanyabiashara ndogo ndogo ‘mamchinga’ wanaendelea kuuza bidhaa zao, ingawa kwa kificho.

Mwananchi ilipotaka kuzungumza na wafanyabiashara hao, hakuna aliyekuwa tayari kuzungumzia mgomo huo.


Mkoani Iringa

Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa wameungana na wenzao kufunga maduka wakiishinika Serikali kusikiliza malalamiko yao dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mwananchi Digital imepita katika maeneo ya Manispaa ya Iringa, hasa katikati ya mji maeneo ya Miyomboni na kukuta maduka karibu yote yamefungwa.

Baadhi ya wanunuzi wamelalamikia hali hiyo na kuiomba Serikali iingilie kati kumaliza mgomo huo.

Mmoja wa wafanyabiashara, Enock Jonde amesema wameamua kuungana na wenzao kwenye mikoa waliofunga biashara kuonyesha kuwa hali iliyopo inawaumiza.

“Hatuwezi kuendelea kufanya biashara katika mazingira haya ya kuwa na kodi lukuki, kamatakamata, hatuwezi,” amesema Jonde.

Jitihada za kuwapata viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Iringa zinaendelea.


Hali ilivyo Jijini Mwanza

Wakati Polisi wakitapakaa mitaani Jijini Mwanza, wafanyabiashara wao wanaendelea na mgomo wao waliouanza jana Jumanne Juni 25, 2024.

Wapo maofisa wa Jeshi la Polisi wanaotembea na waliopo kwenye magari, wakipita katika mitaa mbalimbali ya jijini hilo, huku maduka yakiwa yamefungwa.

Kamera ya Mwananchi Digital iliyoko mtaani kuanzia saa 12:30 hadi saa 3:00 asubuhi ya leo Jumatano Juni 26, 2024, imeshuhudia magari yaliyojaa askari wa Jeshi la Polisi yakikatiza mitaani, huku baadhi ya askari polisi wakitembea kwa miguu kuzunguka mitaa ya jiji hilo.

Alipoulizwa kuhusu askari hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kuwasambaza askarimitaani, huku akidokeza kuwa jukumu lao ni kuimarisha ulinzi kwa wafanyabiashara watakaofungua maduka wasifanyiwe fujo na waliogoma.

Kamanda Mutafungwa amesema ulinzi na doria hizo zitakuwa endelevu hadi hali itakaporejea katika utimamu na kuwaonya watakaojaribu kuwafanyia vurugu wafanyabiashara walioridhia kufungua maduka yao.

Imeandikwa na Allen Msungu (Iringa), Saddam Sadick (Mbeya na Mgongo Kaitira (Mwanza).