Jeshi la Polisi Mwanza latoa kauli mgomo wa wafanyabishara

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa akizungumza muda mfupi baada ya kufanya doria katika mitaa mbalimbali ya Jiji hilo kufuatilia sakata la mgomo wa wafanyabiashara. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Mgomo wa wafanyabiashara unalenga  kupinga sheria za kodi wanazodai zinachangia unyonyaji na kuwarudisha nyuma

Mwanza. Wakati baadhi ya wafanyabiashara jijini Mwanza wakigoma na kufunga maduka, Jeshi la Polisi limewataka walioridhia kufungua maduka na wafanye biashara kwa amani kwa kuwa ulinzi umeimarishwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Juni 25, 2024, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa baada ya kufanya doria yenye lengo la kuangalia hali ya usalama katika mitaa mbalimbali ikiwamo ya Rwagasore, Kaluta, Uhuru, Liberty, Nyamagana na Miti Mirefu.

Kamanda Mutafungwa amesema jeshi hilo lilijulishwa uwepo wa mgomo huo kuanzia asubuhi ndipo lilipoanza kusambaza maofisa wenye sare na wasiyo na sare ili kuimarisha ulinzi katika maduka ya wafanyabiashara waliokubali kufungua.

“Tumeimarisha hali ya usalama tangu asubuhi kwa sababu kuna waliokubali kufungua maduka. Tukawa tunapokea taarifa kwamba wanaotaka kufungua wamekuwa wakizuiwa na wale ambao wamefunga tumeimarisha ulinzi na wanaendelea na biashara zao bila kubugudhiwa,” amesema Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa amesema doria hizo zitakuwa endelevu hadi pale mgogoro huo utakapomalizika huku akiwataka waliogoma kutotumia njia hiyo badala yake watumie njia rasmi kuieleza Serikali malalamiko yao.

“Walioridhia kufungua maduka wasiwe na hofu ya aina yoyote ulinzi umeimarishwa katika viunga vyote vya Mkoa wa Mwanza, askari wanafanya doria za magari na miguu, wako tayari kumdhibiti atakayewafanyia vurugu wafanyabiashara waliokubali kufungua maduka yao,” amesema Mutafungwa.

Mfanyabiashara na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa (NEC), Ezekiel Mollel amekosoa uamuzi wa wafanyabiashara hao akisema huenda usilete matokeo wanayotarajia kwa kile alichodai mgomo siyo njia sahihi ya kupata wanachokitaka.

“Niwaombe wafanyabiashara fungueni maduka, mgomo siyo utatuzi, kugoma hakuleti jawabu, acheni kufunga biashara kufanya hivyo ni kumuumiza mwananchi wa chini, mnapofunga biashara mnaua uchumi wa nchi yetu,”amesema  Mollel.

Mfanyabiashara aliyefungua duka eneo la Makoroboi, Hoja Mashingi amesema haamini iwapo mgomo unaweza kuwapatia kile wanachodai zaidi ya kuwapatia hasara.

Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa nje ya maduka yao yaliyofungwa katika mtaa wa Lumumba jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati ametaja sababu za mgomo ni kupinga sheria za kodi zinazochangia unyonyaji na kuwarudisha wafanyabiashara nyuma.

"Hiki ambacho kimewasukuma wafanyabiashara kusitisha biashara zao ni yale ambayo yanaendelea kuhusiana na sheria za kodi. Sheria za kodi zimekuwa tatizo," amesema Masagati.

Alipoulizwa ukomo wa mgomo huo, Masagati amesema hawezi kuweka wazi lini utakoma kwa kile alichodai jukumu ya kusitisha mgomo huo limekabidhiwa mikononi mwa wafanyabiashara wenyewe.

 “Malalamiko na matamanio ya wafanyabiashara ni kuona sheria zinazosimamia wafanyabiashara zimerekebishwa,” amesema Masagati.