Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wapata wasiwasi utekelezaji mtalaa mpya

Muktasari:

  • Wakichangia mjadala wa Mwananchi kwenye mtandao wa X wadau hao wameonyesha wasiwasi kwa Serikali kujipanga katika utekelezaji wa sera mpya ya elimu, inayoanza kutumika mwaka huu.

Dar es Salaam. Waziri kivuli wa elimu wa chama cha ACT- Wazalendo, Riziki Mngwali ameonyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa sera mpya ya elimu inayoanza kutumika mwaka huu.

Hivi karibuni Serikali ilitoa waraka wa elimu Namba 5 ambao pamoja na mambo mengine, unafupisha elimu ya msingi kutoka miaka saba hadi sita na somo la Kiingereza kuanzia darasa la kwanza.

Akichangia mjadala wa mtandao wa X wa Mwananchi leo Jumatano Januari 3, 2024 wenye mada iulizayo ‘Kuanza kutumia mtalaa mpya wa elimu je, tumejipanga kikamilifu?’ Mngwali amehoji namna nchi ilivyojiandaa katika utekelezaji wa sera hiyo huku akigusia elimu ya amali.

“Hizo amali chache tulizokuwa nazo hakukuwa na walimu wa kutosha au kukidhi, tunapoongeza fursa za taaluma ya elimu ya amali tumejiandaa vipi.

“Tunaambiwa somo la Kiingereza wanafundishwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza je, walimu wameandaliwa. Haya tumesikia darasa la tatu watafundishwa Kiingereza kwa wiki sita vipi maandalizi ya hao walimu,” amehoji.

Amesema haoni kama walimu wameandaliwa kuendana na mabadiliko yanayotakiwa ya kutengeneza wanafunzi wenye ujuzi.

“Ukweli ni kwamba hatujajipanga, lugha ya kufundishia imekuwa changamoto na kilio kikubwa lakini sera na mitaala mipya haijaondoa tatizo hilo,”amesema.

Akizungumzia jamii, amesema hata yenyewe baadhi yao ukiiuliza kuhusu sera na mitaala mipya wala hawaelewi.

Amehoji mchakato wa uandaaji wa sera hiyo kama ulihusisha wadau moja kwa moja, huku akitoa mfano wa mchakato wa Katiba mpya uliowafikia watu wengi, lakini huu haujawafikia licha ya umuhimu wake kwa kuwa unagusa wanajamii.

Amesema kuwa hali inaonyesha hatujajipanga hivyo amesema bado Serikali inapaswa kujipanga zaidi.

Wasiwasi wa Mngwali unaungwa mkono na spika wa bunge la wananchi, Suzan Lyimo aliyesema Serikali haijajipanga.

Amesema walitegemea katika kipindi cha miaka tisa kutoka 2014 hadi 2023 Serikali itakuwa imejipanga kikamilifu.

“Kuna tatizo kubwa la kimfumo changamoto ya kwanza ni utata wa lugha ya kufundishia unapokuwa na nchi moja yenye lugha ya kufundishia au mitaala tofauti ni ubaguzi wa hali ya juu,” amesema.

Ameongeza kuwa kuna shule za Serikali sasa hivi zinafundisha Kiingereza, inakuwaje nchi moja kunawepo ubaguzi: “Kilichofanyika ni kubadilisha tu muundo elimu ya Tanzania kwa maana ya kubadilisha miaka, maudhui hayajabadilika.

 “Hata huu uwepo wa shule za amali hazitatubadilishia wanafunzi wetu kifikra na kiakili, hatuna vifaa, wala walimu katika shule hizi,’ amesema.

Amesema shule za ufundi zinahitaji kuwa na vifaa vingi vya kufanyia mazoezi. Mambo yatakuwa yale yale hakuna kilichobadilika.

 “Serikali ihakikishe kuna walimu wa kutosha na wenye sifa, pia waboreshewe masilahi ili wafundishe vizuri,” amesema.                                                                                                                                  

Naye John Sebastian akichangia mjadala huo amesema kilio kikubwa cha Watanzania ni suala la ubora katika elimu.

"Suala la mabadiliko ya mitaala ni zuri lakini tumefanya haraka bila kujiandaa vizuri. Ni kwa namna gani katika siku hizi chache walimu wataweza kuangalia muongozo, vitabu na kujiandaa kuwafundisha wanafunzi.

"Je, walimu wamepewa mafunzo ya namna gani kuhakikisha wanaelewa kilichopo kwenye mtaala ili wakafundishe inavyopaswa,”amesema na kuhoji.