Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Undani mtalaa mpya wa elimu 2024

Macho na masikio yapo kwenye mtalaa mpya utakaoanza kutekelezwa Januari 2024 kwa madarasa ya awali, msingi na sekondari, ikiwa ni juhudi za Serikali kutekeleza malengo ya mafunzo ya amali.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza, la pili na la tatu, wataanza kutekeleza mtaala ulioboreshwa kuanzia Januari, 2024 ambapo watasoma elimu ya msingi na kuhitimu kwa miaka sita kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza.

Utekelezaji wa mtaalaa ulioboreshwa kwa elimu ya sekondari ya chini, mkondo wa awali utaanza mwezi Januari 2024 kwa baadhi ya shule zilizothibitika kuwa na mahitaji maalumu ambapo watakaohitimu watakuwa na vyeti viwili.

Watapata cheti cha mafunzo kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET) na kingine kitatolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta). Wanafunzi wa sekondari mkondo wa jumla, watatunukiwa cheti kimoja na Necta.

Kwa mujibu wa waraka mpya, elimu ya sekondari ya juu mkondo wa jumla itatolewa kwa miaka miwili na elimu ya amali sanifu itatolewa kwa miaka mitatu na Kwa mujibu wa Dk Mtahabwa, mapitio ya sera na uboreshaji wa mitalaa yalishirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, vyuo vya kati, shule za msingi na sekondari, wahadhiri, wakufunzi na walimu kutoka vyuo vikuu.

Wadau wengine walioshiriki katika mchakato huu, kwa mujibu wa kamishna ni pamoja na wabunge, viongozi wa dini na wakuu wa taasisi za elimu.


Muundo mpya

Moja ya maeneo yaliyoboreshwa ni muundo wa elimu ambao utakuwa 1+6+4+2/3+3+, yaani elimu ya awali itatolewa kwa mwaka mmoja, elimu ya msingi miaka sita, elimu ya sekondari ya chini miaka minne, elimu ya sekondari ya juu miaka miwili au mitatu kwa mkondo wa amali na elimu ya juu miaka mitatu au zaidi kulingana na programu husika.

Elimu ya sekondari na msingi itakuwa ya lazima na itatolewa bila ada, huku umri wa kuandikisha mtoto elimu ya awali ukiwa ni miaka mitano na umri wa kuanza darasa la kwanza ukiwa ni miaka sita.

Kwa maana hiyo elimu ya msingi na sekondari itakuwa ni ya lazima kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.

Baadhi ya masomo mapya yatakayofundishwa ni pamoja na Historia ya Tanzania na maadili, huku kompyuta, mawasiliano ya kitaaluma na mafunzo ya biashara yakipewa kipaumbele.

Lugha ya Kiingereza itaanza kufundishwa kuanzia darasa la kwanza kwa shule za umma na binafsi tofauti na mwanzo ambapo shule za umma zilifundishwa lugha hiyo kuanzia darasa la tatu.

Kwa mujibu wa waraka, mwaka wa masomo utakuwa na siku 194 sawa na wiki 39 na umegawanyika katika mihula miwili inayolingana.Katika kila muhula wiki mbili zitatumika kwa ajili ya upimaji endelevu na tamati.

Vipindi na muda wa ufundishaji na ujifunzaji katika elimu ya msingi utakuwa dakika 30 kwa kila kipindi kwa darasa la kwanza na la pili na dakika 40 kila kipindi kwa darasa la tatu hadi la sita.

Katika eneo la dira, malengo na umahiri wa jumla, mtaalaa umelenga kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi na mitazamo chanya, anayethamini usawa, haki na elimu bila ukomo katika kuleta maendeleo endelevu ya kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wa mtalaa huo, maeneo ya kujifunza na umahiri mkuu kwa darasa la kwanza na la pili yamezingatia ujenzi wa lugha, mawasiliano na stadi za hisabati, utamaduni, sanaa, michezo na afya na mazingira.

Kwa darasa la tatu hadi la sita, maeneo ya kujifunza na masomo yamezingatia kumjengea mwanafunzi umahiri wa lugha na mawasiliano, hisabati, sayansi ya jamii, sayansi na teknolojia na sanaa na michezo.

Katika eneo la lugha, wanafunzi hao watajifunza masomo ya lugha za Kiswahili, Kiingereza, Kichina, Kiarabu na Kifaransa.

Mtalaa umeelekeza kuwa katika eneo la sayansi ya jamii, watakuwa na masomo ya historia ya Tanzania na maadili, jiografia na mazingira, hisabati, sayansi, sanaa na michezo.

Sera inatamka kuwa lugha ya Kiswahili itatumika kama lugha ya kufundishia katika shule zinazotumia Kiswahili na Kiingereza kitatumika katika shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kujifunzia na kufundishia.

Aidha, masomo ya lugha za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kichina na Kiarabu yatafundishwa kwa lugha inayohusika.


Hofu utekelezaji wa mtalaa

Kulingana na mipango iliyopo kuwa mingi katika utekelezaji wa waraka mpya, bajeti iliyotengwa kwa ajili ya elimu ni ndogo.

Katika mtazamo wa haraka wafuatiliaji wa maendeleo ya elimu nchini watagundua kuwa bado tuna uahaba mkubwa wa vifaa muhimu vya elimu kama madawati na vitabu.

Mathalani, shule nyingi Dar es Salaam bado watoto wanakaa chini. Idadi ya watoto darasani iliyopendekezwa na wathibiti ubora wa elimu ni 45 kwa kila darasa lakini hali ni tofauti.

Kama ingekuwa ni kutaja majina ya shule husika wilayani Temeke, Kata ya Mbagala, kwa mfano si ajabu kukuta darasa moja likiwa na wanafunzi zaidi ya 80.

Tunapozungumzia waraka na mipango mizuri ya kuboresha elimu, ni lazima tujikite katika uwekezaji wa kutosha ili kuendana na viwango vya kimataifa vinginevyo nchi jirani wataweza kutumia mipango yetu na kuitekeleza huku sisi tukibaki na shauku ya kuiga wanayoyafanya bila kufahamu kuwa maarifa hayo yalichotwa nchini kwetu.

Wakati Tanzania inahangaika na bajeti ya asilimia 14 katika elimu, mwaka 2017, Finland ambayo ni nchi maarufu duniani kwa kutoa elimu bora, ilitenga zaidi ya Euro 4.7 bilioni karibia asilimia 40 ya bajeti ya nchi kwa ajili ya elimu, huku Euro 2.3 billioni ambazo ni takribani asilimia 19 zikitumika katika tafiti na ubunifu.

Kwa historia, Finalnd ni nchi iliyoendelea kiuchumi zaidi ya Tanzania, lakini imefikia hapo kwa sababu mipango yao inaweza kutekelezeka.

Tanzania ina wasomi wengi kama ambavyo wameshirikishwa wakati wa kuandaa rasimu ya mtalaa mpya wa elimu lakini huenda tatizo kubwa lipo kwenye utekelezaji.

Tukijikumbusha adha zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Elimu kwa Shule za Msingi (MMEM) miaka kadhaa iliyopita ni kwamba wengi walipata elimu pasipo walimu wa kutosha, ubora ulitiliwa shaka na msisitizo mkubwa uliwekwa kwenye wingi bila umahiri na ubunifu.

Kwa sasa mpango wa wingi tumeufanikisha kupitia elimu bila ada lakini je ubora utapatikana kwa mtalaa huu mpya? Tumewaadaa walimu wa kufundisha?

 Je, walimu wana hamasa na motisha ya kutosha kukidhi matakwa haya? Je, lugha ya Kingereza ikianza kufundishwa kuanzia darasa la kwanza tuna uhakika na uwezo wa walimu hasa shule za umma kuweza kufundisha kwa umahiri?

Tukitafuta majibu ya maswali haya tutajikuta tunarudi kulekule. Waraka mpya wa mtaala huu unasema kwamba walimu wataandaliwa kwa kipindi cha miaka miwili na uanagenzi (internship) utakuwa ni lazima ufanyike kwa mwaka mmoja, huku vyuo binafsi vya ualimu vikipewa msisitizo wa kutekeleza hitaji hili.

Pamoja na hayo, waraka upo kimya juu ya muda utakaotumika kuwanoa walimu wa kutekeleza mtalaa mpya kwa wiki sita za mwanzo kuanzia mwezi Januari 2024.

Matatizo mengi yanayochangiwa na utekelezaji duni wa mipango mizuri ya elimu nchini, yametokana na uwekezaji duni.

Nchi yetu inawekeza asilimia sita tu ya pato la ndani (GDP) kwa ajili ya elimu, kinyume kabisa na malengo ya elimu kwa wote kama yalivyo pendekezwa Shirika la Elimu la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) katika makubaliano yaliyosainiwa na nchi wanachama nchini Senegal.

Makubaliano hayo yalizitaka nchi wanachama kutenga alimia tisa ya pato la ndani kwa ajili ya elimu.

Badala ya kuwahi kutekeleza mpango, tujikite zaidi kwenye uwekezaji. Nia ya kuwa kama Finland tunayo, nyenzo tunazo, tumuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassani kwa vitendo.