Wanafunzi 319 kuwezeshwa kupata elimu

Wanafunzi wakiwa darasani. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Wanafunzi 19 watasomeshwa bure katika shule za Paradise Mission ya mkoani Mbeya na Patrick Mission ya Dar es Salaam, 300 kupatiwa sare.
Dar es Salaam. Ni miaka takribani 10 sasa tangu Serikali ilipotangaza kufuta ada kwa shule za msingi nchini.
Hatua hiyo imechochea ongezeko la wanafunzi kwenye shule za umma kwa wazazi na walezi kupata mwamko wa kupeleka watoto shule.
Mpango wa kufuta ada kwa shule za msingi na baadaye sekondari ulipitishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, ukilenga kila mtoto aliyefikisha umri wa kwenda shule anapata haki hiyo bila kikwazo.
Hata hivyo, wapo wanafunzi wanashindwa kuendelea na masomo kwa kukosa huduma zingine muhimu kama vile za chakula na michango mbalimbali, ambayo wazazi wanatozwa ili kuchangia uendeshaji wa shughuli za shule.
Takwimu zinaonyesha kati ya wanafunzi 1.3 milioni waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2023, wanafunzi 40,901 hawakufanya mtihani huo.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa ni utoro, wazazi kukwepa kuchangia michango hivyo, watoto kukosa haki ya kupata elimu.
Pia, wanafunzi 263,336 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2023, walifeli hivyo kushindwa kupata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga kwenye shule za umma, jambo lililozusha mjadala mkubwa kuhusu hatima ya wanafunzi hao ambao, kimsingi bado ni watoto.
Mdau wa elimu nchini, Ndele Mwaselela amesema licha ya Serikali kufuta ada kwenye shule za umma, bado wazazi na jamii wana jukumu kubwa la kuendelea kushiriki kuhakikisha wanapata elimu bora.
Amesema hayo leo Jumamosi Desemba 30,2023 alipozungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kukabidhi misaada kwa familia zisizojiweza na zenye uhitaji.
Amesema kufutwa kwa ada hakutoi nafasi kwa mzazi kujiweka pembeni kuhusu elimu ya mtoto wake na hilo, limezifanya taasisi zilizo chini ya Shule za Paradise Mission ya mkoani Mbeya na Patrick Mission ya Dar es Salaam kujikita kusaidia familia za watoto wanaotoka kwenye familia duni na mazingira magumu.
“Serikali imefuta ada ni jambo jema na sasa imetimia miaka zaidi ya tisa, lakini bado kuna mambo ya msingi kwa mzazi kushirikiana na walimu na bodi za shule ili kuzalisha wanafunzi bora. Kuna michango zikiwemo sare kwa wanafunzi, lazima wazazi washiriki,” amesema.
Mwaselela aliungana na walimu na wafanyakazi wa shule hizo kutoa misaada kwa familia hizo kwa ajili ya sikukuu za mwishoni mwa mwaka kwenye maeneo mbalimbali jijini Mbeya.
Miongoni mwa misaada hiyo ni vyakula, vifaa vya shuleni kwa watoto vikiwemo vitabu, madaftari na kalamu.
Hata hivyo, kwa kutambua jukumu la kuendeleza watoto wa Mkoa wa Mbeya kupata elimu, Mwaselela ametangaza kuwasomesha bure wanafunzi 19 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kwenye shule za Paradise Mission na Patrick Mission kuanzia Januari mwakani.
Pia ametangaza kuwapatia sare za shule wanafunzi 300, huku wengine wakitoka kwenye familia zilizofikiwa na msaada walioanza kusambaza kuanzia Desemba 25, mwaka huu.
“Huu ni utaratibu ambao tumejijengea kila mwaka kwa walimu na wafanyakazi wa shule za Paradise na Patrick Mission kuifikia jamii,” amesema.
Akizungumza kuhusu wanafunzi waliofeli mtihani wa darasa la saba mwaka huu, ameshauri kuwekwa mkazo kwenye elimu ya mafunzo ya ufundi ili kuhakikisha wanabaki kwenye mfumo wa elimu.
Amesema idadi ya wanafunzi walioshindwa kufanya mtihani na waliofeli ni kubwa, hivyo Serikali na wadau wa elimu wanapaswa kulichukulia jambo hilo kwa uzito mkubwa.
“Wanafunzi 263,336 wamefeli mitihani kwa mwaka 2023 pekee, wengine zaidi ya 40,000 hawakufanya mtihani, sasa wako wapi na hawa waliofeli wanakwenda wapi? Kama nchi tulipaswa tuwe tumeitisha mjadala wa kitaifa kujadili hili na kupata njia sahihi za kufuata. Tukumbuke hawa si wanafunzi ni watoto wadogo. Wanafunzi wa darasa la saba kwa miaka ya sasa wengi ni chini ya miaka 14, sasa tunawaacha waende wapi hawa, ni lazima tuhakikishe wanabaki ndani ya mfumo wa elimu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule hizo, Edwin Peter amesema wanafunzi hao watapata fursa ya kusoma na kujengewa msingi imara ili kuja kuwa sehemu ya jamii inayokwenda kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali.
“Mbali na kuwapa watoto elimu, lakini tuna utaratibu wa kuwajenga kuwa sehemu bora ya jamii. Kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho kupitia elimu ambayo wataipata wakiwa hapa kwetu. Wamepata nafasi ya kuja kusoma kwenye shule zetu, hivyo tutawaelimisha na kuwapa mbinu za maisha wakitoka hapa wafike mbali zaidi,” amesema.