Wachuuzi wapandisha bei mgomo ukiendelea, wananchi walalama

Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa na mengine wazi jijini Mbeya kufuatia mgomo wa wafanyabiashara ulioanza jana.

Muktasari:

  • Wasema vifaa vya shule vimepanda bei maradufu, wataka Serikali kumaliza tofauti na wafanyabiashara.

Mbeya. Athari ya mgomo wa wafanyabiashara wa maduka jijini Mbeya imeanza kuonekana kwa wananchi kuabza kulalamikia bei ya bidhaa kupanda.

Inaelezwa vifaa na bidhaa zilizopanda bei ghafla ni vifaa vya shule ambavyo sasa wazazi wananunulia watoto wao kutokana na msimu za likizo kueleka kumalizika.

Shule mbalimbali na msingi na sekondaro zinatarajiwa kufunguliwa kuanzia Julai mosi, baada ya msimu wa llikizo kumalizika.

Mgomo huo kwa mkoani Mbeya ambao ulianza jana Jumanne Juni 25, 2024, umeendelea kwa maduka yote jijini humo kufungwa. Wafanyabiashara hao wamegoma kuishinikiza Serikali kuondoa tozo na kodi mbalimbali wanazodai kuwa si rafiki kwao.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Juni 26, 2024, baadhi ya wananchi wamesema hali imeanza kuwa mbaya, kwani hakuna huduma na hata wale wachache waliofungua maduka maeneo ya pembezoni na machinga wamepandisha bei za bidhaa zao.

Ezra Mdamu, mkazi wa jijini hapa amesema wafanyabiashara wadogo wanatumia fursa hiyo kujinufaisha kwa kuongeza bei ya bidhaa.

Amesema mfano bei ya daftari ambalo kabla ya mgomo lilikuwa likiuzwa Sh500, leo linauzwa Sh700 huku soksi zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh1,000 sasa zinauzwa Sh2,000.

"Naomba Serikali wakae na wafanyabiashara hawa wamalize tofauti zao, kwa sababu wanaoumia ni sisi wananchi wa kipato cha chini," amesema Ezra.

Kauli ya Ezra imeungwa mkono na Elizabeth John, aliyesema licha ya bei ya bidhaa kupanda, pia hazipatikani kwa kuwa zimefungiwa na wenye maduka makubwa ya jumla.

Amesema Serikali iharakishe kumaliza mazungumza na wafanyabiashara hao, ili hali irejee kama kawaida.

"Kwanza maisha ni magumu, mzunguko wa hela ni mdogo, Serikali iwaite wafanyabiashara isikilize kilio chao na kumaliza tatizo hili," amesema Elizabeth.

Naye Wilbroad Daud, mkazi wa mtaa wa Makunguru jijini humo, amesema wamekutana na adha ya kukosa mahitaji hasa kwa wanafunzi wanaojiandaa kufungua shule Julai mosi, licha ya viongozi wa Serikali kuona kinachoendelea.

"Leo nimefika sioni huduma yoyote, watoto wanapaswa kwenda shule Julai mosi, maduka yamefungwa na viongozi wanaona, ila hawajasema chochote, hatujui mgomo huu hadi lini ili kupata huduma," amesema Daud.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara soko la Mwanjelwa, Aisea Mwandondwa amesema kwa sasa msimamo wao ni kuendelea kufunga maduka hadi ufumbuzi utakapopatikana.

"Tunajua kuna vikao vinaendelea kule Dodoma, lakini msimamo wa wafanyabiashara ni kuendelea kufunga maduka hadi tamko la viongozi wa juu baada ya vikao na Serikali," amesema Mwandondwa.