Prime
Kesi kupinga wachezaji Singida Black Stars kupewa uraia yatupwa

Muktasari:
- Wakili Madeleka amesema anajipanga kurekebisha dosari ili kuirudisha kesi mahakamani.
Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania imeitupa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Wakili Peter Madeleka kupinga uamuzi wa Serikali kuwapa nyota watatu wa timu ya Singida Black Stars (SBS) uraia wa Tanzania.
Uamuzi wa kuitupa kesi hiyo umetolewa na Jaji Evaristo Longopa wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu ya Dodoma, baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowekwa na wajibu maombi, wakiwamo nyota wawili wa timu hiyo.
Alipotafutwa na gazeti hili baada ya shauri hilo kutupwa na mahakama, Madeleka amesema: “Nimepokea uamuzi wa Mahakama. Kwa vile imeondolewa katika hatua ya pingamizi, inatoa fursa ya kujipanga, kurekebisha dosari na kuirudisha.”
Madeleka aliyewakilishwa kortini na Wakili John Seka, alifungua kesi hiyo pamoja na mambo mengine akiiomba mahakama itamke kuwa uamuzi wa kuwapa uraia nyota hao watatu wa SBS ulikiuka Katiba ya Tanzania.
Katika uamuzi alioutoa Aprili 9, 2025 na nakala yake kupatikana katika tovuti ya Mahakama leo Aprili 11, 2025, Jaji Longopa amesema pingamizi za awali zilizotolewa na wahojiwa zina mashiko na zinastahili kuzingatiwa.
“Katika mazingira, ombi mbele ya mahakama hii halifai kwa sababu ya kasoro iliyoonekana kulingana na uchambuzi. Kwa sababu hiyo, ni fursa kwa Mahakama kutupilia mbali ombi hilo kwa kuwa na dosari isiyotibika,” amesema Jaji.
Shauri hilo la kikatiba lilikuwa dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani kama mdaiwa wa kwanza, Kamishina Jenerali wa Uhamiaji (CGI), mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akiunganishwa kama mdaiwa wa tatu.
Pia nyota hao watatu wa SBS – Emmanuel Keyekeh, raia wa Ghana; Josephat Bada (Ivory Coast) na Muhamed Camara (Guinea), waliunganishwa kama wajibu maombi wa 4, 5 na 6 mtawalia.
Wengine walioshtakiwa ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji nchini ambao walikuwa wadaiwa wa saba na nane mtawalia.
Maombi yalivyokuwa
Wakili Madeleka alikuwa anaiomba Mahakama itamke kinga aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani kupitia kifungu cha 23 cha Sheria ya Uraia, haiendi mbali na kufikia hatua ya kukiuka Katiba na kifungu cha 9 cha sheria ya uraia.
Aliiomba Mahakama itamke kuwa kwa kupendekeza wachezaji hao wapewe uraia, CGI na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji walikiuka Katiba ya nchi na sheria ya uraia.
Pia aliomba Mahakama itamke kwamba kwa kuwapa uraia wachezaji hao, Waziri wa Mambo ya Ndani alikiuka ibara ya 26(2) ya Katiba ya nchi na kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Uraia Tanzania.
Madeleka vilevile aliomba Mahakama itamke kuwa wachezaji hao hawana sifa ya kupewa uraia na kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI na wachezaji hao kwa pamoja walishiriki kughushi au kutoa uraia katika mazingira yasiyokubalika.
Aliomba Mahakama itoe amri kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na CGI kutaifisha mara moja vyeti vya uraia walivyopewa wachezaji hao, na kuwaamuru kusalimisha vyeti hivyo kwa Msajili wa Mahakama wakati hukumu ikisubiriwa.
Madeleka aliomba Mahakama imwamuru AG kama mshauri mkuu wa Serikali, kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha ‘kumulikwa’ kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI na Mkurugenzi wa Uhamiaji na walio chini yao.
Aliiomba Mahakama imwagize DPP kuanzisha uchunguzi kuhusu vitendo na ushiriki wa Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI, wachezaji hao na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji kuona kama jinai yoyote ilitendeka na kuchukua hatua.
Hakuishia hapo, aliiomba Mahakama itoe amri kwa waziri, CGI na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji kulipa Sh500 milioni kama fidia ya adhabu kwa matendo yao ambayo hayakuzingatia Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Kama haitoshi, aliiomba Mahakama iwaamuru wachezaji hao kulipa Sh200 milioni kama fidia ya adhabu ya kufanya matendo yanayokiuka Katiba. Pia wadaiwa walipe gharama za kesi na mahakama itoe amri yoyote inayoona inafaa.
Kigingi kortini
Katika majibu ya maandishi, wadaiwa Josephat Bada na Muhamed Camara, waliwasilisha pingamizi la awali wakidai kesi dhidi yao ina dosari kwa vile mdai hakueleza yeye binafsi ameathirika vipi.
Katika hoja ya pili ya pingamizi walieleza kesi hiyo ni mbaya kwa kuwa inakiuka baadhi ya vifungu vya sheria na hoja ya tatu walidai shauri lina kasoro kwa kumuunganisha mdaiwa wa nane ambaye haishi kisheria.
Ukiacha hilo, wadaiwa wa kwanza, pili, tatu, na saba nao waliwasilisha pingamizi lao lenye hoja nne. Moja ni kuwa mdai hakuonyesha ni kwa vipi ukiukwaji wa Ibara ya 12 na 29 ya Katiba ya Tanzania imemuathiri binafsi.
Hoja ya pili walidai kesi hiyo ni mbaya kisheria kwa kuwa inakiuka vifungu vya 4(5) na 8(2) vya haki za msingi na wajibu cha sheria hiyo ya mwaka 2019, kwa mdai kutomaliza nafuu nyingine kabla ya kukimbilia mahakamani.
Pia walidai mahakama hiyo ilikuwa haina mamlaka ya kushughulikia amri zinazoombwa na mdai na shauri hilo ni baya kisheria kwa kuwa linamwingiza mdaiwa ambaye kisheria haishi.
Kwa niaba ya wadaiwa hao, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Edwin Webiro alidai mdaiwa wa nane, Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji haishi kisheria baada ya marekebisho ya sheria ya uraia ya mwaka 2015.
Wakili Anatory Nyaki aliyewawakilisha wadaiwa wa tano na sita, hoja zake zilifanana kwa kiasi kikubwa na za Webiro.
Licha ya Seka kujaribu pangua hoja hizo, Mahakama haikukubaliana naye.
Uamuzi wa Mahakama
Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, Jaji Longopa amesema Mahakama inakubaliana na hoja za mawakili wa wadaiwa wa kwanza, pili, tatu na saba kuwa vifungu vya Katiba vinatekelezwa kwa matakwa ya taratibu kulingana na sheria ya Bunge.
“Kwa hakika, ili kutekeleza ibara ya 12 na 29 ya Katiba ya Tanzania, mleta shauri la kikatiba alipaswa kutimiza vifungu vya Sheria ya Haki na Wajibu (Bradea) na Kanuni zake na akatoa mifano ya kesi zilizoweka msimamo wa sheria.
Jaji amesema kwa kutazama kiapo cha Madeleka, inaonyesha mleta shauri ni mwanaharakati wa haki za binadamu, shabiki wa soka na hakuonyesha alivyoathirika.
“Kama hayo ndiyo maudhui ya jumla ya kiapo kilichopokewa, ni wazi mleta shauri hajaweza kwa umakini kueleza namna ukiukwaji huo wa ibara ya 12 na 29 ya Katiba imemuathiri yeye binafsi. Alipaswa aeleze ameathirika vipi,” amesema Jaji.
“Kwa maoni yangu, hakuna maelezo ya kutosha kukidhi vigezo katika kifungu cha 4(2) cha sheria ya Bradea yanayoonyesha ukiukwaji wa ibara ya 12 hadi 29 ya Katiba umemuathiri binafsi mleta shauri,” amesema.
Kuhusu hoja ya kumshtaki mdaiwa asiyehusika, Jaji amesema wadaawa (parties) wanakubaliana kuwa mjibu shauri wa nane, Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji, haishi tena baada ya marekebisho ya sheria ya uraia ya Tanzania.
“Shauri la kikatiba ni moja ya mashauri ambayo mwenendo wake ni muhimu kwa vile linahitaji kushughulikia masuala makini. Kama ndivyo, mtu anapofungua shauri la kikatiba ni lazima apime uzito dhidi ya wajibu shauri ambao ni sahihi,” amesema.
Jaji amesema ni suala lililopo katika kumbukumbu za Mahakama kuwa Wakili Madeleka hapingi kifungu chochote cha sheria ya uraia, kwamba ni kinyume cha Katiba, bali ni namna ilivyotumiwa kuwapa uraia wachezaji hao nyota.
“Malalamiko mbele ya Mahakama ni madai ya kukiukwa kwa kifungu cha 9(1) cha sheria ya uraia ambacho kinadaiwa kilisababisha kukiukwa kwa Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Tanzania.
“Katika mazingira hayo na kwa kuongozwa na msimamo (precidents) wa Mahakama ya Rufaa ni kwamba ukiukwaji huo unaweza kushughulikiwa kwa njia ya mapitio ya Mahakama badala ya shauri la Katiba kama lililofunguliwa,” amesema.
Katika mazingira hao, amesema ombi mbele ya Mahakama halifai kwa sababu ya kasoro iliyoonekana, na kwa sababu hiyo, Mahakama inaitupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa na dosari zilizoonekana haziwezi kutibika.