Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Lusinde alia wanaoomba ajira kufanyishwa mitihani, atoa pendekezo

Muktasari:

  • Mbunge wa Mvumi (CCM) Livingtone Lusinde amelia na mfumo wa ajilra kuwakuwakusanya mahali pamoja na kuwapa mtihani wa muda mfupi.

Dodoma. Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde amekosoa utaratibu wa waajiriwa wapya kufanyiwa mtihani kabla ya kuajiriwa na badala yake ametaka vitumike vyeti.

Lusinde ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 14, 2025 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/26.

Makadirio hayo yaliwasilishwa Aprili 9, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiomba Bunge limuidhinishie Sh782.08 bilioni.

Akichangia mjadala huo, Lusinde amesema kama Serikali inaona hawawezi kuajiri Watanzania wote kwa kutumia ajira kupitia mfumo wa ajira wa portal, basi zigawanywe katika kila halmashauri.

Amesema endapo halmashauri hawatapata watu wenye elimu inayohitajika basi watazirudisha katika mikoa mingine ili waweze kuajiriwa.

“Huu utaratibu wa kuwaleta pamoja, hivi vyeti mlivyowapa mnavikagua unasema hiki ni cheti chako original (halisi) kabisa halafu baadaye unamuingiza katika mtihani wa dakika moja ndio umkoseshe mtoto ajira, haiwezekani,” amesema.

Mbunge alia na wanaoomba ajira kufanyiwa mtihani

Lusinde amesema:“Haiwezekani tunawastress (tunawapa msongo) watoto wetu, cheti cha ualimu mtu anasoma zaidi ya miaka mitatu, yaani wewe unakuja kumpa mtihani wa dakika mbili unafuta yote haya masomo yote aliyosoma miaka mitatu yanaonekana haina maana kwa sababu ya mtihani wa dakika mbili, hapana.”

Ametaka kama uwezo wa Serikali ni kuajiri watu 15,000 basi iseme na kuzigawa ajira katika halmashauri bila kuwasumbua watu kwa kuwajaza jijini Dodoma.

“Wanakuja wanalala nje, watoto wa watu wanakuja na nauli za kukopa, wakija hapa wanaishi maisha ya taabu sana mheshimiwa mwenyekiti, hii si sawa badala ya kuondoa kero tunazalisha kero,” amesema.

Lusinde amehoji kama Serikali ikisema ina uwezo wa kuajiri watu 15,000 kwa nini wasiwaambie watu walete vyeti na kuvikagua na kisha kuwaajiri.

“Leo unakuja kunipa mtihani wa dakika moja, halafu unaniondolea sifa yote, halafu huyohuyo aliyekosa mwaka huu mwakani anafaulu, hii inakuwa si sawa ni lazima tuwatendee haki sawa wananchi wetu,” amesema.

Machi 3, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alipohutubia ufunguzi wa kikao kazi na wakuu wa taasisi za umma, kinachofanyika jijini Dodoma aligusia suala la usaili huo.

Simbachawene alisimulia kilichobainika katika usaili wa walimu, akisema yupo mmoja asiye na taaluma hiyo aliyepenya hadi akaingia kusailiwa.

“Kwenye usaili watu wengine ni wachawi sijui wanapenyaje, yaani mnachuja mtakavyochuja, unajua kuna majamaa yanaingia kwenye usaili wa walimu wakati sio mwalimu, hajawahi kusomea ualimu kabisa.

“Umeweka mtihani anafaulu sasa ukishakuja kwenye usaili wa mdomo ndio anaulizwa hivi ukiwa na darasa unafanyaje yule jamaa anapata nne, wakati huku kwenye kuandika amepata 99,” alisema.

Alisema upo uwezekano wa kuwepo walimu wasio na taaluma kutokana na uzoefu wa kilichojitokeza.