Wachimbaji wadogo waonywa tabia ya kupuuza matumizi sahihi ya zebaki

Wachimbaji wadogo wa Mgusu, wakipanga vifaa vya usalama kazini vilivyotolewa na taasisi ya uchimbaji mdogo Tanzania (FADEV) lengo likiwa kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa usalama na kujikinga na matumizi yasiyo salama ya kemikali ya Zebaki.
Muktasari:
- Wachimbaji wadogo wanakadiriwa kutumia takribani tani 24 za zebaki kwa mwaka, mikoa inayoongoza kwa matumizi ni Geita, Mbeya, Shinyanga na Mara.
Geita. Wakati Serikali ikisubiriwa kuja na njia mbadala na rahisi ya kuchenjua madini ya dhahabu, wachimbaji wadogo wametakiwa kuzingatia uvaaji wa vifaakinga ili kuondokana na madhara yatokanayo na kemikali hiyo inayoathiri afya na mazingira.
Uchenjuaji wa dhahabu hutumia asilimia 80 ya zebaki yote inayotumika nchini na kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa Minamata matumizi ya kemikali hiyo yanapaswa kusitishwa ifikapo mwaka 2030.
Kemikali hiyo inaelezwa kuharibu ubongo na mfumo wa mishipa ya fahamu, figo, watoto kuzaliwa na ulemavu, kupoteza kumbukumbu, kushindwa kupumua na kuathiri moyo, mapafu na mimba kuharibika
Akizungumza Juni 6, 2024 wakati wa utoaji mafunzo ya kuhamasisha uchimbaji bora unaozingatia usalama, afya na mazingira, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchimbaji Mdogo Tanzania (Fadev), Theonistina Mwasha amesema bado wachimbaji wadogo hawazingatii matumizi sahihi ya zebaki.
“Tunawapa mafunzo mbalimbali ya uchimbaji bora unaozingatia usalama afya na utunzaji wa mazingira hasa matumizi mazuri ya zebaki lakini bado hawaendani na kanuni na sheria zinavyotaka wafanye kwa ajili ya kutunza afya zao na wale wanaowazunguka maana madhara ya zebaki yanawaathiri zaidi hawa wanaoitumia,” amesema.
Amesema pamoja na wachimbaji wadogo kufundishwa madhara yatokanayo na zebaki bado wanaichukulia kiholela na hawazingatii madhara yaliyopo kutokana na imani potofu walizonazo, ikiwemo kutovaa glovu wakati wa kukamatisha dhahabu kwa madai kuwa itapotea.
Mwasha amesema pamoja na Mkataba wa Minamata kutaka zebaki isitishwe ifikapo 2030 huenda azma hiyo isitimie kutokana na njia mbada ambayo ni bei nafuu na rahisi kutumia bado haijapatikana kwa wachimbaji wadogo na kipindi kilichobaki ni kifupi.
“Miaka sita imebaki kusitisha matumizi ya zebaki lakini huenda kemikali hii ikaendelea kutumika kwa kuwa mambo ya kufanya bado ni mengi na wachimbaji wadogo wengi hawajafikiwa, amesema.
Amesema Serikali inapaswa kuongeza kasi kutekeleza mambo yaliyopo kwenye mpango kazi wa 2020-25 na endapo zebaki itasitiswa 2030 kama Mkataba wa Minamata unavyotaka ipo hatari wachimbaji wadogo wengi wakabaki bila kazi.
Taasisi hiyo pia imetoa vifaa vya usalama kazini vyenye thamani ya Sh22.2 milioni kwa wachimbaji wa katika mgodi wa Mgusu na migodi mingine iliyopo Nyarugusu wilayani Geita.
Wakizungumza wakati wa mafunzo hayo baadhi ya wachimbaji wadogo wamesema yamewasaidia kujua madhara ya zebaki na kujua namna gani ya kujikinga wawapo kazini ili kupunguza au kujikinga na madhara ya zebaki.
“Wachimbaji wadogo hawatumii vifaakinga kwa sababu ya kutoamini kama kweli zebaki ina madhara lakini mafunzo tuliyopata ya kuonyesha jinsi wenzetu huko nje waliathirika hii imetufanya tuamini zebaki ni mbaya na labda sisi sote tumeshaathirika na kazi yetu, sasa ni kusaidia kizazi chetu kisiendelee kuathirika,” amesema Daudi Mesi.
Mesi ameiomba Serikali kutenga fedha kutokana na mapato yanayotokana na uchimbaji mdogo kwa ajili ya elimu kwa wachimbaji ya namna bora ya kutumia zebaki kwa usalama na kuwatafutia kemikali mbadala itakayowasaidia kuondokana na matumnizi ya zebaki ambayo ni hatari kwa afya na mazingira.
Josephina Michael, mkazi wa Mgusu amesema kwa kiasi kikubwa kina mama wameathirika na zebaki kutokana na wao kufanya kazi kwenye mazingira yenye kemikali hiyo pasipo kuzingatia usalama, ikiwa ni pamoja na kuishika kwa mkono huku wakinyonyesha watoto au kula.
“Kwa wachimbaji wadogo uathirikaji ni mkubwa maana unakuta mama ananyonyesha akiwa machimboni, bado mwingine anaweza kuiba na kuficha kwenye kifua lakini hata vijana wakiwa huku hawavai vifaakinga, ni sawa na wote tumeshaathirika lakini tusaidiwe kizazi chetu kisipate madhara,” amesema Michael.
Kwa wa mujibu wa mpangokazi wa Taifa wa kupunguza matumizj ya zebaki wa 2020-2025, uchenjuaji dhahabu hutumia takribani asilimia 80 ya zebaki yote inayotumika nchini, wachimbaji wadogo wakikadiriwa kutumia takribani tani 24 za zebaki kwa mwaka na mikoa inayoongoza kwa matumizi ni Geita, Mbeya, Shinyanga na Mara.
Sekta ya uchimbaji mdogo inatoa ajira ya moja kwa moja kwa takribani watu 1.2 milioni na ajira zisizo za moja kwa moja kwa watu 7.2 milioni na ni sekta inachangia asilimia 90 ya nguvukazi katika sekta ya madini nchini.