Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DC ataka wahalifu migodini watajwe kwa siri

Mkuu wa Wilaya ya  Chunya, Salmon Mayeka  akizungumza na wadau wa sekta ya madini na wachimbaji wadogo wilayani humo katika kikao kilichoratibiwa Ofisi ya Tume ya Madini cha kusikiliza kero zao. Picha na Hasa Mathias

Muktasari:

  • Baada ya kuzuka kwa wimbi la uhalifu kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wilayani Chunya, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mayeka S. Mayeka amewataka wachimbaji hao kutoa taarifa za siri dhidi ya wahalifu hao.Baada ya kuzuka kwa wimbi la uhalifu kwenye migodi ya wachimbaji wadogo wilayani Chunya, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mayeka S. Mayeka amewataka wachimbaji hao kutoa taarifa za siri dhidi ya wahalifu hao.

Chunya. Katika kuondoa matukio ya uhalifu kwa wachimbaji madini wadogo wa madini, Serikali wilayani hapa, imetaka waathirika wa matukio hayo watoe taarifa za siri ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa watakaobainika.

Hayo yamesemwa leo Alhamis Novemba 30, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka S Mayeka mara baada ya kupata malalamiko ya uwepo wa vitendo vya uhalifu katika maeneo ya wachimbaji hao.

Aliyewasilisha malalamiko juu ya uhalifu huo ni Haruna Salehe, mmoja wa wachimbaji wadogo kutoka Kata ya Makongorosi.

Salehe alimwambia DC Mayeka kuwa kumeibuka matukio kadhaa ya uhalifu na hivyo kuomba uwepo wa askari wa akiba na kwamba wachimbaji hao wako tayari kuchangia gharama za kujikimu kwa walinzi hao.

Salehe amewasilisha malalamiko hayo kwenye kikao cha wadau wa sekta ya madini kilichoitishwa na Tume ya Madini wilayani hapa, kikihusisha wachimbaji wadogo 200 kutoka kata mbalimbali sambamba na watendaji wa Serikali.

“Mkuu wa Wilaya tumeleta ombi hilo mbele yako, tunajua liko ndani ya uwezo wako, tunahitaji askari wa jeshi la akiba (mgambo,) au wa Suma JKT, sisi kama wachimbaji tuko tayari kulipia gharama serikalini, lengo ni tuwe sehemu salama kuendesha shughuli zetu,” amesema.

Amesema wanatambua uwepo wa changamoto ya idadi ndogo ya askari wa Jeshi la Polisi, hivyo ni vyema akasikia ombi lao, na kwamba uwepo wa askari huyo utasaidia kupunguza matukio hayo na utoroshaji wa madini uliokithiri.

“Wanaotorosha madini wanafanya hivyo kutokana na utitili wa tozo, na kwa kuwa hatuna ulinzi katika maeneo ya machimbo, ni rahisi wahalifu kufanya hivyo, Serikali ikae na kuliangalia hilo ili kudhibiti madini yetu yasiuzwe nje ya masoko rasmi,” amesema.

Kufuatia kauli hiyo DC Mayeka amesema kuwa asilimia kubwa watu wanaojihusha na uhalifu wanatoka katika maeneo husika kwa kula njama na kufanikisha matukio hayo.

“Nionye hao watu wachache, ambao wanachora ramani pindi wanapobaini mchimbaji ameingiza kaboni au kapata madini, na hivyo wanakula njama na kufanya uhalifu, waache mara moja... Serikali haitawavumilia...nanyi wachimbaji toeni taarifa za siri,” amesema Mayeka.

Kaboni ni kemikali inayotumika katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu, ambayo haileti athari kwa afya ya binadamu na mazingira yake, kama kwa zebaki.

Kwa upande mwingine Mayeka amesema yupo kutetea haki ya wanyonge na hayuko tayari kuona haki ya mtu yeyote inapotea.

Kuhusu suala la ombi mgambo, Mayeka amesema amesikia ombi la wachimbaji ataangalia kwa kuwa hilo liko ndani ya uwezo wake na atazungumza na uongozi wa Suma JKT.

“Nimesikia ombi lako bwana Salehe kwa upande wa Suma JKT nitazungumza nao ili kuona ni namna gani utaratibu wao kama kunakuwa na mahitaji ya askari, ila niwahakikishie ombi lenu nimelibariki,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Aidha, Mayeka amekemea tabia utoroshaji wa madini inayofanywa na baadhi ya wachimbaji na kwamba jambo hilo limetia doa wilaya hiyo.

Wakati huohuo, Mayeka amesema Serikali itafunga mashimo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ambayo hayatafanyiwa marekebisho wakati huu wa mvua ili kuepusha vifo vya kizembe.

“Nimetoa tahadhari na tuna taarifa kuna mashimo yako kwenye hatari kubwa, sasa sitavumilia kusikia kuna watu au mtu kapoteza maisha kwa kuangukiwa na kifusi au kukosa hewa; lazima wamiliki wachukue hatua,” amesema.

Ofisa Madini Mkazi wa Wilaya ya  Chunya, Laurent Mayala amesema lengo la kikao hicho ni kutekeleza agizo la Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alililolitoa hivi karibuni alipofanya ziara wilayani humo.

“Waziri alitoa maelekezo ya kukutana na wachimbaji kwa lengo la kutoa elimu, ya ukamilishaji wa maombi ya leseni za uchimbaji wa madini kwa kuwa asilimia kubwa hawana vibali halali,” amesema.

Amesema lengo la Serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizowekwa, ikiwepo kupata vibali na leseni halali zauchimbaji.

Akizungumza katika mkutano huo, Pili Chitemi ameomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha wanawake wanaojihusha na shughuli hizo kupata mikopo na leseni za uchimbaji madini ili kuwasaidia kuongeza tija na kuchangia mapato ya Serikali.