Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge watwishwa zigo la bajeti kuu

Muktasari:

  • Juni 12, 2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba huku akiomba Bunge kumuidhinishia Sh56.49 trilioni

Dodoma. Wakati wabunge kesho Jumatatu, Juni 16, 2025 wakianza kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2025/26, Watanzania wameshauri wajielekeze kuibua vyanzo vipya vya mapato ambavyo havitawaumiza.

Bajeti kuu ya Serikali iliwasilishwa bungeni jijini Dodoma Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba huku akiomba Bunge kumuidhinishia Sh56.49 trilioni.

Ni bajeti yenye sura mbili kwa kuwa, wapo ambao huenda wakapata nafuu kupitia bajeti hiyo baada ya kuwa na mapendekezo ya kuondolewa kwa kodi na tozo na kupendekezwa kuwekwa kodi na tozo.


Wabunge wataanza kuijadili bajeti hiyo kwa siku saba kuanzia kesho Jumatatu hadi Juni 24, 2025 watakapohitimisha na kupiga kura.

Mwananchi imezungumza na wadau wa bajeti hiyo na kushauri maeneo mbalimbali ambayo wawakilishi hao wa wananchi wanapaswa kuyatolea macho.

Wameshauri wabunge kujielekeza katika kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kutotegemea wahisani katika miradi ya maendeleo.

Mchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka amesema wabunge wamepata muda wa kutosha kusoma makadirio hayo ingawa kuna maeneo mengine yanataka takwimu na tathimini.

Amesema wabunge wanaweza kuangalia maeneo ya mkakati ambayo sehemu kubwa yanaweza kuwa na msaada kwa wananchi ikiwamo katika huduma za kijamii zinazowagusa.

“Wakati mwingine fedha ni ndogo lakini mahitaji ni mengi, kuangalia mgawanyo wa fedha uweze kwenda katika maeneo ambayo ni kipaumbele kwa wananchi wahitaji,” amesema Dk Mwinuka.

Mhadhiri huyo amesema ni vyema wakaibua maeneo mengi yanayoweza kuibua vyanzo vipya vya mapato bila kuleta makali kwenye uchumi.

“Kunapaswa kuwa na ubunifu, inawezekana Serikali imefikiria, wizara imefikiria lakini na wao bado wanafursa ya kushauri maeneo mapya yenye ubunifu yanayoweza kusaidia, nchi inaweza kupata mapato ya ziada na kupunguza utegemezi kwa fedha zisizo za uhakika za kutoka nje,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Kusundwa Wamalwa amesema bajeti nyingi zinavyotengwa hutengwa kwa maneno na kusababisha kutokwenda kiasi chote kama kilichopitishwa.

Wamalwa amesema wafugaji wana changamoto za kudumu nchini ikiwamo kutokuwa na maeneo rasmi ya ufugaji ambayo yamepimwa na kutungiwa sheria kisha kurasimishwa kwa kundi hilo kama ilivyo kwa hifadhi.

“Kutokuwa na miundombinu nayo ni shida ambayo imekuwa ikitukumba, majosho ya kunyweshea mifugo, hayatengewi fedha ili kuweza kushughulikia changamoto hiyo,” amesema.

Wamalwa amesema changamoto hiyo imekuwa ikipanuka mwaka hadi mwaka kutokana na kuongezeka kwa wafugaji na kupungua kwa maeneo ya malisho ya mifugo.

Amesema kupima vijiji vya wafugaji na kutoa maeneo maalumu kwa wafugaji, kutakomesha tabia ya kuhamahama kwa kundi hilo na kupunguza idadi ya mifugo.

“Niombe sana wabunge wakati wanajadili bajeti hii wajielekeze katika kutenga fedha za kutosha kupima maeneo ya ufugaji, malisho, kutengeneza majosho na visima vya maji kwenye maeneo ya wafugaji,” amesema Wamalwa.

Aidha, Wamalwa amewashauri wabunge kuangalia suala la wazee kuzingatiwa katika bajeti hiyo kwa kuhakikisha wanapata huduma za uhakika za afya kwa sababu eneo hili bado lina changamoto kubwa.

Ameshauri wabunge kushawishi Serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya matibabu ya wazee ili waweze kupata huduma bora na za haraka.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Tanzania, Said Kagomba amewaomba wabunge kupitisha kipengele cha kupunguza gharama za leseni kutoka Sh70,000 hadi Sh30,000 kama ilivyopendekezwa na Waziri Mwigulu.

“Lakini waangalie pikipiki ziweze kushuka bei zake kila siku zinapanda. Sisi tunapatiwa pikipiki na hawa ndugu zetu wageni, sasa hili ni soko huria. Hata kulinda masoko basi sio hivyo Watanzania tunaumia,” amesema Kagomba.

Amesema bei ya pikipiki imekuwa ikipanda kila baada ya miezi sita nchini na sasa imefikia kati ya Sh3.2 milioni na Sh3.6 milioni huku zinazotumia umeme zikifika Sh6 milioni.

Kagomba  ameshauri wabunge wajadili jinsi ya kuvutia wawekezaji wa viwanda vya pikipiki na bajaji nchini ili kuwezesha kupungua kwa bei.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema wabunge wajielekeze kuangalia vyanzo vya bajeti vikoje kwa kuongeza vyanzo vya ndani zaidi katika kuchangia bajeti zetu.

"Kuangalia pia namna ambavyo tunaweza kubana matumizi ya Serikali kwa ajili ya kuhakikisha fedha nyingi zinakwenda katika maendeleo na si shughuli za kawaida,” amesema Ole Ngurumwa.

Amesema katika bajeti hiyo karibu asilimia zaidi ya 80 zinakwenda katika mitumizi ya kuiwezesha Serikali jambo ambalo linafaa kutazamwa upya.

“Kuangalia namna gani tunaweza kupunguza fedha za nje, na wananchi wanataka kupata taarifa kamili kutokana na deni la nje, nini kilikopwa na kwa ajili gani na wabunge wasikie wananchi wanachosema ili wakijadili bungeni,"amesema

Ole Ngurumwa amesema waangalie sheria za kodi ambazo zinapendekezwa zisije zikaleta shida katika mchakato wa kodi kwa kuwa lengo la Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ni kuhakikisha mazingira ya kodi yanakuwa rafiki kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Machinga mkoani Dodoma, Christian Msumari amesema wabunge waangalie namna bajeti inavyoweza kuinua kundi la wafanyabiashara wadogo ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.

Amesema kwa kufanya hivyo, kutafanya vijana wengi kuvutiwa na ufanyaji wa biashara ndogo kwa sababu itakuwa ni rahisi kupata mitaji na maeneo yatakuwa ni rafiki kwa ufanyaji biashara.