Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wabunge waja na mpango mikopo elimu ya juu

Wabunge wakiwapongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na Naibu wake, Wanu Hafidh Ameir baada ya kupitisha bajeti ya Wizara hiyo leo Mei 8, 2026 bungeni Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Ni baada ya kuwepo malalamiko ya kukosa mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu ama kutokana na vigezo au kushindwa kujaza fomu kwa usahihi kwenye mfumo.

Dodoma. Suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu limeendelea kugonga vichwa vya watu, lakini wabunge wamekuja na pendekezo la nini kifanyike.

Hali hiyo inakuja huku kukiwa na malalamiko ya kukosa mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu ama kutokana na vigezo au kushindwa kujaza fomu kwa usahihi kwenye mfumo.

Wakichangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia, wabunge wamependekeza mambo matatu ili kutoa nafasi ya idadi kubwa ya wananfunzi kufikia na mikopo ya elimu ya juu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Asha Feruzi amependekeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Kuibadilisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuwa Mfuko wa elimu kwa lengo la kutanua wigo wa upatikanaji wa mapato.

Feruzi anasema kitendo cha Bodi ya Mikopo kuendelea kusubiri chanzo kimoja cha mapato kinafanya watoto wa wakulima na masikini kukosa mikopo na hivyo mpango huo ni kama unaweka matabaka.

Hata hivyo, mbunge huyo amelalamikia alichokiita zuio la wanafunzi la kutokufanya mitihani kwa sababu za kutolipa ada kwamba linawaumiza wanafunzi wa masikini badala yake akaomba waruhusiwe kufanya mitihani lakini mwishoni wataona namna ya kulipa ada.

“Lakini, nashauri Serikali kudhibiti wanafunzi kuzuiliwa kufanya mitihani ya mwisho kwa kukosa ada, kitendo hicho kinawaumiza watoto wa masikini na kingine Serikali angalieni upya kozi zinazotolewa vyuoni wakati hazipo kwenye kada za ajira nalo ni janga,” amesema Feruzi.

Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Paschal Chinyele yeye amezungumzia uanzishwaji wa mfuko wa elimu lakini akapendekeza kuwepo na utaratibu wa kuuchangia mfuko huo kupitia tozo za simu.

Chinyele anasema Serikali ikiweka utaratibu mzuri inaweza kukusanya fedha na mapato ya kutosha ambayo yatasaidia kuwafikia idadi kubwa ya wanafunzi wenye uhitaji.

Mbunge huyo amesema, mpango wa kukusanya fedha za elimu kupitia simu unaweza kuwa na tija zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo watoto wengi wanakosa kupata elimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo umasikini.

“Tusifikiri yule mtoto mmoja ambaye vyombo vya habari vilimfikia, kuna watoto wengi wa masikini ambao vyombo vya habari haviwafikii, huko ni matatizo matupu ndugu zangu, bila kuliangalia hili hali itazidi kuwa ngumu,” amesema Chinyele.

Mbunge huyo amesema kuanzishwa kwa mfuko huo kutakwenda sambamba na maandalizi ya siku za usoni hasa wanafunzi wanaokwenda kuanza kidato cha kwanza kwa mkupuo 2028 kwamba hadi watakapomaliza elimu ya sekondari wangekuta zipo fedha za kutosha.

Mbunge mwingine aliyechangia kuwepo kwa mfuko wa elimu alikuwa ni Ester Bulaya (Bunda) ambaye alisema kwa sasa uwezo wa utoaji wa mikopo kwa kutumia Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu hauwezi kuendana na ongezeko la mahitaji kwa idadi ya wanafunzi.

Kwa upande wake Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege yeye alizungumzia ulazima wa mpango wa chakula shuleni kwamba Serikali ije na agizo la mfanano kwa nchi nzima kuliko ilivyo sasa ambapo wanafunzi kwa mikoa wanarudi kula majumbani kisha wanakwenda mchana shuleni.

Chege alisema mpango wa chakula unasaidia kuboresha uwezo wa wanafunzi kujifunza na kuelewa masomo darasani, lakini akataja changamoto ya chakula shuleni bado ni kubwa licha ya kuwepo kwa utaratibu wa wazazi kuchangia katika baadhi ya maeneo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Katavi, Taska Mbogo, amependekeza matumizi ya Kiswahili na Kiingereza yaende sambamba katika ufundishaji kwa elimu ya msingi nchini ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi na kuwajengea uwezo wa kushindana kimataifa.

Hata hivyo, Mbogo ameendeleza msimamo wake alioutoa Bungeni Aprili 18,2024 ambapo alionyesha kupinga uanzishwaji wa shule za mchepuo wa Kingereza badala yake akaomba walimu wanaofundisha masomo hayo watawanywe kwenda shule zote ili somo hilo lifundishwe kwa wote.

Mbunge wa Viti Maalumu wa kundi la wenye ulemavu, Stella Ikupa, ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuingiza somo la lugha ya alama katika mfumo wa elimu kwa kila Mtanzania ili kurahisisha mawasiliano na watu wenye ulemavu wa kusikia.