Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wizara yataja vipaumbele vitano ya elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Adolf Mkenda

Muktasari:

  • Vipaumbele hivyo ni pamoja na  kufanya mapitio ya sheria, kuandaa miongozo na kutoa mafunzo, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo.

Dodoma. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetaja vipaumbele vitano katika bajeti Sh2.4 trilioni kwa mwaka 2026/27, huku ikitupia jicho maandalizi ya kidato cha kwanza 2028 na mafunzo kwa shule za amali.

Kati ya fedha hizo, Sh1.7 trilioni zimeombwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ambapo Sh1.3 trilioni ni fedha za ndani,  wakati Sh360 bilioni zikitarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Adolf Mkenda amewasilisha bajeti hiyo ikiwa pungufu ya  bajeti ya mwaka 2025/26 iliyokuwa Sh2.436 trilioni.

Ametaja vipaumbele hivyo  kuwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa sera na mitalaa, kufanya mapitio ya sheria, kuandaa miongozo na kutoa mafunzo, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo na kuongeza fursa katika kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi na sekondari.

Vipaumbele vingine kwenye bajeti hiyo ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchochea uchumi wa viwanda. 

Waziri amesema, wizara itaendelea kuweka jitihada  katika maandalizi ya elimu ya lazima ya miaka 10, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, kuimarisha matumizi ya Tehama katika elimu na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuendana na Dira 2050.

Kuhusu kupokea madarasa mawili ya kidato cha kwanza mwaka 2028, amesema:  “Serikali itaendelea na maandalizi ya elimu ya lazima ya miaka 10 ili kupokea wanafunzi wa darasa la sita na la saba mwezi Januari 2028, utekelezaji wa jambo hili unafanywa na Tamisemi, lakini Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaandaa miongozo, kutafuta rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa na vinavyohitajika.’’

Amesema Serikali itafanya mkakati wa Kitaifa wa Kisomo na Elimu kwa Umma, kwa lengo la kuimarisha ushiriki wa umma katika kupata maarifa, ujuzi na stadi za maisha kupitia elimu ya watu wazima.

Amesema wataandaa na kusambaza kiunzi cha Taifa cha Elimu Jumuishi ili kuwezesha utekelezaji wa elimu jumuishi,  lakini kuwa na mwongozo wa kitaifa wa uendelezaji wa wakufunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na wafanyakazi wasio wakufunzi.

Kuhusu ubunifu, Waziri  Mkenda amesema ili kuimarisha ufanisi na mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia (1996) ili iendane mahitaji ya nchi katika sayansi, teknolojia, ubunifu na utafiti.

Kwa upande wa shule za amali, bajeti ijayo inakwenda kusajili vyuo 263 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ambapo kati ya hivyo,vyuo vya elimu ya ufundi ni 45, vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 152 na shule za sekondari za amali 66.

Idadi hiyo itafikisha vyuo 577 vya elimu ya ufundi, vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi 1,066 na shule za sekondari za amali zitafikia 267,  huku wakilenga kudahili jumla ya wanafunzi 374,000 wa elimu ya ufundi na mafunzo na ufundi stadi.

Ametaja kuwa, ongezeko la udahili wa wanafunzi wa vyuo vya ufundi kutaongeza idadi ya vijana wenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kulingana na mahitaji ya soko la ajira kitaifa na kimataifa.

Katika maboresho hayo, Wizara imetangaza kuandaa vigezo vya umahiri katika programu 50 za mafunzo yanayotolewa na vyuo vya elimu ya ufundi,  ili kuandaa wataalamu na mitalaa kulingana na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa upande wa walimu, Serikali, itatoa mafunzo kuhusu mbinu za kufundishia na kujifunzia kwa walimu wapya wapatao 1,427 (amali 207 na biashara 1,220) wa shule za sekondari za amali na mafunzo ya muda mrefu ya ufundi stadi kwa washiriki 15,000 katika vyuo vya maendeleo ya wananchi 55.

Kwenye ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari,  amesema watawezesha ujenzi wa madarasa 1,360 kwa ajili ya utekelezaji wa elimu ya miaka 10 ya lazima, mabweni 17 kwa shule za sekondari 17, nyumba 33 za walimu na vituo 50 vya walimu.


Maoni ya kamati

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge Utamaduni na Michezo imesema kutokamilika kwa ujenzi wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kunatokana na mtiririko mdogo wa fedha.

Akisoma maoni ya kamati hiyo, mjumbe, Asha Feruzi amesema pia kutoktolewa kwa fedha za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa ukamilifu,  kunaathiri lengo la Serikali la kutoa mikopo ya wanafunzi wa ili kuwapunguzia vikwazo vya kiuchumi katika kupata elimu bora. 

Katika mchango wake,  ameeleza masikitiko yake kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakizuiwa kufanya mitihani yao ya mwisho kwa madai ya kushindwa kulipa ada,  jambo alilosema linawaumiza vijana.

Aidha, kamati imeomba wizara kuongeza kasi ya ununuzi wa vitabu,  kutokana na ongezeko la wanafunzi linalosababisha uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi kutoka 1:3 hadi 1:5.

“Tunaitaka Serikali itoe fedha zote za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kama zilivyoidhinishwa na Bunge kwa wakati na kwa wanafunzi wote wenye sifa za kupata mikopo hiyo ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwapunguzia vikwazo vya kiuchumi wanufaika katika kupata elimu bora,” amesema Feruzi.

Pia mbunge huyo ameomba Serikali iandae mkakati wa kuviwezesha vyuo kuwa na hospitali za mafunzo kwa vitendo.