Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waasisi chama cha siasa IPP wamburuza Msajili kortini

Dar es Salaam. Waasisi wa chama cha siasa cha Independent People's Party (IPP), wamefungua shauri Mahakama Kuu dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushindwa kukipa usajili wa muda chama hicho kwa miaka miwili sasa.

Maombi hayo ya mwaka 2025 yaliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, masjala ndogo ya Dar es Salaam, yamepangwa kutajwa Mei 22, 2025 saa 2:30 asubuhi, mbele ya Jaji Obadia Bwegoge.

Katika maombi hayo, waasisi hao, Vyonheaven Urima na Andrew Bomani wamemuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kama mjibu maombi wa pili.

Kwa mujibu wa wito, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilipokea wito huo wa Mahakama Aprili 24, 2025, AG alipokea nyaraka hizo Aprili 21, 2025 na Ofisi ya Msajili Aprili 24, 2025 na wote wamegonga mihuri.

Waasisi hao wa IPP wanaiomba Mahakama iwape kibali cha kufungua maombi ili itoe maagizo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania kukipa usajili wa muda chama hicho kipya cha siasa.


Wanacholalamikia

Waasisi hao wanalalamika kuwa Mei 3, 2023 waliwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, maombi ya kusajiliwa chama cha IPP kwa kujaza fomu kama inavyoelekezwa katika sheria ya usajili wa vyama vya siasa nchini.

Baada ya kuwasilisha maombi, wanadai Juni 8, 2023 Ofisi ya Msajili iliwaandikia barua yenye ikikiri kupokea maombi yao kwa ajili ya usajili wa muda wa chama hicho.

Katika barua hiyo, Msajili aliwataka wawasilishe nakala tete (soft copies) ya katiba ya chama, uthibitisho wa uraia wa waombaji, bendera ya chama, vyeti vya kuzaliwa vya waasisi hao na uthibitisho kuwa wamelipa ada ya usajili wa chama cha siasa.

Baada ya kupokea barua hiyo, waasisi hao walitimiza maelekezo na kuwasilisha nyaraka hizo kama walivyoelekezwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, wakiamini wametimiza matakwa ya kisheria kupata usajili wa muda.

Hata hivyo, Novemba 2, 2023 Msajili aliwaandikia barua nyingine yenye akiwataka wawasilishe baadhi ya viambatanisho ambavyo msajili alieleza havikuwa vimewasilishwa.

Viambatanisho hivyo ni sera ya chama, uthibitisho wa uraia wa waasisi, vyeti vyao vya kuzaliwa na fomu namba PP1 na PP2 ambazo ni kwa ajili ya kuomba usajili ili ombi lao lifanyiwe kazi na Msajili.

Miezi mitatu baadaye baada ya kuwa wamewasilisha kila nyaraka iliyohitajika, wanadai Msajili aliwaandikia barua nyingine Machi 4, 2024 ikiwa na maelekezo wanayodai yalikuwa yakijirudia kama ya awali ambayo walitakiwa kuyatekeleza.

Wanadai waliwasilisha tena nyaraka hizo kama walivyotakiwa na Msajili lakini, bado aliendelea kuwa kimya juu ya usajili wa chama hicho pasipo kuwapa sababu za ukimya huo.

Machi 6, 2024, waombaji wanadai walimwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa wakielezea masikitiko yao kutokana na urasimu usio wa lazima na ukimya wake katika kukisajili chama hicho kipya.

Waasisi hao kupitia hati ya kiapo cha pamoja wanadai Msajili kwa sababu anazozijua bado aliendelea kukaa kimya pasipo kujibu barua hiyo.

Mei 18, 2024 kupitia wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), alimwandikia Msajili barua kuulizia suala hilo akiambatanisha na viambatanisho walivyovituma awali.

Barua hiyo haikujibiwa, Septemba 4, 2024 waasisi hao kupitia LHRC waliandika barua nyingine kukumbushia na Novemba 13, 2024 wakaandika tena barua.

Barua zote hizo wanadai hazikujibiwa na Msajili.


Wanachoomba

Waasisi hao wameiomba mahakama iwape kibali wafungue maombi ya kisheria ili kuiagiza Ofisi ya Msajili kukipa usajili wa muda chama hicho.

“Labda tu kama maombi haya yatakubaliwa lakini tofauti na hivyo, waombaji wataathirika na kupata hasara isiyoweza kufidiwa kulinganisha na hasara ambayo wajibu maombi ambao ni Msajili wa vyama na AG wataipata,” wanadai katika hati ya kiapo.

Wanadai Msajili amekiuka vifungu vya 8 na 9 vya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 ambavyo vimeweka masharti ya usajili wa chama cha siasa. Wanadai Msajili amewanyima haki yao ya kikatiba na amekaa kimya kwa miaka miwili.

“Kwamba wajibu maombi wamekiuka ibara ya 20 na 21 ya Katiba kwa kuwanyima waombaji usajili wa muda, hivyo kuwanyima haki ya msingi ya kikatiba ya kukusanyika pamoja na uhuru wa kushiriki katika mambo ya umma,” wanadai.

Pia wanadai wamekiuka misingi ya haki za asili kwa msajili kushindwa kukisajili chama hicho na siyo tu kukiuka Katiba bali ni kinyume cha haki ya asili kwa kushindwa kuwaeleza sababu kwa nini anakataa kusajili chama chao.

Maombi hayo yamepangwa kutajwa Mei 22, 2025. Msajili wa Vyama vya Siasa na AG wametakiwa kuhudhuria pasipo kukosa na kuwasilisha nyaraka zozote ambazo wanakusudia kuzitumia kujenga msingi wa utetezi wao katika maombi hayo.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hadi kufikia Machi 17, 2025, Tanzania ina vyama 19 vyenye usajili wa kudumu, ambavyo vyote vimesaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu 2025 isipokuwa Chadema.

Vyama hivyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM),  chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo). Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Civic United Front (CUF), Union for Multiparty Democracy (UMD) na National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi).

Katika orodha hiyo, vimo National League for Democracy (NLD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP), National Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA) na Tanzania Labour Party (TLP).

Pia katika orodha hiyo vimo United Democratic Party (UDP), Chama cha Demokrasia Makini (Makini), Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Chama cha Kijamii (CCK).

Vingine ni Alliance for Democratic Change (ADC) na  Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).