Vituo vya afya Nyankumbu, Kasamwa vyapewa vitanda

Muktasari:
- Vituo vya afya vya Nyankumbu na Kasamwa vya Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani hapa, vimekabidhiwa msaada wa vitanda vine vya kina mama kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).
Geita. Vituo vya afya vya Nyankumbu na Kasamwa vya Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani hapa, vimekabidhiwa msaada wa vitanda vine vya kina mama kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).
Msaada huo umekabidhiwa wiki iliyopita na Meneja Mwandamizi Mahusiano wa kampuni hiyo Gilbert Mworia, baada ya kupokea ombi la vituo hivyo kuhusu adha wanayopata wanawake kutokana na upungufu wa vitanda hivyo.
Mworia alisema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Machi 2023, kampuni hiyo ilipokea ombi kuhusu uhaba wa vitanda vya kujifungulia kutoka kwa wanawake wa maeneo hayo.
“Leo tunakabidhi rasmi vitanda hivi ambavyo wazo lake lilitokana na adha wanazopata akina mama wakati wa kujifungua, ugumu wa maisha ambao ulibainishwa na akina mama wa Geita,” amesema.
Aidha, akizungumza makabidhiano ya vitandani hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe amewaagiza timu ya madaktari wa vituo vya afya vya Kasamwa na Nyankumbu kutunza vitanda hivyo vya kujifungulia vilivyotolewa.
"Hatupati msaada wa aina hii mara kwa mara kwa hivyo ninawahimiza kila mmoja wenu hapa kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika suala la utunzaji mzuri wa vitanda hivi vilivyotolewa," alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Nyankumbu, Irene Temba alipongeza GGML kwa msaada huo na kubainisha kuwa kituo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto nyingi hususani katika upande wa huduma ya kujifungua.
"Tunarekodi ya kuzaliwa kwa watoto wasiopungua 300 kila mwezi jambo ambalo huwalazimu baadhi ya mama zetu kutumia vitanda vya kawaida wakati wa kujifungua.” Amesema na kuongeza;
“Tungependa katika siku za usoni, GGML ifikirie pia kutusaidia na vitanda vya kufanyia uchunguzi, samani na vifaa vingine kwa sababu kila mwezi hapa tunapokea zaidi ya kesi 1,000 za huduma ya afya ya uzazi na ujauzito. Pia tunatoa huduma kwa watu 1,000 kila mwezi katika Kituo cha Matunzo na Tiba,” alisema.
Mmoja wa wanufaika wa awamu ya pili ya vitanda vya kujifungulia katika Kituo cha Afya cha Kasamwa, Mganga Mfawidhi Thomas Mafuru pia ameshukuru kwa msaada huo.