Vifo vyafikia 42 ajali ya Same

Muktasari:
- Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi la Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi.
Moshi. Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ajali ya kugongana uso kwa uso kwa magari mawili katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, imeongezeka na kufikia 42.
Majeruhi wawili wa ajali hiyo bado wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, baada ya wengine 24 kuruhusiwa.
Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025, katika eneo la Sabasaba, Same mjini. Ilihusisha basi la Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitoka Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi. Magari hayo yaligongana uso kwa uso na kuwaka moto yakiwa na abiria ndani.
Akizungumza leo Jumatano Julai 2, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema; “Awali tulitoa taarifa ya vifo vya watu 39 lakini mpaka sasa kuna ongezeko na sasa vimefikia 42.”
Amesema kati ya waliopoteza maisha, 31 walikuwa kwenye Coaster (wanawake 21 na wanaume 10) na 11 walikuwa kwenye basi la Chanel One. Hivyo, jumla ya vifo ni 42.
“Jumla ya abiria wote katika magari hayo mawili walikuwa 67, wakiwemo watu wazima 64 na watoto watatu,” amesema Babu.
Kuhusu chanzo cha ajali hiyo, amesema uchunguzi umebaini kuwa ni kupasuka kwa tairi la mbele upande wa kulia wa basi la Chanel One.
“Hali hiyo ilisababisha dereva kushindwa kulimudu gari na kuvuka kwenda upande wa kulia wa barabara, ambako aligongana uso kwa uso na Coaster na magari yote yakawaka moto,” amesema Babu.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.