Janga la ajali laibua mjadala wa tiba

Muktasari:
- Matukio ya ajali wilayani Same si jambo adimu kutokea, hasa tangu ulipoanza mwaka huu. Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ndani ya miezi mitatu (Januari–Aprili), zimetokea ajali 1,322 na kusababisha vifo vya watu 1,275.
Dar/mikoani. Tukio la ajali iliyohusisha mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso katika eneo la Sabasaba, Same Mjini, mkoani Kilimanjaro, limeondoa uhai wa watu 38, huku wengine 29 wakijeruhiwa.
Katika ajali hiyo, basi la Kampuni ya Channel One na basi dogo aina ya Coaster yaligongana uso kwa uso na kuwaka moto papo hapo katika eneo hilo lenye historia ya mfululizo wa matukio ya ajali.
Ajali hiyo, iliyotokea jana, Juni 28, 2025, ndiyo inayotajwa kugharimu uhai wa watu wengi zaidi kati ya zote za barabarani zilizowahi kutokea tangu kuanza kwa mwaka huu.
Tukio hilo linatokea siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka wazi kuwa ajali za barabarani ndilo eneo ambalo Jeshi la Polisi halijafanikiwa vema kulidhibiti.
“Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani, lazima nazo tuendelee kuzitafutia muarobaini wake,” alisema Rais Samia katika hotuba yake ya kuhitimisha Bunge la 12, Juni 27, mwaka huu.
Sio tukio la kwanza
Watu hao waliofariki dunia kwa pamoja katika ajali hiyo ni rekodi mpya ya kwa mwaka huu, baada ya Juni 7, 2025, watu 28 kufariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu eneo la Mlima Iwambi jijini Mbeya.
Ajali hiyo wilayani Same si ya kwanza, kwani Machi 30, 2025, watu saba wakiwemo wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Chome – Usharika wa Mmeni, walifariki dunia papo hapo na wengine 23 kujeruhiwa.
Hii ni baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kupinduka katika milima ya Pare, wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro.
Chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu katika mfumo wa breki na kusababisha gari kurudi nyuma kwa kasi kabla ya kuteleza na kupinduka.
Vilevile, Aprili 3, 2025, watu wanane walifariki dunia na wengine 31 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Matukio hayo ya ajali yanayoripotiwa kila uchwao ndiyo yamemfanya Rais Samia, wakati akihutubia hotuba ya kulifunga Bunge la 12 jijini Dodoma, kukiri kuwa tatizo la ajali za barabarani linahitaji kutafutiwa muarobaini.
Kwa mujibu wa Rais Samia, ndani ya miezi mitatu (Januari–Aprili), zimetokea ajali 1,322 na kusababisha vifo vya watu 1,275.
Kutokana na hilo, mkuu huyo wa nchi, Juni 9, 2025, alipohutubia hafla ya kufunga mafunzo ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa Jeshi la Polisi, alitaka kuwe na mkakati wa kukomesha matukio hayo.
“Kila tunavyochukua hatua, ndivyo ajali nazo zinaongezeka. Sasa hebu tulitazameni vizuri eneo hili kuna nini hasa. Kama ni barabara zetu, kama Taifa, tufunge mikaja eneo lingine tutengeneze barabara zetu ili ajali zisitokee.
“Kama ni kufunga vifaa vya usalama barabarani, tufanye hivyo. Kama ni uzembe wa madereva, wawekwe wafundishwe. Muweke masharti magumu ya kumfanya mtu kuwa dereva,” alisema Rais Samia.
Hata hivyo, sababu ya kushamiri kwa matukio ya ajali inawekwa wazi na ripoti mbalimbali za Jeshi la Polisi, ikiwemo iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2025.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa chanzo kikuu cha ajali za barabarani zilizotokea mwaka 2024 ni uzembe wa madereva wa vyombo vya moto, uliochangia asilimia 44.1 ya ajali zote zilizotokea kwa mwaka huo.
Kwa nini Same
Baadhi ya madereva wanaotumia Barabara Kuu ya Same–Mwanga–Moshi wameeleza kuwa barabara hiyo imekuwa ikichangia ajali za mara kwa mara, huku wakitaja upepo mkali kama moja ya changamoto kuu.
Abdalah Mgonja, dereva anayefanya safari katika eneo hilo, amesema kuwa barabara hiyo hukumbwa na upepo mkali na pia ina changamoto ya wembamba, hali inayoongeza hatari.
“Wakati mwingine tunakabiliana na upepo mkali kwenye hii barabara, na kila siku kuna ajali hapa Same,” amesema Mgonja.
Dereva mwingine, Omari Shaban, amesema mbali na tatizo la upepo, wananchi pia wamekuwa wakipitisha mifugo katikati ya barabara hiyo, jambo ambalo limekuwa likisababisha ajali za mara kwa mara.
“Unakuta uko kwenye mwendo, ghafla mfugaji na mifugo yake unakuta inakatiza barabarani hata maeneo ambayo hayana tahadhari,hiyo nayo inawatesa sana madereva hasa wale wanaoendesha magari ya abiria,” amesema Shaban.
Pia amesema eneo hilo lina ukungu mwingi hasa kipindi cha baridi na kusababisha madereva kutoona mbele.
Tunakomeshaje
Mkurugenzi na mwanzilishi wa taasisi inayojihusisha na maafa na majanga (Sukos), Kamishna wa Polisi mstaafu, Suleiman Kova, amesema pamoja na mbinu nyingine, makali ya kisheria ni moja ya hatua muhimu za kukabili majanga ya ajali.
Makali hayo yanayopaswa kuongezwa kisheria, amesema, ni pamoja na kuwanyang’anya leseni madereva wenye mfululizo wa matukio ya makosa barabarani.
Ukali wa kisheria, ametaka, uambatane na mafunzo ya udereva wa kujihami kwa madereva wote nchini ili wawe na uwezo wa kuendesha katika mazingira ya kuziba makosa ya dereva mwenzake.
“Sheria inayohusu umiliki wa leseni iwe na sheria kali. Dereva akifanya makosa ya mara kwa mara wanyang’anywe leseni. Kuwe na kumbukumbu za mwenendo wa dereva husika,” amesema.
Jambo lingine alilopendekeza ni kuwepo mwendelezo wa mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva kama inavyofanyika kwa taaluma nyingine.
“Lazima kuwepo na semina na makongamano ili madereva wapate angalau ushauri wa namna ya kuboresha weledi wao. Mafunzo ya mara kwa mara hakuna kwa madereva,” amesema Kova.
Kwa sababu Tanzania inapokea magari ya aina nyingi kutoka mataifa mbalimbali, kamanda huyo mstaafu amesema mafunzo ya udereva yanapaswa kujielekeza kwa gari husika, isiwe kila dereva anaendesha kila gari.
“Siku hizi dereva akiomba kazi, kila gari anapewa aendeshe, hiyo si sahihi,” amesema Kova.
Kwa upande wa bodaboda, amesema wanapaswa kupewa mafunzo ya namna ya kutekeleza sheria ya usalama barabarani ili wasiwe chanzo cha ajali.
“Suala la ajali barabarani linawahusu zaidi madereva, ingawa kuna sababu nyingi ikiwemo ufinyu wa barabara, ubovu wa barabara na ubovu wa magari.
“Lakini dhima kubwa inamuangukia dereva, na tatizo kubwa ni kwamba madereva wanafanya kazi kwa mazoea, si kwa kujihami. Hawaendeshi kwa kujihami,” amesisitiza.
Mmoja wa wahandisi waandamizi waliosimamia ujenzi wa madaraja kadhaa nchini, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema barabara si tatizo, kwa sababu ujenzi wake umezingatia viwango vya kimataifa.
Katika ujenzi wa barabara hizo, amesema, yamezingatiwa makundi yote ya watumiaji, ndiyo sababu kumewekwa alama za barabarani.
Tatizo, amesema, ni elimu duni kwa watumiaji wa barabara, ndiyo inayosababisha matukio ya ajali, na wengine kuamua kutozingatia sheria.
“Viwango vyote vya barabara zetu ni vya kimataifa, lakini shida kubwa ni elimu kwa watumiaji wa barabara. Barabara zote nchini zimejengwa kukidhi mahitaji ya watumiaji wote, kwa hiyo barabara si shida,” amesema.