Vifo vyafikia 37 ajali ya magari mawili Same, chanzo chatajwa

Muktasari:
- Aidha, Babu amesema baadhi ya miili iliyoungua katika ajali hiyo bado haijatambuliwa hivyo serikali itafanya vipimo vya Vinasaba (DNA) ili kubaini miili hiyo.
Same. Idadi ya vifo vilivyokana na ajali ya magari mawili kugoganga uso kwa uso na kupelekea kuwaka moto Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro imeongezeka na kufikia vifo 37 baada ya majeruhi mmoja kufariki na kusalia 29.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Juni 28, 2025 na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi alisema ajali hiyo ilitokea eneo la Sabasaba, Same mjini, ikihusisha basi Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuungua moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.

Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema ajali hiyo ni msiba mkubwa kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla na kwamba haijawahi kutokea.
Babu amesema, mpaka jana usiku waliofariki ni 37 na majeruhi ni 29, ambapo kati ya majeruhi hao majeruhi 24 wapo katika Hospitali ya Mji wa Same na watano wapo katika Hospitali za KCMC na Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.
Aidha, Babu amesema baadhi ya miili iliyoungua katika ajali hiyo bado haijatambuliwa hivyo serikali itafanya vipimo vya Vinasaba (DNA) ili kubaini miili hiyo.

"Serikali itaanza kufanya utaratibu wa upimaji wa vinasaba (DNA) kwa miili ya marehemu ili iwe rahisi kutambua ndugu na jamaa zao kutokana na miili hiyo kuungua vibaya na kutotambulika kirahisi," amasema RC Babu
Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa amewaomba ndugu, jamaa na marafiki kuendelea kufuatilia taarifa za ndugu zao ambao hawajawaona mpaka sasa ili kujiridhisha kwa kuwa ipo miili ambayo haijatambuliwa kutokana na kuungua.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tayari ya basi la Kampuni ya Chanel One na kupoteza mwelekeo na kwenda kugongana uso kwa uso na Coaster.

Kamanda Maigwa amesema, taarifa zaidi kuhusiana na ajali hiyo zitaendelea kutolewa kadri uchunguzi na zoezi la utambuzi wa miili unavyoendelea.