Ajali ya Hiace, bajaji yasababisha vifo sita, majeruhi 21

Watu sita wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha Toyota Hiace na bajaji katika mteremko wa Mlima Ulinji, uliopo Kijiji cha Ulinji, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumamosi Juni 28, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere imesema Hiace ilipinduka katika Kata ya Mollo.

Amesema waliofariki dunia ni watu wazima watatu (wanaume wawili na mwanamke mmoja) na watoto watatu (wavulana wawili na msichana mmoja).
Makongoro amesema miili imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ismail Macha amethibitisha kupokea majeruhi na miili ya watu waliopoteza maisha.
Kuhusu majeruhi amesema wanaume ni wanane na wanawake 13, ambao wamepelekwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.
Amewataka madereva wa vyombo vya moto kuwa makini wanapoedesha vyombo hivyo na wamiliki kuhakikisha vinakuwa salama wakati wote ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.