Ajali ya lori la makaa ya mawe yagharimu maisha ya watu Lindi, wanne wajeruhiwa

Muktasari:
- Lori la makaa ya mawe lagonga watu Kijiji cha Mtegu mkoani Lindi na kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine wanne wajeruhiwa, akiwemo mtoto wa miaka mitatu.
Lindi. Watu wanne wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya kugongwa na lori la mizigo lililokuwa likisafirisha makaa ya mawe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amesema lori hilo mali ya kampuni ya Specialised Hauliers Ltd, likiwa na mzigo wa makaa ya mawe, baada ya kufika kwenye mteremko katika Kijiji cha Mtegu ndipo lilitoka pembezoni mwa barabara likiwa mwendo wa kasi na kuwagonga watu zaidi ya 10.
Kamanda Imori amesema ajali hiyo ilitokea jana Ijumaa Juni 27, 2025, mida ya saa moja usiku baada ya kufika kwenye mteremko wa Kijiji cha Mtegu mkoani Lindi.
Akitoa taarifa ya ajali hilo leo Jumamosi Juni 28, 2025 Kamanda Imori amesema lori hilo lilikuwa safarini likitoka Mkoa wa Ruvuma kwenda Mtwara.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi John Imori akiangalia gari lililosababisha vifo vya watu wa nne papo hapo.
Kamanda Imori amewataja waliofariki dunia kwenye ajali hiyo ni Salumu Mangowela (61), Shamte Mangowela (73), Amina Kuchekecha (36) na Roza Namiundu (19).
Pia, amewataja majeruhi wa ajali hiyo ni Raufu Mohamed (21), Nasra Manjeda (22), Salha Falhani (17) na mtoto wa miaka mitatu Musali Mangowela, ambaye amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula mkoani Mtwara, kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, majeruhi wengine watatu walipatiwa matibabu katika Zahanati ya Madangwa na kuruhusiwa.
"Chanzo cha ajali hiyo gari liliacha njia likiwa kwenye mwendo kasi na kisha kuelekea upande wa kulia na kuwagonga watu waliokuwa maeneo hayo na kusababisha vifo vya watu wanne." amesema Kamanda Imori.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Irun Saidi amesema kuwa wakati ajali hiyo ikitokea, alikuwa nyumbani kwake aliposhuhudia lori hilo likitoka barabarani na kuingia kwenye makazi ya watu, hali iliyosababisha vifo.

"Mimi nilikuwa nyumbani ghafla nikaona gari linatoka barabarani kwenda kwenye makazi ya watu na kusababisha vifo misiba hii ni mizito kwetu kwani ni watu ambao tulikuwa tunaishi nao kwa wema," amesema Saidi.