Mama asimulia alivyomwokoa kichanga akimtupa dirishani ajali iliyoua watu 37 Same

Muktasari:
- Ajali hiyo iliyoua watu 37 na majeruhi 30 ilitokea eneo la Sabasaba, Same mjini, baada ya basi Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuungua moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Same. Domitilia Ezekiel amabye ni mama wa mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi miwili amesimulia namna alivyokitupa kichanga kupitia dirishani ili kumuokoa, huku yeye akinusurika kwa kurushwa nje ya gari baada ya kioo kupasuka katika ajali iliyoua watu 37 na majeruhi 30, wilayani Same.
Miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni wananchi wa wilaya hiyo ambao walikuwa wakienda kwenye sherehe iliyokuwa inafanyika Moshi mjini.
Jana Juni 28, 2025 Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi alisema ajali hiyo ilitokea eneo la Sabasaba, Same Mjini, baada ya basi kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuungua moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Akisimulia ajali hiyo iliyotokea mama wa kichanga hicho, amesema wakati ajali ilivyotokea walibanwa kwenye gari hivyo akaamua kukirusha kichanga hicho dirishani ili kukiokoa.
"Nilikuwa natokea Moshi kwenda Tanga kwenye msiba lakini tulipofika pale ajali ilipotokea, tulishindwa kutoka na hatukupata mtu wa kuja kutuokoa kwa ule muda," anasimulia mama huyo.
Anasema "Ilibidi nimrushe mtoto wangu kwa dirishani kwanza, na wakati huo mimi miguu yangu ilikuwa umebanwa kwenye gari, lakini Mungu alinisaidia maana nilikuwa nimekaa upande wa dirishani, kioo kilipodondoka na mimi nikadondoshwa kama gunia, sikuweza kuruka maana miguu ilikuwa inauma," amesimua.
Mama huyo amesema kupona kwake katika ajali hiyo ni neema ya Mungu kwa kuwa wenzake wengi walifariki.
"Wenzetu wamekufa, nashukuru Mungu sisi tumepona na majeraha ni madogo, tunamshukuru sana Mungu wetu," amesema mama huyo.
Ajali hiyo imetokea miezi mitatu baada ya ajali nyingine kutokea Machi 30, 2025, ambayo ilihusisha watu saba, wakiwemo wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mmeni Chome, baada ya gari aina ya Coaster walilokuwa wakisafiria kupinduka katika Milima ya Pare, na kujeruhi wengine 23.