Vifo vyafikia 39, ajali ya magari mawili kugongana Same

Muktasari:
- Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi la kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Moshi. Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya magari mawili yaliyogongana uso kwa uso Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro imeongezeka na kufikia 39, huku mabaki ya miili 33 ikipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi la kampuni ya Chanel one lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Akizungumzia hali za majeruhi Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema 22 kati ya 28 wameruhusiwa hospitalini baada ya afya zao kuimarika.
Amesema mabaki ya miili 33 yamepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuitambua na kuikabidhi kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi. Ambapo miili mitano imeshatambuliwa.
"Katika ajali hiyo iliyotokea Juni 28 watu 38 walipoteza maisha, tulikuwa na majeruhi sita baada ya 22 kuruhusiwa jana, lakini kwa bahati mbaya majeruhi mmoja aliyelazwa Hospitali ya KCMC leo asubuhi amefariki dunia kwa hiyo sasa tuna watu 39 ambao wamefariki."
"Wananchi hawa ni wa maeneo mbalimbali kwa hiyo hawa watano wametambuliwa kwa sababu hawakuungua sana na leo ndugu wataruhusiwa kuchukua miili yao kwa ajili ya kwenda kuhifadhiwa,”amesema Babu.