Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya mzee aliyepoteza 10 ajalini Same

Muktasari:

  • Kati ya watu 38 waliopoteza maisha katika ajali wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, Abdalah Kiluvia ana ndugu na jamaa 10 ndani yake.

Same. Matarajio ya kusherehekea harusi yamegeuka huzuni na majonzi kwa familia ya mzee Kiluvia, anayeishi Ngusero, Same Mjini, mkoani Kilimanjaro, baada ya kupoteza watu 10, kati yao ndugu zake ni wanne na sita ni wapangaji wake.

Watu hao ni kati ya 38 waliopoteza maisha katika ajali ya Basi la Kampuni ya Channel One na basi dogo aina ya Coaster, yaliyogongana uso kwa uso na kuwaka moto, Sabasaba wilayani humo.

Watu hao walikuwa wakisafiri kwa gari dogo la abiria aina ya Toyota Coaster waliyopanda kutoka Same kwenda Moshi Mjini, kwenye sherehe ya harusi ya ndugu yao, iliyokuwa ikifanyika katika ukumbi wa Kuringe, mjini Moshi.

Katika ajali hiyo iliyotokea jana, Juni 28, 2025, watu 29 wamejeruhiwa na ilitokea eneo la Sabasaba, Same Mjini wakati basi la Channel One likitokea Moshi kwenda Tanga na Coaster ikitoka Same Mjini kwenda Moshi. Magari hayo yalipogongana yaliwaka moto, huku abiria wakiwa ndani.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi ya basi la Channel One, kulikosababisha dereva kupoteza mwelekeo na kwenda kugongana uso kwa uso na Coaster.

Kati ya waliojeruhiwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema 24 walipelekwa katika Hospitali ya Mji wa Same na watano katika Hospitali za KCMC na Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi.

Simulizi aliyepoteza 10

Ingawa tukio kama hilo ni pigo kwa Taifa, lakini kwa Abdalah Kiluvia ni simulizi chungu zaidi, baada ya kile alichoeleza, amepoteza ndugu wanne na wapangaji sita katika ajali hiyo.

Kiluvia amesema wote hao waliungua kiasi cha kutotambulika kwa macho ya kawaida, bali msaada wa vipimo vya vinasaba (DNA).

"Ukweli wa kwamba hakuna ambacho unaweza kukitambua, ndio maana tunafanya utaratibu wa kwenda Hospitali ya KCMC kufanya DNA angalau yale mabaki tuyahifadhi, lakini hakuna kitu unaweza kukitambua, waliungua sana," amesema.

Kati ya ndugu wanne aliowapoteza, amesema yumo mdogo wake, shemeji yake na ndugu wengine wawili, sambamba na wapangaji sita, walioambatana katika safari hiyo ya kwenda harusini.

"Tunasikitika kupoteza watu wanne kwa wakati mmoja, ni msiba mkubwa kwenye nyumba hii, lakini wapangaji sita wa nyumba hii, nao ni msiba mzito," amesema Kiluvia.

Majonzi hayo sio kwa mzee Kiluvia pekee, hata mwanawe, Ramadhani Kiluvia anakabiliwa nayo, akisema amepoteza mama na mdogo wake.

Akiwa Moshi katika maandalizi ya harusi, amesema badala ya taarifa ya kuwapokea ndugu zake hao, akaarifiwa kuhusu ajali inayohusisha gari walilopanda nduguze.

"Nimempoteza mama na mdogo wangu, shangazi, dada wa baba yetu mkubwa na majirani wa hapa, walikuwa wamepanda gari moja kuja Moshi kwenye harusi ya ndugu yetu," amesimulia huku akibubujikwa na machozi.

Baada ya taarifa ya tukio la ajali, amesema alijaribu kupiga simu mara kadhaa kwa nduguze waliokuwa ndani ya Coaster bila mafanikio, baadaye akaambiwa gari hiyo imewaka moto, hivyo hakuna aliyepona.

"Bahati nzuri nilimpata aliyekuwa nyumbani akasema kuna gari limewaka moto pale Sabasaba, sidhani kama mtu aliyekuwa kwenye Coaster amepona, ilibidi nizime simu maana wote waliokuwa wamepanda lile gari watu 30 wote ni familia," amesimulia Ramadhani.

Ameeleza baadaye akaambiwa kuna mtu aliyeona nguo aliyokuwa amevaa mama yake na hata alipofika chumba cha kuhifadhia maiti kukagua miili ya ndugu zake, hakufanikiwa, kwa jinsi walivyoungua.

"Nilifika mochuari kumtafuta mama yangu na mdogo wangu hakuna hata mmoja niliyemuona, maana wakati nafika eneo la tukio watu walikuwa wanachukua mabaki ya miili kwenye eneo la tukio," amesimulia.

Mwingine aliyepoteza ndugu kwenye ajali hiyo ni Gloria Nehemiah, aliyesema amepoteza mama yake mzazi.

"Nimempoteza mama yangu mzazi wakati wakienda kwenye harusi Moshi, sisi tulikuwa tumeshatangulia na gari jingine na wao walikuja na gari jingine," amesema.

Amesema muda mfupi baada ya ajali hiyo, alimpigia simu mama yake mzazi na hakupokea na baada ya kufuatilia alipata taarifa ya ajali.

"Taarifa tulizipata tukiwa tumeshafika Moshi, nilijaribu kupiga simu ya mama yangu ikawa haipatikani na wote aliokuwa nao mama yangu, wote walikuwa ni mama zangu, jambo lao lilikuwa ni jambo letu.

"Nakumbuka mara ya mwisho kuongea na mama ilikuwa saa 11 jioni hivi, nilimwambia naenda, akanambia Mungu akubariki ufike salama na mimi nikamwambia Mungu akubariki ufike salama, ndio yalikuwa maneno yetu ya mwisho," ameeleza binti huyo huku akitokwa na majonzi.

Majeruhi wasimulia

Mudin Waziri, ni majeruhi wa ajali hiyo aliyelazwa katika Hospitali ya Mjini Same, amesema alikaa siti ya nyuma, wakati ajali inatokea alirushwa mbele na wakati huo kila mtu alikuwa akipambana kivyake kutoka ndani ya basi.

"Nilitokea Arusha kwenda Tanga na nilikuwa nimekaa siti ya nyuma kabisa, ghafla nilisikia mtikisiko mkubwa na mbele sikuona ni nini kinaendelea, wakati moto unawaka nilijikuta nipo mlangoni nimetupwa na ndio iliyonisababishia kuvunjika sehemu ya nyonga," amesema.

Majeruhi mwingine, Miliad Mndeme amesema akiwa ndani ya basi la Channel One tairi la mbele upande wa kushoto lilipasuka na kugongana na gari lingine na kushika moto.

"Nilikuwa natokea Njoro kuja Same Mjini, basi nililopanda lilipasuka tairi upande wa kushoto na kuwaka moto, bahati tulisaidiwa na kukimbizwa hospitalini," amesema.


Daktari azungumza

Akizungumzia vifo na majeruhi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Same, Dk Lwitiko Mwalukumba amesema miili minne kati ya mitano ambayo haikuungua sana imetambuliwa.

"Jana tulikuwa na majeruhi 30 kati ya hao sita walipewa rufaa KCMC, 24 tukabaki nao hapa na leo asubuhi 22 wameruhusiwa, lakini wawili bado tupo nao. Tunaendelea kuwafanyia utaratibu, mmoja tunampa rufaa kwenda KCMC na mwingine tupo naye baada ya afya yake kuendelea vizuri," amesema.

Mkuu wa wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema mabaki ya miili ya watu 33 yamepelekwa Hospitali ya KCMC kwa ajili ya kufanyiwa vinasaba.

"Mpaka sasa waliofariki ni 38 na majeruhi 29, kati yao hapa Same wamebaki wawili na wengine wameruhusiwa na hali zao ziko vizuri," amesema.

Miili mingine 33 ya waliofariki, amesema imepelekwa Hospitali ya KCMC na kwamba maiti tano zimetambuliwa na nyingine zimeungua sana na zimepelekwa kufanyiwa DNA.

"Serikali ya Same inawapa pole wananchi wa Same, maana hatuna idadi sahihi ila wale waliofariki ni wale waliokuwa kwenye Coaster. Kwa kweli Mji umezizima, una majonzi, hivyo niombe wenzetu kuendelea kuwa na uvumilivu na watulivu, wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali," amesema.