Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Madarasa, funza vyatishia usalama wa wanafunzi Mwanga

Sehemu ya madarasa yanayotumiwa na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlevo iliyopo katika Kijiji cha Kilomeni, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Shule hiyo ilianza mwaka 1975 lengo la kuokoa wanafunzi waliokuwa wanaenda mbali mrefu kutafuta elimu lakini ujenzi wake unadaiwa ulikuwa chini ya kiwango.

Mwanga. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlevo iliyopo katika Kijiji cha Kilomeni, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wapo hatarini kutokana na uchakavu wa madarasa wanayotumia, kujaa kwa vyoo na kushambuliwa na funza.

Madarasa hayo ambayo hayana sakafu, yamejaa vumbi linalodaiwa kuwa na funza wanaowaingia wanafunzi miguuni.

Pamoja na uchakavu huo, inaelezwa wanafunzi hao wapo pia hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na vyoo wanayotumia kujaa.

Wanafunzi wakiwa darasani katika Shule ya Msingi Mlevo iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital, baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, wamesema tangu shule hiyo ijengwe mwaka 1975 haijawahi kufanyiwa ukarabati wa aina yoyote.

Mmoja wa wazazi, Stela Mcharo amesema mazingira ya wanafunzi kujisomea shuleni hapo si mazuri na baadhi miguu yao huliwa na funza wanaokaa kwenye vumbi la madarasani.

"Mimi ni mzazi ninayesomesha watoto hapa, nasikitika sana kwa hii shule yetu, haina  madirisha wala milango, majengo ya shule ni chakavu, watoto wanaliwa funza,” amesema mzazi huyo.

Mcharo amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan asikie kilio chao. “Watoto wetu wanapata taabu sana, hawana pa kusomea hata hawa walimu ambao wapo hapa wanafundisha pia funza wanawaingia miguuni.”

Alipotafutwa kwa simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zahara Msangi aliomba apewe muda kwenda kuangalia hali ilivyo katika shule hiyo na kwamba leo mchana na timu yake imeelekea kuangalia hali ilivyo katika shule hiyo.

Madarasa, funza hatari kwa wanafunzi shuleni

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Samora Temba ambaye alihitimu shuleni hapo mwaka 1987 amesema hajawahi kuona mabadiliko katika shule hiyo tangu ijengwe.

"Hili ni tatizo na kama hiki kilio chetu kitafika mahali husika, tutashukuru sana. Kwa Tanzania ya leo watoto kuliwa funza ni aibu, wanateseka sana, watoto hawasomi kwa raha, hiki chumba nimekisomea mimi tangu mwaka 1987 kipo hivyo hivyo," amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilomeni, Joseph Msangi amekiri kuwepo kwa uchakavu wa miundombinu ya shule hiyo na kwamba mara kadhaa wamekuwa wakitafuta wafadhili kuibuka changamoto za hapa na pale.

"Nimepambana na uongozi wa halmashauri ya  kijiji na diwani wa kata hii angalau tupate fedha au wafadhali wa kutusaidia kujenga hii shule  kwa sabau siku zote imekuwa ni chakavu, lakini bado kuna changamoto zinazojitokeza," amesema.

Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya shule hiyo, Diwani wa Kata ya Kilomeni Mohammed Mgala, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo lakini hakuna kinachotekelezeka.

"Shule hii ilianza mwaka 1975 wakati wa UPE (elimu ya msingi kwa wote) ili kuwezesha wanafunzi kwenda shule, kwa hiyo ilijengwa kwa taratibu ambazo si za viwango na ndio imetufikisha hapa tulipo.

“Tunashukuru Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kujenga shule hii lakini haijengwi, mwaka jana shule hii  ilipewa Sh50 milioni, mwaka huu imepewa Sh67 milioni kwa ajili maboresho mbalimbali lakini haijengeki," amesema Mgala ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo.

"Shule imepewa fedha za vyoo zaidi ya Sh10 milioni lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika," ameongeza Mgala, bila kufafanua fedha hizo zimekwenda wapi.