Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walia uchakavu wa madarasa shuleni

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Sinde, Manispaa ya Lindi, wakiwe kwenye darasa ambalo sakafu yake imepasuka.

Muktasari:

  •  Ni shule ya msingi Sinde, Mkurugenzi akiri changamoto ipo akiahidi ukarabati kufanyika mapema iwezekanavyo

Lindi. Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Sinde katika Manispaa ya Lindi, wameiomba Serikali iwaboreshee madarasa kutokana na uchakavu wa madarasa wanayotumia sasa.

 Wakizungumza na Mwananchi shuleni hapo leo Februari 3, wanafunzi hao wamesema madarasa yao yamekuwa ni chakavu,  hayana madirisha, sakafu imeharibika na mvua zinaponyesha madaftari yao yanalowana kutokana na bati kuvuja.

 "Madarasa yetu ni mabovu yapo yanayovuja na kwenye sakafu saruji imebanduka na mengine hayana madirisha. Tunapokuwa darasani na mvua ikinyesha ikatukuta tunaandika maji yanaingia ndani madaftari yanaloa," amesema Rashidi Abdallah,  mwanafunzi shuleni hapo.

 Kwa upande wake, Hithamu Hamisi ambaye pia ni mwanafunzi katika shule hiyo,  amesema wanaomba msaada Serikali iwape bati, iwaboreshee madarasa ili wasomee katika mazingira mazuri.

  "Mvua zinaponyesha madarasa yanavuja tunalazimika kusogeza madawati mbele tunajibana bana hata mwalimu akiwa anafundisha tunashindwa kumuelewa vizuri, "amesema mwanafunzi huyo.

 Akizungumzia uchakavu huo, Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Mohamedi Mlaulau amesema mazingira kama hayo ya uchakavu wa miundombinu,  yanashindwa kumvutia mwanafunzi.

 "Hili eneo linatakiwa liwe na mvuto lakini mwanafunzi akishafika hapa madarasa yanavuja, sakafu mbovu, madawati mabovu inaondoa mvuto kwa mwanafunzi anaona ni kama adhabu. Unaweza ukawa unafundisha ukasikia dawati limeanguka watoto wako chini wakati mwingine wanaumia" amesema Mohamedi.

 Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele amekiri kuwapo kwa uchakavu wa miundombinu katika shule hiyo, akisema  imewekwa katika mipango ya mwaka wa fedha ujao ili ujenzi wa miundombinu yake ufanyike.

 "Shule ya Msingi Sinde ni miongoni mwa shule kongwe zilizopo manispaa na inakumbwa na uchakavu, zipo jitihada tunazozifanya tutapeleka mifuko 100 ya saruji pia tutapeleka fedha kwa ajili ya kumlipa fundi ili kuanza kukarabati katika yale maeneo ambayo yana athari zaidi na mpango mkubwa ni kuanza kujenga madarasa kidogo kidogo kwa kutumia fedha zetu za ndani,” amesema Mnwele.