VIDEO: Foleni yawatesa madereva bandarini Dar

Muktasari:
Madereva wa malori walia na foleni ya bandarini, wadai wanakaa hadi siku tatu kusubiri kuingia
Dar es Salaam. Madereva wa malori yanayopandisha na kushusha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania wamelalamikia foleni iliyokithiri katika kazi hiyo.
Madereva hao wameeleza kuwa kutokana na foleni hiyo wanalazimika kukaa hadi siku tatu kusubiri kuingia bandarini.
MCL Digital imefika katika eneo hilo leo Alhamisi Septemba 5, 2019 na kukuta msururu wa malori kutoka eneo la Uhasibu hadi bandarini ikiwa ni umbali wa kilomita nne huku madereva wakiwa wamekata tamaa.
Akizungumzia hilo Nahad Kimela ambaye ni dereva amesema ana siku ya tatu yupo kwenye foleni hiyo na hana matumaini ya kuingia ndani siku ya leo.
“Kwa kweli tunashindwa kuelewa hii foleni chanzo ni nini, siku hizi imekuwa kawaida, kinachotupa wakati mgumu msururu mrefu hata haijulikani nani anapakia nani anashusha,” amesema
Kilio kama hicho kimetolewa na Hemed Juma aliyeeleza kuwa yupo kwenye foleni hiyo tangu asubuhi ya jana.
“Tunapata wakati mgumu niko hapa tangu jana na hii sasa imekuwa kawaida, wala hakuna taarifa yoyote kwamba kuna kitu kuna shida hatuelewi shida nini kama ni utendaji au system,” amesema
Jitihada za kupata uongozi wa bandari ili kuelezea chanzo cha foleni hizo zinaendelea baada ya leo kukwama kupatikana.