Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uvunjaji mikataba unavyoitafuna nchi

Muktasari:

  • Mwananchi, limedokezwa katika kipindii cha miaka mitano (2015-2020) Tanzania imejikuta katika migogoro na kampuni kadhaa  za wawekezaji kutoka nje, zinazodai fidia ya   mabilioni  baada ya  Tanzania kudaiwa kuvunja mikataba.

Moshi/Dar. Wakati mijadala ya Tanzania kutakiwa kulipa mabilioni ya fedha baada ya kushindwa kesi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID) ikiendelea, wanasheria wataja sababu za mashauri hayo na njia bora za kuepuka.

Miongoni mwa sababu hizo ni wanasheria wabobevu kutohusishwa katika majadiliano na kuingiwa mikataba kati ya Serikali na wawekezaji.

Mwananchi, limedokezwa katika kipindi cha miaka mitano (2015-2020) Tanzania imejikuta katika migogoro hiyo na wawekezaji kutoka nje kutokana na hatua ilizochukua katika sekta mbalimbali.

Sababu nyingine ni kutozingatiwa kwa utawala wa sheria, ukiukwaji wa sheria katika kuvunja mikataba na kasoro za kikatiba ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchagiza Tanzania kushitakiwa na hata kushindwa kesi katika Mahakama za Kimataifa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wa zamani, Fredrick Werema aliliambia Mwananchi uamuzi wa pupa ya kuvunja mikataba bila kuzingatia ushauri wa AG.
Miongoni mwa majukumu ya AG ni kuishauri Serikali juu ya masuala yote ya kisheria ikiwemo mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania ni sehemu ya mkataba ama ina masilahi katika mkataba hiyo.

Ofisi hiyo inayoongozwa na Dk Eliezer Feleshi ina Divisheni ya mikataba na makubaliano ya kimataifa na ndiyo divisheni inahusika na kutoa ushauri na kuendesha majadilano kwa niaba ya Serikali katika Mikataba yote inayoingiwa.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia alisema moja ya sababu za kushtakiwa nje ni kukosekana utawala wa sheria utakaowezesha mahakama za ndani kutoka haki bila kuangalia huyu ni Serikali au sekta binafsi.

Wanasheria na mawakili wengine wamekuwa na hoja zinazoshabihiana na kupingana kuhusu ubobevu wa wanasheria wa Serikali, huku Tundu Lissu akisema kinachotokea sasa ni jambo alilitahadharisha ndani ya Bunge mwaka 2016/2017.

Mijadala mizito imeibuka katika mitandao ya kijamii na katika baadhi ya vyombo vya habari baada ya Serikali kushindwa kesi katika Baraza la Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICSID) na kutakiwa kulipa Dola milioni 109.

Hukumu hiyo ilitolewa Julai 14 mwaka 2023 na kuitaka Serikali ya Tanzania kuilipa kampuni ya Indiana Resources fedha hizo ambazo ni sawa na Sh260 bilioni za Tanzania ambapo Serikali imekata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Taarifa zilizopatikana wiki iliyopita na kuthibitishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniphace Luhende, zilisema Serikali imeridhia kwa maandishi katika ICSID kwamba itailipa kampuni ya Indiana Resources endapo itashindwa rufaa hiyo.

Hiyo ni moja kati ya kesi kadhaa zilizofunguliwa katika mahakama za kimataifa dhidi ya Serikali ya Tanzania na mwelekeo wa nchi kushindwa mfululizo katika kesi zilizotolewa maamuzi siku za karibuni ndio ambao inaibua mijadala mitandaoni.

Kwa mujibu wa ICSID, Serikali bado inakabiliwa na kesi 11 za madai ya fidia zilizosajiliwa katika mahakama hiyo, ikiwemo iliyofunguliwa Julai 27,2020 na kampuni ya Winshera Gold Corporation na Montero Mining & Exploration Ltd.
Kabla ya uamuzi huo, tayari Serikali imeshakiri kuanza kulipa fidia ya Dola 165 za Marekani, sawa na Sh380 bilioni kwa kampuni ya Eco Energy Group iliyoshinda kesi dhidi ya uamuzi wa Serikali wa kuipokonya hatimiliki ya hekta 20,400 Bagamoyo.


Kauli ya AG Feleshi

Akizungumza na Mwananchigazeti hili, Dk Feleshi alisema si kwamba Serikali inashindwa kesi nyingi kama inavyodhaniwa na wengi na kueleza kuwa shida si wanasheria na utaalamu wao na kusisitiza mkataba ni mapatano.

“Kwamba hadi unafikiwa uamuzi wa kwenda mahakamani kunakuwa na jambo ambalo pande mbili hazikuelewana. Mkataba ni mapatano unatengeneza assumptions (mawazo) kwa sababu unayeingia naye anaweza kufariki,"alisema.

Dk Feleshi alisema hilo, ndilo linalosababisha kuwepo na vipengele vya mabadiliko katika mikataba na kusema kinachoshangaza ni watu kuona majadiliano ya kutatua migogoro ya mikataba ni kitu kipya bali ni suala la uelewa.


Alichokisema Jaji Werema

Kwa upande wake, AG wa sita wa Serikali ya Tanzania, Jaji Frederick Werema ametaja sababu zinazosababisha serikali kujikuta kwenye wakati mgumu katika mahakama za usuluhishi akisema kila shauri linatofautiana na lingine.

Jaji Werema ambaye amekuwa AG kuanzia Oktoba 20,2009 na Desemba 16, 2014 alisema changamoto nyingine ni kutofanya uchambuzi wa kina wa mradi kabla ya kuamua kuwekeza na kutowahusisha wajuzi na wabobezi katika kuhakiki miradi.

"Wataalamu wakihusishwa watachambua hatari na kuzigawa lakini kwa kuwa hawazingatii hilo, baadaye mnaona mkataba haulipi au huyo (mwekezaji) hana uwezo wa kuutekeleza," alisema.
Werema aliongeza, wanasheria wanalalamikiwa kuwa sehemu ya tatizo lakini yeye ana maoni tofauti katika hilo.

 "Mkataba ni hatua ya mwisho ambayo inapaswa kuzingatia kilichoonekana kwenye uchambuzi wa kiuchumi wa mradi. Sheria pekee haikupi ujuzi. Inabidi usome uchumi pia,”alisisitiza.


TLS, wanasheria wafunguka

Kwa upande wake, Rais wa TLS, Sungusia aliyataja mambo matatu yanayochagiza Tanzania kushtakiwa katika mahakama hizo na hata kushindwa kesi akitaja miongoni mwake ni tatizo la kikatiba na utawala wa sheria.

Alisema Serikali imejiwekea ulinzi wa kisheria katika mahakama zake za ndani, hali inayofanya ikose nguvu ya ushindani katika majukwaa huru ya kimataifa.
“Katika mazingira hayo, ikitokea Serikali inafanya biashara na ikashitakiwa kwenye mahakama inayotoa ushindani wa haki inakosa nguvu ya kushindana hatimaye inashindwa”

Kutibu tatizo hilo, mwanazuoni huyo wa taaluma ya sheria, alisema lazima Serikali iondoe ulinzi wa kisheria iliyojiwekea ikiwemo ule utaratibu wa ili kuishitaki Serikali au taasisi zake inakupasa uandike notisi ya siku 90.

“Huo utaratibu ukomeshwe lakini, sheria inayoikinga Serikali dhidi ya kukamata mali zake hata kama imeshindwa kesi, unapaswa uondolewe,”alisisitiza.

"Kwa kuwa hapa ndani imejiwekea mipaka ya kujilinda, na ulinzi huo haufai nje ya mipaka, ndio maana watu wakishinda kesi wanasubiri ndege zetu nje hakuna wigo wanazikamata," alisema na kupendekeza serikali iache kufanya biashara.

Wakili huyo alitaka wanasheria wa Serikali wasilaumiwe katika hilo huku akisema wanasiasa wamekuwa wakivunja mikataba ovyo bila kufuata sheria ndiyo maana kunakuwa na ugumu wa kushinda kwa kuwa kisheria wewe ndio mkosaji.

upande wake, wakili Kiongozi wa kampuni ya Haki Kwanza Advocates, Aloyce Komba alisema kinachokosewa ni kuingia mikataba ambayo masharti yake ni vigumu kutekeleza kwa mujibu wa sheria mpya za madini au za uwekezaji.

Kiini kingine kulingana na wakili huyo, ni Serikali kukiuka vipengele muhimu vya mkataba na kutolea mfano katika kutoa leseni, utozaji kodi na masuala ya umiliki ardhi kwamba hapo si rahisi kushinda kesi katika mahakama yoyote.

“Lakini pia mara nyingi kuna hili la kukosa wanasheria wabobevu wa sheria za mikataba ya biashara au uwekezaji hususan wa kampuni za kigeni. Wakili Mkuu wa Serikali ashirikishe mawakili wazawa wa kujitegemea,”alisema Komba.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora alieleza sheria za kiuchumi mikataba iingiwe kwa majadiliano na ukitokea mkwamo utatuliwe kwa majadiliano.

Akizungumza na gazeti hili jana, mwanasheria Tundu Lissu alisema suala la Tanzania kujiingiza kwenye hatari ya kushtakiwa na kudaiwa fidia kubwa alilisema bungeni mwaka 2016/2017 na watanzania watafakari tangu atahadharishe ni kesi ngapi zimefunguliwa.


Imeandikwa na Daniel Mjema (Moshi) na Juma Isihaka na Tuzo Mapunda (Dar)