TPA yafungua ofisi Malawi, yaahidi neema

Muktasari:
- Katika kurahisisha huduma za kibandari katika Tanzania na Malawi, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), leo Jumatatu Desemba 18 imefungua ofisi yake katika mji wa Lilongwe katika taifa hilo jirani.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imefungua ofisi yake nchini Malawi ikilenga kuongeza ufanisi na kuimarisha biashara ya bandari kati ya mataifa hayo mawili.
Ofisi hizo zimefunguliwa leo Jumatatu, Desemba 18, 2023 Mjini Lilongwe tukio lililohudhuriwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Malawi, Jacob Hara na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.
Katika hafla hiyo, Mbossa amesema miongoni mwa majukumu yatakayofanywa na ofisi hiyo ni kutoa taarifa muhimu kuhusu mizigo inayoingizwa Malawi kupitia bandari ya Mbamba-bay na Kyela.
“Itasaidia katika kuhakiki gharama za bandari kabla ya malipo kukamilika, kufuatilia madai yanayoweza kutolewa na wateja kutokana na uharibifu unaoweza kujitokeza katika bandari ili kutolewa haraka kwa fidia.
“Ofisi hii ya TPA itawasaidia wateja kufuatilia maombi yote na utoaji wa taarifa za kutosha juu ya orodha ya magari ambayo hupigwa mnada kwa kuzidisha muda. Tunafanya hivi ili kuwajulisha na kuwakumbusha wateja wetu juu ya umuhimu wa malipo ya haraka ya gharama za bandari ili kuzuia magari kupigwa mnada,” amesema Mbossa.
Mbossa amewahakikishia wananchi wa Malawi kuwa TPA itaendelea kuboresha huduma zake ili kujenga uhusiano bora wa kibiashara na wafanyabiashara wa Taifa hilo.
Amesema TPA itahakikisha wafanyabiashara wa Malawi wanafikia malengo na mipango kwa kutumia bandari za Tanzania ikiwemo ya Dar es Salaam.
Naye, Waziri Mbarawa amesema uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Malawi umesaidia kwa kiasi kikubwa TPA kufungua ofisi katika nchini humo huku akiwahimiza wafanyabiashara wa Taifa hilo waendelee kutumia huduma na kunufaika na uwepo wa ofisi za TPA.
“Hii ni ishara ya uhusiano wenye nguvu wa pande zote kati ya Malawi na Tanzania na jukumu letu la pande mbili la kuwezesha mtiririko wa biashara kati ya nchi zetu mbili. Biashara kati ya Tanzania na Malawi inakua kwa kasi, mwaka 2022/2023, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia mizigo ya tani 610,507 ya Malawi.
“Kutokana na ukuaji huu, Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na TPA kuhusu kutafuta njia bora ya kuboresha vifaa vya bandari itakayokuwa bora ya kuhudumia soko la Malawi,” amesema Profesa Mbarawa
Kwa upande wake, Waziri Hara ameipongeza Tanzania kufungua ofisi hiyo, nchini Malawi ikiwa ni sehemu moja ya utekelezaji wa mkataba wa umoja wa nchi za ushoroba wa kati.
“Hii dalili nzuri mlioiweka katika ushirikiano wa kikanda utakaowezewesha na mataifa yasiofungana na bandari kama Malawi kunufaika. Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa Malawi, kuwezesha usafirishaji mizigo na katika siku za hivi karibuni imekuwa ni eneo kuu la kupitisha mizigo.
“Umuhimu wa kuwa na ofisi ya TPA nchini hapa kutawezesha usafirishaji wa bidhaa kwa urahisi. Ufunguzi wa ofisi za TPA ni hatua muhimu itakayoifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa lango la mauzo na uagizaji wa bidhaa za Malawi,” amesema Hara.